Rais Mstaafu wa
Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa leo tarehe 27 Agosti, 2016
ameadhimisha Jubilei ya Dhahabu ya Miaka 50 ya Ndoa yake na Mama Anna Mkapa
katika kanisa la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay Jijini Dar es Salaam.
Hafla ya Jubilei
hiyo imefanyika nyakati za mchana katika ukumbi wa Kardinali Rugambwa uliopo
kando ya kanisa la Mtakatifu Petro-Oysterbay na imetanguliwa na Misa ya
shukrani iliyofanyika katika kanisa hilo majira ya asubuhi.
Jubilei hiyo
imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli, Makamu wa Rais
Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais Mstaafu wa Awamu ya Sita wa Zanzibar Dkt. Amani Abeid Karume, Mke
wa Baba wa Taifa Mama Maria Nyerere, Mawaziri Wakuu Wastaafu Mhe. Cleopa Msuya,
Dkt. Salim Ahmed Salim, Jaji Joseph Warioba na Mhe. Edward Lowassa.
Misa Takatifu ya
Shukrani imeongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha Mhashamu
Askofu Josephat Lebulu na kuhudhuriwa na Maaskofu na Maaskofu Wakuu saba
akiwemo Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp
Kardinali Pengo.
Akizungumza baada
ya kumalizika kwa Misa Takatifu Rais Magufuli amempongeza Rais Mstaafu Benjamin
William Mkapa kwa kutimiza miaka 50 ya ndoa na ameeleza kuwa ndoa hiyo
iliyowaunganisha wanandoa wanaotoka katika madhehebu tofauti ya Kikristo imetoa
fundisho kubwa kuwa binadamu wanapaswa kuwa wamoja hata kama wana tofauti
mbalimbali zikiwemo za kimadhehebu ya dini, siasa na kanda.
Rais Magufuli
amesema miaka 50 ya ndoa ya Mhe. Benjamin William Mkapa ambaye ni Muumini wa
Kanisa Katoliki na Mkewe Mama Anna Mkapa ambaye ni Muumini wa Kanisa la
Kilutheri inawafundisha watanzania wote hususani wanasiasa kuishi kwa upendo na
kuilinda amani waliyonayo na ametoa wito kwa viongozi dini kuendeleza juhudi
zao za kuliombea taifa na kuwaunganisha wananchi licha ya tofauti walizo nazo.
Kwa upande wake
Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa pamoja na kuwashukuru
Viongozi wote, ndugu, jamaa na marafiki waliohudhuria Misa ya Shukrani na
Jubilei hiyo ya miaka 50 ya ndoa yake amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuijaalia
ndoa yake umri mrefu.
Rais Mstaafu Mkapa
pia ametoa wito kwa watanzania kupenda na kushirikiana huku akibainisha mafunzo
aliyoyapata kutoka kwa viongozi wa dini kuwa "Kila mmoja ni zawadi kwa mwenzake"
Nae Askofu Mkuu wa
Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amempongeza
Rais Mstaafu Mkapa na Mkewe Mama Anna Mkapa kwa kuadhimisha miaka 50 ya ndoa na
amewasihi watanzania kuiga mfano mwema uliooneshwa na wana ndoa hao ambao
wamedumu katika imani bila kuyumba.
Kardinali Pengo
amesema ndoa ya Rais Mstaafu Mkapa anaifundisha jamii kuwa tunaweza kuishi kwa
imani zetu bila kubadili dini.
Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Petro Fr. Stephano Kaombwe akiongoza Ibada ya ukumbusho wa
ahadi za ndoa wakati wa Misa ya Jubilei ya Dhahabu (miaka 50) ya ndoa ya Rais
Mstaafu Mhe Benjamin Mkapa na Mama Anna Mkapa katika kanisa la Mt. Petro
jijini Dar es salaam leo Jumamosi Agosti 27, 2016
Rais Mstaafu Mhe Benjamin Mkapa na
Mama Anna Mkapa wakipokea hati maalumu kutoka kwa Baba Mtakatifu Francis toka kwa Askofu Mkuu
wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo wakati
wa Misa ya Jubilei ya Dhahabu ya ndoa ya Rais Mstaafu Mhe Benjamin
Mkapa na Mama Anna Mkapa katika kanisa la Mt. Petro jijini Dar es salaam
leo Jumamosi Agosti 27, 2016
Rais Mstaafu Mhe Benjamin Mkapa
akitoa shukurani wakati wa Misa ya Jubilei ya Dhahabu ya ndoa yake na
na Mama Anna Mkapa katika kanisa la Mt. Petro jijini Dar es salaam leo
Jumamosi Agosti 27, 2016
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akitoa salamu zake za pongezi
wakati wa Misa ya Jubilei ya Dhahabu ya ndoa ya Rais Mstaafu Mhe
Benjamin Mkapa na Mama Anna Mkapa katika kanisa la Mt. Petro jijini Dar
es salaam leo Jumamosi Agosti 27, 2016
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli katika picha ya pamoja viongozi
wa dini na viongozi wastaafu na wake zao wakati wa Misa ya Jubilei ya
Dhahabu ya ndoa ya Rais Mstaafu Mhe Benjamin Mkapa na Mama Anna Mkapa
katika kanisa la Mt. Petro jijini Dar es salaam leo Jumamosi Agosti 27,
2016
Rais Mstaafu Mhe Benjamin Mkapa na
Mama Anna Mkapa wakikata keki katika hafla ya chakula cha mchana
waliyoandaa baada ya Misa ya Jubilei ya Dhahabu ya ndoa yao katika
kanisa la Mt. Petro jijini Dar es salaam leo Jumamosi Agosti 27, 2016.
Kwa picha zaidi BOFYA HAPA
Kwa picha zaidi BOFYA HAPA
CHUKI HUFUNGA AKILI INAZUIA UBUNIFU WOWOTE WA MBINU, VIONGOZI HAWANA NAFASI YA KUCHUKIA, VILE VILE VIONGOZI KUMBUKENI, UKWELI UNATABIA MOJA NZURI SANA, HAUJALI MKUBWA WALA MDOGO, HAUJALI ADUI WALA RAFIKI, KWAKE WOTE NI SAWA.
ReplyDeletePICHA ZENU ZIMEKAA VIZURI, ZINAONYESHA AMANI SANA TENA SANA,MUNGU IBARIKI TANZANIA.
DR, JAMESSY