Wanafunzi wa shule ya msingi Loiborsiret Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wameondokana na adha ya ukosefu wa madawati baada ya kukabidhiwa madawati 60 na kampuni za Tanzania Bundu Safaris na Rungwa Game Safaris.

Hivi karibuni, wanafunzi wa shule hiyo, pia walikabidhiwa madawati 100 na diwani wa kata hiyo ya Loiborsiret Ezekiel Lesenga (Maridadi) ambaye alidhibitisha kwa vitendo adhma yake ya kuona tatizo la madawati linamalizika.

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Mahmoud Kambona, akizungumza jana wakati akipokea madawati hayo 60 kwa mkurugenzi wa kampuni ya Bundu Safaris na Rungwa Game Safaris, alisema huu ni wakati wa jamii ya wafugaji kupata elimu.

Kambona aliwataka wazazi wa jamii ya wafugaji wa eneo hilo kutumia fursa ya kuwepo kwa madawati hayo kwa kuwahimiza wanafunzi wasome kwa bidii ili wapate elimu bora itakayowasaidia kwa siku za usoni kwani elimu ndiyo hazina.

“Nimetembelea shule nyingi za msingi kwenye hii wilaya yangu lakini sijaona shule yenye maktaba kama yenu hivyo hongereni, ila wazazi mjitahidi kuwapa chakula wanafunzi wanaotoka mbali ili wasome vizuri,” alisema Kambona.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa kampuni hizo, Harpreet Brar alisema hiyo siyo mara ya kwanza kusaidia jamii inayozunguka eneo hilo kwani alishachangia sh10 milioni za ujenzi wa maabara na kusomesha wanafunzi wawili kila mwaka.

Brar alisema pia katika kuhakikisha anaendelea kusaidia jamii ya eneo hilo alishatoa sh500,000 za ujenzi wa choo, alitoa madawati 75 na chakula kwenye shule ya Namelock na ataendelea kushirikiana kwenye suala maendeleo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro Jackson Sipitieck alitoa wiki mbili kwa uongozi wa kata ya Loiborsiret, kuhakikisha wanajenga nyufa zilizojitokeza kwenye baadhi ya madarasa ya shule hiyo.

“Sisi jamii ya wafugaji ni matajiri mno kwani tuna mifugo mingi sasa itakuwa jambo la kushangaza kusikia eti darasa limeanguka na kusababisha matatizo kwa watoto wetu, hivyo mkarabati haya madarasa,” alisema Sipitieck.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Mahmoud Kambona (kushoto) na Mkurugenzi wa kampuni za Tanzania Bundu Safaris na Rungwa Game Safaris, Harpreet Brar, wakiwa na moja kati ya madawati 60 yaliyotolewa na kampuni hiyo kwenye shule ya msingi Loiborsiret.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Mahmoud Kambona (kushoto) na Mkurugenzi wa kampuni za Tanzania Bundu Safaris na Rungwa Game Safaris, Harpreet Brar, wakifurahia jambo baada ya kampuni hiyo kugawa madawati 60 kwenye shule ya msingi Loiborsiret
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Mahmoud Kambona (kushoto) akimpa mkono wa pongezi Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Lucas Mweri, baada ya kumkabidhi madawati 60 ya shule ya msingi Loiborsiret yaliyotolewa na Mkurugenzi wa kampuni za Tanzania Bundu Safaris na Rungwa Game Safaris, Harpreet Brar.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...