Na.Aron Msigwa- MAELEZO.

Serikali imesema kuwa katika mwaka wa fedha 2016/2017 itatekeleza mradi wa ujenzi wa mfumo mpya wa uondoaji na usafishaji wa majitaka yanayozalishwa katika jiji la Dar es salaam ili kuliweka jiji hilo katika hali ya usafi na kuongeza wastani wa huduma hiyo kutoka asilimia 10 ya sasa hadi asilimia 30 ifikapo mwaka 2017.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amesema mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Korea ya Kusini na Serikali ya Tanzania kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 89.

Amesema mradi huo utahusisha upanuzi wa miundombinu ya maji taka kwenye maeneo ya katikati ya jiji, ujenzi wa miundombinu mipya ya kupitishia maji hayo katika maeneo ya Ilala, Magomeni hadi Ubungo pamoja na maeneo ya Sinza, Kinondoni , Mwananyamala, Oysterbay na Masaki.

Maeneo mengine yatakayoguswa na mradi huo jijini Dar es salaam ni Msasani, Kawe, Mbezi Beach, Kurasini,Keko, Chang'ombe, Temeke, Hananasif, Tandale, Kijitonyama, Makumbusho, Mabibo, Ubungo, Manzese, Sandali, Tandika na Miburani.Mhandisi Lwenge amesema mradi huo wa kipekee utahusisha ujenzi wa mitambo mitatu ya kisasa ya kusafisha majitaka katika maeneo ya Jangwani, Kurasini na Mbezi Beach.

Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Korea ya Kusini na Benki ya Dunia itatekeleza mradi wa huduma ya uondoaji wa majitaka na ujenzi wa miundombinu ya uondoaji wa maji ya mvua katika jiji la Dar es salaam ambayo yamekuwa kero kwenye miundombinu ya jiji hilo.

"Serikali tumeanza kutekeleza mpango wa kupanua mfumo wa uondoaji na usafishaji wa majitaka yanayozalishwa na watumiaji maji , usanifu wa awali wa miradi mipya ya majitaka umekamilika,kazi inayoendelea ni usanifu wa kina ili kuweza kupata vitabu vya zabuni na michoro itakayotumika kumpata mkandarasi wa ujenzi" Amesisitiza Mhandisi Lwenge.

Amesema kuwa kupitia mpango huo bomba linalomwaga majitaka baharini litaacha kutumika na badala yake maji hayo yatapelekwa katika mtambo mpya wa kisasa wa kusafisha majitaka utakaojengwa maeneo ya Jangwani ambao pia utasafisha majitaka kutoka maeneo yote ya katikati ya jiji Dar es salaam yaliyo jirani ambapo maji hayo ambayo yatakua yamesafishwa yatauzwa na kutumiwa katika shughuli mbalimbali za upozaji wa mitambo na umwagiliaji.

Amebainisha kuwa katika kulishughulikia tatizo la majitaka jijini Dar es salaam Serikali itajenga mitambo mingine miwili eneo la Kurasini na Mbezi Beach itakayotumika kuzalisha gesi asilia kwa ajili ya kuendeshea mitambo ya kusafishia maji hayo hivyo kupunguza matumizi na gharama za umeme.

Katika hatua nyingine Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amesema katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali itafanya ukarabati na upanuzi wa mfumo wa kusambazia maji safi katika jiji la Dar es salaam.

Ujenzi wa mfumo huo unalenga kuongeza idadi ya wananchi wapya watakaounganishwa na mtandao wa mabomba ya maji safi kutoka Mradi wa Ruvu Juu na ule wa Ruvu Chini ulioigharimu Serikali bilioni 141 ambao sasa maji yake yanaingia katika matanki ya maji yaliyoko Chuo Kikuu Ardhi jijini Dar es salaam.

Amesema kukamilika kwa mradi wa Ruvu Chini na Ruvu Juu mpaka sasa kumeyawezesha baadhi ya maeneo ya jiji hilo yakiwemo ya Segerea, Kimara, Kibangu na Kinyerezi ambayo yalikua na mabomba ya maji maarufu kama mabomba ya mchina kuanza kupata huduma ya majisafi.

Aidha, kupitia miradi hiyo mikubwa Serikali inaendelea kuishughulikia kero ya uhaba wa maji katika maeneo ya Bunju,Mabwepande, Boko,Tegeta,Kunduchi, Mbezi Beach, Mbezi Juu, Salasala, Kawe, Makongo, Mikocheni, Msasani, Masaki, Mwananyamala, Kinondoni, Magomeni, Sinza, Manzese, Ubungo, Mabibo, Kigogo, Buguruni na maeneo yote ya katikati ya jiji hilo.

Mhandisi Lwenge amefafanua kuwa Kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 32.93 kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa mfumo wa kusambaza majisafi katika jiji hilo na kuongeza kuwa wananchi wasiopata huduma ya maji kutoka mtandao wa maji wa DAWASCO wataendelea kuhudumiwa na mradi wa visima vilivyochimbwa.

" Hadi mwezi Machi, 2016 tumechimba visima 52 na kati ya hivyo visima 32 vinatumika kutoa huduma ya majisafi katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam" Amesema Mhandisi Lwenge.

Wakazi wa jiji la Dar es salaam wapatao milioni 4.5 wamekuwa wakipata huduma ya majisafi kutoka chanzo cha Ruvu Chini ambacho kwa siku kinazalisha mita za ujazo 270,000 kwa siku, Mtambo wa Ruvu Juu unaozalisha mita za ujazo 182,000, Mtambo wa mtoni 9000 na Visima Virefu 27,000 na kufanya jumla ya mita za ujazo zinazozalishwa kwa siku kufikia 502,000 kutoka 300,000 za awali.
 Ramani inayoonesha Mpango wa upanuzi wa mfumo wa uondoaji wa majitaka katika jiji la Dar es salaam utakaotekelezwa na Serikali kwa lengo la kuondoa wastani wa uondoaji wa majitaka kutoka asilimia 10 hadi asilimia 30 ifikapo mwaka 2017.

Mtambo mpya wa kusafishia maji katika chanzo cha maji Ruvu chini mara baada ya kukamilika.Mtambo huo sasa unazalisha maji lita milioni 270 kwa siku.
Taswira ya Mtambo wa Ruvu Juu mara baada ya upanuzi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...