Na
Veronica Simba – Sikonge
Imeelezwa kuwa nishati ya umeme kwa wananchi sasa
ni muhimu sawa na ilivyo kwa chakula.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard
Kalemani aliyasema hayo kwa nyakati tofauti hivi karibuni (Julai 27), katika
vijiji vya Kiloleli na Mole, wilayani Sikonge mkoani Tabora, alipokuwa katika
ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini awamu ya pili
maarufu kama REA II.
Akifafanua kuhusu ulinganifu wa umeme na chakula kwa
wananchi, Dkt Kalemani alieleza kuwa, mwananchi anayepata umeme, ana uhakika wa
kuishi maisha mazuri yanayojumuisha afya njema na maendeleo kwa kila nyanja.
“Bila umeme, hakuna maendeleo kwa jamii. Huduma
zote muhimu kwa binadamu, ili ziwe katika viwango stahiki, zinahitaji umeme.
Afya, elimu, biashara na vingine mvijuavyo, vinahitaji umeme ili vifanyike kwa
ubora. Hivyo basi, kama ilivyo muhimu kwa binadamu kupata chakula ili aishi,
ndivyo ilivyo muhimu kuwa na umeme ili kuwa na uhakika wa maisha bora,”
alisisitiza.
Dkt Kalemani alieleza kuwa, kutokana na umuhimu
huo wa nishati ya umeme kwa wananchi, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali
ukiwemo wa Umeme Vijijini (REA) ili kuhakikisha huduma hiyo muhimu inapatikana
kwa watanzania wote hata wale walio vijijini.
Aidha, alisema kwamba, Serikali haitasubiri mtu
ajenge nyumba ya kiwango fulani ndipo aunganishiwe umeme bali kila mwananchi
ataunganishiwa huduma hiyo hata kama nyumba yake ni duni.
“Serikali inatambua kuwa siyo kila Mtanzania ana
uwezo wa kujenga nyumba bora kwa kuwa tunatofautiana kipato. Hivyo, nyumba duni
haitakuwa sababu ya kuzuia mwananchi husika kuunganishiwa umeme. Zoezi la
kuunganisha umeme litaendelea wakati wananchi wakiendelea kuboresha makazi yao
ili umeme uwasaidie kuinua vipato vyao.”
Kuhusu suala la vijiji ambavyo havikuunganishiwa
umeme katika Mradi wa REA Awamu ya Pili, Naibu Waziri alieleza kuwa vijiji
hivyo vyote vitapatiwa umeme katika Awamu ya Tatu (REA III) ya Mradi husika
ambayo inatarajiwa kuanza rasmi utekelezaji wake mwezi Septemba mwaka huu.
Alisema kuwa, uzoefu uliopatikana kutokana na
utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili umebainisha kuwa hakukuwa
na ushirikiano mzuri baina ya wasimamizi wa Mradi na viongozi mbalimbali katika
ngazi za Wilaya, Halmashauri na Vijiji ambako Mradi husika ulikuwa
ukitekelezwa, hali iliyosababisha baadhi ya maeneo muhimu kurukwa pasipo
kupatiwa huduma hiyo.
Naibu Waziri alieleza kuwa, kutokana na uzoefu
huo, Serikali imedhamiria, katika Awamu ya Tatu ya Mradi, kuwashirikisha
ipasavyo, viongozi katika ngazi hizo, ambao ndiyo wanafahamu vema maeneo yao
ili wabainishe maeneo ya vipaumbele kwa ajili ya kupatiwa nishati ya umeme.
Katika hatua nyingine, Dkt Kalemani aliwataka
watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuendelea kutoa elimu kwa
wananchi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo ili kuwaepusha
wateja wao kutapeliwa na matapeli maarufu kama ‘vishoka’ ambao hutumia fursa ya
uelewa mdogo wa wananchi.
Miongoni mwa mambo muhimu ambayo Naibu Waziri aliagiza
wananchi wapewe elimu ni pamoja na umuhimu wa kutunza miundombinu ya umeme na
bei halisi ya umeme wa REA.
Alitoa onyo kwa wale wanaohujumu miundombinu ya
umeme kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao endapo watabainika
kufanya hivyo kwani wanarudisha nyuma jitihada za Serikali kuwaletea wananchi
wake maendeleo.
Naibu Waziri anatarajia kuhitimisha ziara yake
mwishoni mwa mwezi huu katika Mkoa wa Geita. Mikoa ambayo amekwishaitembelea
katika ziara hiyo ni Dodoma, Iringa, Rukwa, Katavi na Tabora.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa
Tabora ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa huo, Thea Ntala akizungumza na
wananchi wa eneo la Kiloleli wilayani Sikonge mkoani humo hivi karibuni wakati
wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani kukagua
utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Pili.
Mbunge wa Sikonge,
George Kakunda (kushoto) akimweleza jambo Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Dkt Medard Kalemani (katikati), wakati wa ziara ya Naibu Waziri wilayani humo
hivi karibuni kukagua utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Pili. Kulia kwa
Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Peres Magiri.
Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (wa pili kutoka kushoto) akiwakabidhi
viongozi wa Wilaya ya Sikonge, kifaa kinachotumika kuunganisha umeme pasipo
kutumia nyaya za kawaida za kuunganishia kijulikanacho kitaalam kama ‘Ready
Board’ au UMETA (Umeme Tayari), wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha
Kiloleli wilayani humo hivi karibuni.
Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (kushoto), akikagua mtambo unaotumika
kusukuma maji kwa ajili ya matumizi ya wakazi wa Wilaya ya Sikonge mkoani
Tabora hivi karibuni. Mtambo huo uliopo katika eneo la Utyatya, hutumia mafuta
ya dizeli ambayo ni gharama kubwa. Eneo hilo ni mojawapo ya maeneo
yanayotarajiwa kuunganishiwa umeme wa REA Awamu ya Tatu na hivyo kuondoa kabisa
changamoto hiyo. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Peres Magiri.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...