Na Felix Mwagara, MOHA

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira amesema fedha za kuwalipa watumishi 597 waliositishiwa mikataba yao katika Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) zipo na watalipwa hivi karibuni.

Rwegasira alisema kiasi cha shilingi bilioni 2.3 zimetengwa kwa ajili ya malipo ya Watumishi hao waliachishwa kazi Machi 7, 2016 ambapo wanaidai Mamlaka mishahara ya miezi mitatu nyuma, malimbikizo ya fedha katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na makato ya fedha za Bima ya Afya.

Akuzungumza na watumishi wa Makao Makuu ya NIDA pamoja na Maafisa Wasajili wa Vitambulisho vya Taifa, jijini Dar es Salaam jana, Rwegasira aliwataka watumishi hao waliositishiwa mikataba yao, wasipotoshwe na mtu yeyote kuhusu kutokulipwa haki zao kwani wapo katika hatua ya mwisho ya kukamilisha taratibu ndogo ndogo kabla ya kuanza kuwalipa.

“Naomba muwaambie waondoe wasiwasi wowote, waache maneno, watulie kwani Serikali ipo makini na fedha tunazo na tutaanza kuwalipa mara tumalizapo taratibu ndogo ndogo zilizobaki.” Alisema Rwegasira.

Aidha, Rwegasira aliwataka watumishi wa Mamlaka hiyo kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha ifikapo Desemba 31 mwaka huu Watanzania Milioni 23 wanatakiwa watambuliwe na kupata namba kabla ya kuanza kupewa Vitambulisho vya Taifa.

Hata hivyo, watumishi hao walimuakikishia Katibu Mkuu huyo, kuwa kazi hiyo ya utambuzi itakamilika kama ilivyopangwa na itafanyika kwa umakini mkubwa kama inavyotarajiwa.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa NIDA, Dk. Modestus Kipilimba alimshukuru Katibu Mkuu huyo kwa kuwatembelea na kuwatia hamasa katika kukamilisha kazi pamoja na kufikisha lengo lao la kukamilisha utambuzi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

“Tunakuahidi Katibu Mkuu kuwa tutatimiza lengo letu na tunakuakikishia tutafanya kazi kadiri ya uwezo wetu tukiongozwa na kauli mbiu ya ‘hapa kazi tu’, alisema Dk. Kipilimba.

Katibu Mkuu Rwegasira alifanya ziara hiyo kwa lengo la kujifunza zaidi shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka, hata hivyo alipata muda wa kuzungumza na watumishi wa Mamlaka hiyo kuhusu masuala mbalimbali ya kiutendaji.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa katika ofisi za Mamlaka hiyo zilizopo katika Jengo la BMTL, jijini Dar es Salaam, jana. Katika hotuba yake, Rwegasira aliwataka watumishi 597 waliositishiwa mikataba yao waondoe hofu kwani hivi karibuni Serikali itaanza kuwalipa fedha zao baada ya taratibu chache za kiutendaji kukamilika.
Afisa Usajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Ansigar Chilemba akitoa maelezo jinsi taarifa za muombaji wa Kitambulisho cha Taifa zinavyohakikiwa, kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira (kulia). Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dk. Modestus Kipilimba. Rwegasira alifanya ziara ya kikazi katika ofisi za Mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam jana.
Afisa Usajili Kitengo cha Ubora wa Kadi, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Jemima Mulokozi (kushoto) akimuonyesha vitambulisho vilivyokamilika vikiwa na ubora unaohitajika, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira (katikati). Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dk. Modestus Kipilimba. Rwegasira alifanya ziara ya kikazi katika ofisi za Mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam jana.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira (wa tano kushoto), Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dk. Modestus Kipilimba (wa tano kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mamlaka hiyo, mara baada ya Katibu Mkuu kumaliza ziara ya kikazi katika ofisi za Mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...