Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Wawekezaji na wananchi wa Jamuhuri ya Cuba wana nafasi nzuri ya kutumia mlango wa uwekezaji uliofunguliwa na Zanzibar katika kuanzisha miradi mipya kwenye Sekta ya Utalii hapa Nchini.

Alisema mpango huo ambao licha ya kuimarisha uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya Zanzibar na Cuba tokea Uhuru wa Mataifa hayo Mawili lakini pia utaongeza ushirikiano wa pande hizo zinazofanana katika Historia zake.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati wa mazungumzo yake na Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Bwana Jorge Luis Lopez aliyefika kumuaga rasmi baada ya kumaliza muda wake wa kazi hapa Nchini.Alieleza kwamba Cuba imekuwa mshirika mkubwa wa harakati za maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar hasa katika kusaidia Taaluma ya Sekta za Afya na Kilimo chini ya Muasisi wa Taifa hilo Marehemu Fidel Castro.

Balozi Seif alisema mafungamano hayo kwa sasa yanapaswa kuelezwa nguvu zake katika Sekta ya Utalii inayoonekana kushamiri zaidi hivi sasa Ulimwenguni na kuleta mapato makubwa yanayochangia Mataifa mbali mbali ambayo tayari yamekwisha wekeza kwenye miradi hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuomba Balozi Jorge Luis licha ya kumaliza muda wake wa Kidiplomasia hapa Tanzania lakini bado ana nafasi ya kuisaidia Tanzania na Zanzibar kwa ujumla katika kuzitangaza Kiutalii kwa wawekezaji wa Nchi yake wakati atakaporejea nyumbani.

Aliishukuru Serikali ya Cuba kwa juhudi kubwa iliyochukuwa katika kusaidia maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar ambao katika maisha yao yote ya baadaye wataendelea kuzikumbuka juhudi hizo.Balozi Seif alifahamisha kwamba wataalamu wengi wa Cuba hasa wale wa Sekta ya Afya waliowahi kutoa Taaluma kwa vijana na Wananchi tofauti wa Zanzibar ni mfano halisi wa juhudi hizo.

Mapema Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Bwana Jorge Luis Lopez alisema kwamba uhusiano wa Kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na Cuba utaendelea kama kawaida licha ya mabadiliko ya watendaji wanaosimamia uhusiano huo.Balozi Lopez alimuhakikishia Balozi Seif kuwa mrithi wa kuchukuwa nafasi yake anayetarajiwa kuingia Nchini Tanzania wakati wowote kuanzia sasa ni Mwanadiplomasia mzoefu mwenye upeo wa kuzifahamu Siasa na mazingira ya Mataifa ya Bara la Afrika.

Bwana Lopez alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba wazo lake la kumuomba kuitangaza Zanzibar atakaporejea nyumbani kwake atalifanyia kazi ipasavyo ili kuweka kumbu kumbu nzuri wa uwepo wake wa kazi Nchini Tanzania.

Balozi wa Cuba Nchini Tanzania Bwana Jorge Luis Lopez ambae mapema alikutana kwa Mazungumzo na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Zubeir Ali Maulidi anarejea Nyumbani baada ya kumaliza muda wake wa kazi wa Miaka Minne hapa Tanzania.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Balozi wa Cuba Nchini Tanzania Bwana Jorge Luis Lopez aliyefika Ofisini kwake Vuga kumuaga rasmi baada ya kumaliza muda wake wa kazi Nchini Tanzania.
Balozi Seif akibadilishana mawazo na Balozi wa Cuba Nchini Tanzania Bwana Jorge Luis Lopez aliyefika kuaga rasmi akimalizia utumishi wake wa Kidiplomasia Nchini Tanzania.
Nakukabidhi Picha hii tuliyopiga siku ya kwanza wakati nakukaribisha Zanzibar ulipoanza kazi yako ya Ubalozi. Picha hiyo walipiga pamoja miaka Minne iliyopita.
Balozi Seif akimkabidhi Mlango Balozi wa Cuba Bwana Jorge Lopez kama kumbu kumbu ya kukaribishwa tena Zanzibar wakati wowote atakapopenda.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...