Jumuiya ya Madhehebu
ya Dawoodi Bohra imetoa mchango wa Dola za Marekani laki mbili na nusu (Usd. 250,000)
sawa na Shilingi Milioni Mia Tano Arobaini na Tano za Kitanzania (Ths.
545,000,000) kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lilitokea
katika Mkoa wa Kagera tarehe 10 Septemba, 2016.
Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Bohra Duniani Dkt. Syedna
Mufaddal Saifuddin amekabidhi mchango huo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, walipokutana na kufanya Mazungumzo leo
tarehe 13 Oktoba, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Kati ya fedha hizo
Dola za Marekani laki moja (Usd. 100,000) zimetolewa na Dkt. Syedna Mufaddal
Saifuddin mwenyewe, Dola za Marekani laki moja (Usd. 100,000) zimetolewa na
Viongozi wengine wa Madhehebu ya Bohra na Dola za Marekani Elfu Hamsini (Usd.
50,000) zimetolewa na wana Jumuiya ya Bohra wa Tanzania.
Pamoja na kutoa
mchango huo, Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin ameahidi kuwa Jumuiya hiyo ambayo
inamiliki hospitali kubwa zilizopo maeneo mbalimbali duniani ikiwemo India,
itajenga hospitali hapa nchini kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu.
Pia Dkt. Syedna
Mufaddal Saifuddin ameahidi kuwa Jumuiya ya Bohra itatoa udhamini wa masomo ya
udaktari kwa vijana wa Tanzania na pia itadhamini matibabu kwa wagonjwa 20
watakaopelekwa nchini India kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Kwa Upande wake
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amemshukuru
Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin na Jumuiya nzima ya Dawoodi Bohra kwa mchango
walioutoa kwa waathirika wa tetemeko la ardhi Mkoani Kagera na pia kwa kufanyia
mkutano wao wa mwaka hapa nchini uliowaleta wageni takribani 31,000 kutoka
mataifa mbalimbali duniani.
“Dkt. Syedna
Mufaddal Saifuddin nakushukuru sana kwa kuja hapa nchini kwetu na kutuletea
mkutano huu mkubwa, ujio wenu umeimarisha uhusiano kati ya Bohra na Tanzania na
pia umechangia uchumi wa nchi yetu.
“Nakushukuru pia
kwa nia yenu ya kujenga hospitali hapa nchini, kuwasomesha madaktari na
kudhamini matibabu ya wagonjwa huko India, naomba nikuhakikishie kuwa mchango
mlioutoa utatusaidia sana na pia mkijenga hospitali na kufundisha madaktari
mtakuwa mmesaidia kuokoa fedha nyingi ambazo Serikali ingetumia”
amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais
Magufuli amewaalika wanajumuiya ya Dawoodi Bohra kuja kuwekeza hapa nchini
katika sekta mbalimbali zikiwemo viwanda, kilimo, usafirishaji, madini na uvuvi
na amewahakikishia kuwa Serikali itawaunga mkono wote watakaokuwa tayari kuja
kuwekeza Tanzania.
Jumuiya ya
Madhehebu ya Dawoodi Bohra Duniani imeadhimisha mwaka mpya wa Kiislam na
kumbukumbu ya kifo cha Mjukuu wa Mtume Muhammad (S.A.W) aitwaye Imamu Hussein
ambapo maadhimisho yake ya kidunia yaliyoambatana na tamasha la zaidi ya wiki
mbili yamefanyika hapa nchini kuanzia tarehe 01 Oktoba, 2016 hadi tarehe 11
Oktoba, 2016.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es
Salaam
13 Oktoba,
2016
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakipokea mfano wa hundi ya dola za kimarekani 50,000 ukiwa msaada wa Jumuiya ya Bohora Dar es salaam kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera toka kwa Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Dawoodi Bohora duniani Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 13, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakiwa katika dua na Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Dawoodi Bohora duniani Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin na ujumbe wake Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 13, 2016
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakimshukuru Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Dawoodi Bohora duniani Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin na ujumbe wake Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 13, 2016 .
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakiwa katika picha ya pamoja na Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Dawoodi Bohora duniani Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin na ujumbe wake Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 13, 2016
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakiagana na Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Dawoodi Bohora duniani Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin na ujumbe wake Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 13, 2016.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...