Na
Lydia Churi
Mahakama, Tanga
Mahakama ya Tanzania imeshauriwa kuwa na Mpango
endelevu wa kuwajengea uwezo watumishi wake wa ngazi zote ili waweze kufanya
kazi zao kwa ufanisi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya
Tanga Mhe. Imani Abood (pichani) alitoa ushauri huo leo jjini Tanga alipokuwa akielezea
utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama ya Tanzania katika
Kanda yake.
Alisema pamoja na kuwa Mahakama inaendesha mafunzo
mbalimbali kwa watumishi wake lakini mafunzo hayo hayana budi kutolewa kwa
watumishi wote kuanzia ngazi ya chini mpaka ngazi ya juu kabisa katika
Mahakama.
Akizungumzia nguzo ya pili ya Mpango Mkakati wa Mahakama
inayohusu upatikanaji wa haki kwa wakati, Mhe. Abood alisema ni muhimu suala la
mafunzo likapewa kipaumbele hasa kutokana na kukua kwa sayansi na Teknolojia.
Alisema , hivi sasa katika Mahakama upo ushahidi wa kielekitroniki unaotolewa
hivyo ni muhimu mafunzo yakatolewa ili kuleta ufanisi katika suala zima la
utoaji wa haki.
Akizungumzia mikakati iliyowekwa na kanda yake ili
kuondosha mashauri mahakamani kwa wakati, Jaji Abood alisema wanakusudia
kuziwekea umeme Mahakama za Mwanzo kupitia Mradi wa REA na kuwapatia Mahakimu
wote katika kanda yake vitendea kazi kama vile laptops na printer ili
ziwarahisishie kutoa hukumu kwa wakati.
Alisema hivi sasa Mahakimu katika Mahakama za Mwanzo
hulazimika kupeleka hukumu walizoandika kwa mkono ili zikachapishwe kwenye Mahakama
za wilaya ambapo kuna umeme.
Alisema licha ya changamoto hizo, bado watumishi wa
Mahakama Kuu kanda ya Tanga wanakuwa wakifanya kazi kwa bidii na Mahakimu kuhakikisha
hukumu zinatolewa kwa wakati ikiwa ni pamoja na na wananchi kupatiwa nakala za
hukumu ndani ya siku 21 zilizopangwa.
Mkakati mwingine uliowekwa ili kuondosha mashauri
mahakamani ni pamoja na, kufanya vikao na Mahakimu wafawidhi wa wilaya pamoja
na wadau wa Mahakama ili kurahisisha kazi kwa kuwa kila mdau anaposhughulikia
eneo lake shauri huisha mapema.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...