Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa
ametoa muda wa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la
Ndege Tanzania (ATCL), kufanya mabadiliko katika menejimenti ya Shirika
hilo ili kuongeza ufanisi na kuboresha utendaji kazi.
Ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza katika
mkutano wa Menejimenti pamoja na wafanyakazi wa Shirika hilo na
kuwataka kutoa huduma bora ili kulifanya Shirika hilo kuwa miongoni mwa
mashirika bora ya ndege barani Afrika.
“Nataka ndani ya mwezi mmoja uwe umeshafanya mabadiliko katika
menejimenti, mabadiliko lazima yaanzie juu kwanza kwa watoa maamuzi
na ishuke hadi kwa wafanyakazi wazembe na wasio waadilifu”, amesema
Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa Menejimenti na Wafanyakazi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri Mbarawa amepinga nyongeza ya mshahara kwa wafanyakazi wa
Shirika hilo hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali ipo katika juhudi za
kulifufua na kuliimarisha Shirika hilo.
Aidha Waziri Mbarawa ameitaka Idara ya Masoko ya shirika hilo
kuzunguka katika taasisi zote zilizo chini ya Wizara yake na kuzishawishi
kuweza kutumia huduma za usafiri wa anga wa ATCL.
“Serikali imekamilisha upande wake wa ununuzi wa ndege, sasa kazi
inabaki kwenu, sitaki watu wa masoko kukaa ofisini”, amesema Prof.
Mbarawa.
Ameongeza kuwa wafanyakazi wa ATC wanatakiwa kujipanga kutoa
huduma iliyotukuka kwa wateja wake ili kuweza kuhimili ushindani uliopo
katika mashirika ya ndege nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Eng. Ladislaus Matindi akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani), wakati Waziri huyo alipokutana na menejimenti ya shirika hilo pamoja na wafanyakazi wake jijini Dar es Salaam.
“Inabidi tofauti kubwa ionekane kati yenu na mashirika mengine, yeyote
ambaye anaona hawezi kutoa huduma bora kwa mteja atafute sehemu
nyingine kwani hapa hatufai ”, amesisitiza Waziri Mbarawa.
Profesa Mbarawa amelitaka shirika hilo kutumia mfumo wa kisasa wa
kukata tiketi kwa njia ya simu na kompyuta ili kuwarahishia watumiaji wa
shirika hilo kuweza kupata tiketi kwa haraka na urahisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Eng. Ladislaus
Matindi amemhakikishia Waziri Mbarawa kufanyia kazi maagizo aliyotoa na
kuahidi kuboresha utendaji kazi wa shirika hilo kwa lengo la kuteka soko la
ushindani wa usafiri wa anga nchini.
“Kwa sasa tumeanza vizuri na naamini uwezo wa kuzalisha faida zaidi
tunao, tunaahidi kuboresha utendaji kazi ili kuendana na kasi ya mabadiliko
ya Serikali ya Awamu ya Tano”, amesema Eng. Matindi.
Wafanyakazi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), wakimsikiliza Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (hayupo
pichani), alipozungumza na uongozi wa Shirika hilo na Wafanyakazi jijini
Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa
akimpongeza mmoja wa watoa huduma wa ndege za ATCL kwa utoaji wa
huduma bora kwa wateja katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...