Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, James Ihunyo amewataka vijana wenye ulemavu kuchangamkia fursa zitolewazo na Serikali pamoja na wadau mbalimbali ili ziwasaidie kuboresha maisha yao.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Kilombero ameyasema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hii juu ya ushiriki wa walemavu katika Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) unaoratibiwa na shirika la Plan International.

Mhe. Ihunyo amesema asilimia kubwa ya vijana wenye ulemavu wamekosa nafasi ya kupata elimu na wengine wameishia njiani hivyo ili kuwafanya wawe sawa na vijana wengine Halmashauri ina wajibu wa kuwapatia mafunzo ya ufundi ili waweze kujiajiri na kujipatia vipato vitakavyowawezesha kujitegemea na kupunguza utegemezi kwa kiasi kikubwa.

“Katika maeneo mbalimbali nchini walemavu wamekuwa wakitengwa na wengine kufichwa ndani ikiaminika kuwa hawawezi kufanya shughuli yoyote, kwa kupitia mradi wa YEE unaoratibiwa na shirika la Plan International ninawaomba vijana walemavu kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa hiyo,”alisema Mhe. Ihunyo.

Ameongeza kuwa tangu mwaka 2015 mradi ulivyoanzishwa jumla ya vijana 1376 wameshapatiwa mafunzo chini ya mradi huo lakini vijana wenye ulemavu ni 13 tu ambayo ni sawa na asilimia 3 kati ya asilimia kumi iliyopangwa katika mradi huo hivyo vijana walemavu wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kwani mradi huo una manufaa katika maisha yao.

Aidha, Mhe. Ihunyo ametoa wito kwa watendaji wa Serikali za Vijiji, Kata na Vitongoji kujitahidi kuwaibua vijana walemavu ili waweze kupatiwa mafunzo yatakayowasaidia kuimarisha maisha yao pamoja na Taifa kiujumla.

Amefafanua kuwa Serikali inashirikiana na Shirika hilo katika kutoa maeneo ya kufundishia pamoja na kutoa mikopo inayotumika kama mitaji ya kuanzishia shughuli mbalimbali kwa vijana wanaohitimu mafunzo hayo.

Kwa upande wake mzazi wa kijana mwenye ulemavu, Menhad Limota amelishkuru shirika hilo kwa kuweza kuwapatia vijana hao mafunzo ya ufundi pamoja na ushauri wa kitaalamu ambao umewawezesha kufanya shughuli zao zinazowasaidia kupata fedha za kujikimu.

“Miaka ya nyuma kabla mwanangu hajapatiwa mafunzo alikuwa akinitegemea mimi kwa kila kitu lakini baada ya mafunzo hayo ameweza kujiunga na walemavu wenzie na kuanzisha shughuli mbalimbali ambazo kwa namna moja au nyingine zinamsaidia yeye pamoja na sisi wazazi wake,”alisema Limota.

Mradi huo wa miaka mitatu 2015 hadi 2018 unatekelezwa kwa ushirikiano wa mashirika ya VSO, CCBRT, VETA, UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya Tanzania huku ukiratibiwa na Shirika la Plan International chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...