Na Mwandishi Maalum, New York

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Fiji zimekubaliana kuanzisha uhusiano wa kudiplomasia katika ngazi ya Mabalozi.

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, na Mwakilishi wa Kudumu wa Fiji katika Umoja wa Mataifa Balozi Peter Thomson ndio waliotia sahihi hati za kuanzishwa kwa uhusiano huo kwa niaba ya serikali zao katika hafla fupi iliyofanyika siku ya Alhamisi katika Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania.

Fiji inakuwa nchi ya tatu baada ya Malta na Equador ambazo tayari zimekwisha anzisha uhusiano wa kidiplomasia na Tanzania katika ngazi ya Mabalozi. Kama ilivyokuwa kwa nchi hizo mbili hati za makubaliano hayo zitawasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Wakizungumza mara baada ya kubadilishana hati , wawakilishi hao pamoja na kuonyesha kufurahishwa na uhusiano huo, pia walielezea namna gani wanavyoweza kukuza ushirikiano katika masuala mbalimbali yenye maslahi kwa pande hizo mbili hapa Umoja wa Mataifa na nje ya Umoja wa Mataifa.

“ Ni kwa muda mrefu serikali yangu ( Fiji ) imekuwa ikitamani sana kuwa na uhusiano wa Tanzania, labda pengine niongeze kwamba sisi wananchi wa Fiji baadhi ya vizazi vyetu asili yake ni Tanganyika ( Tanzania) kwa hiyo uhusiano huu utaimarisha zaidi siyo tu kutambua na kuthamini kule tulikotoka, lakini pia tunayo mambo ambayo tunaweza kubadilishana uzoefu kwa manufaa ya nchi zetu na watu wake”. Akasema Balozi.

Kwa upande wake, Balozi Tuvako Manongi amemwambia Balozi Thomson kwamba, nchi hizo mbili zimefungua ukurasa mpya. Na akaongeza . “ nimewahi kutembelea Fiji, ingawa ilikuwa ni kwa muda mfupi lakini niliweza kujionea nakujifunza kilimo cha kisasa na endelevu na pia zao la nazi ambalo hata kwetu ( Tanzania) ni moja ya zao muhimu sana, kwa niyo ninaamini kwamba kwa kuanzisha uhusiano huu tunayo mengi ya kujifunza kutoka kwetu.”

Jamhuri ya Fiji ni Kisiwa kilichoko katika Bahari ya Pacific ya Kusini ( South Pacific Ocean) na lilikuwa koloni la Uingereza kabla ya kujipatia uhuru wake mwaka 1970. Uchumi wa nchi hiyo pamoja na mambo mengine, unaendeshwa kwa kiasi kikubwa na sekta za utalii, madini, bidhaa za misitu, uzalishaji wa sukari, mazao yatokanayo na nazi, pamoja na viwanda vidogo vya pamba na pia Fiji inatengeneza nguo…..
Wawakilishi wa Kudumu wa Tanzania na Fji katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi na Balozi Peter Thomson, wakitia sahihi Hati za kuanzisha Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Nchi hizo Mbili katika nganzi ya Mabalozi. Hafla hiyo fupi ilifanyika siku ya Alhamisi katika Ofisi za Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania. Kushoto kwa Balozi Manongi ni Afisa wa Uwakilishi Bi, Tully Mwaipopo akimwelekeza Balozi sehemu ya kuweka sahihi yake.
Balozi Tuvako Manongi na Balozti Peter Thomson wakipongezana mara baada ya kubadilishana hati za kuanzishwa kwa ushirikiano wa kidiplomasia katika ngazi ya Mabalozi. Hati hizo zitawasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
"Unajua baadhi ya raia wa Fiji walitoka Tanganyika, kwa hiyo hii ni hatua muhimu sana kwetu ya kuwa na uhusiano wa kidiplomasia na Tanzania" hiyo ilikuwa ni kauli ya Balozi Thomson akimweleza Balozi Manongi na kuwafanya waangue kicheko cha furaha.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...