Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki atembelea watumishi katika ofisi zao.

Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wameaswa kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili kuongeza ufanisi kwenye maeneo yao ya kazi. 

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) alipokuwa anatembelea ofisi za watumishi hao jijini Dar es Salaam jana asubuhi. 

”Nimekuja kuwatembelea katika maeneo yenu ya kazi ili nijionee mazingira mnayofanyia kazi pamoja na changamoto zinazowakabili ili kwa pamoja tutafute namna ya kuzitatua”. Mhe. Mahiga aliwaeleza watumishi hao kila ofisi aliyopita.

“Lengo la ziara yangu kwenu ni kuwatia morari ili mfanye kazi kwa bidii na kwa ubunifu wa hali ya juu ili tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea kwa mwaka huu wa fedha 2016/2017. Kutimia kwa Malengo ya taasisi moja moja kama yetu ndiyo itapelekea kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa awamu ya pili ambayo imejikita katika uwekezaji wa viwanda”.

Alisema watumishi hawana budi kufanya kazi kwa bidii na kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuwa Serikali yao chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imejipanga kuboresha maslahi yao. Alisema dhamira hiyo imedhihirishwa na kitendo cha Rais Magufuli kupunguza kodi ya mapato (payee) kutoka asilimia 11 hadi 09.

Aliwataka watumishi kuepuka vitendo vya ubadhirifu badala yake kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni za utumishi na kuonya kuwa, Serikali haitamvumilia mtumishi yeyote atakayebainika kwenda kinyume na maadili ya utumishi.

Waziri Mahiga aliendelea kuwaeleza watumishi wake kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ambayo inajukumu la kuratibu Sera ya Mambo ya Nje ya Nchi ina mchango mkubwa wa kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa na jina zuri na kubwa ulimwenguni kote ili sifa hiyo itumike vizuri kuvutia uwekezaji wa viwanda nchini. 

“Alisema kwa nafasi zenu nyie watumishi mlio hapa Makao Makuu na wale wa Balozini lazima mshirikiane kwa pamoja kwa kutumia taaluma zenu na vipaji alivyowapa Mwenyezi Mungu kuzitangaza rasilimali za Tanzania ulimwenguni kote, kwa madhumuni ya kuvutia uwekezaji na utalii ili kuongeza mapato ya Serikali na ajira kwa Watanzania”.

Alihitimisha nasaha zake kwa kuwakumbusha watumishi kaulimbiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya “Hapa kazi tu” Alisema kauli hiyo lazima itafsiriwe kivitendo kwa kila mtumishi bila kusahau kuweka mbele uzalendo na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu.
Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Dar es Salaam, 23 Juni 2016.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...