WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema viongozi wa mataifa ya Afrika wamekubaliana kufungua
fursa za kiuchumi baina ya nchi hizo pamoja na kuweka utaratibu wa kutumia hati
moja ya kusafiria.
Alitoa kauli
hiyo jana (Jumatano, Machi 22, 2017)
wakati akingumzia makubaliano yaliyofikiwa katika uzinduzi wa Jukwaa la Uchumi
Barani Afrika (AEP) uliofanyika nchini Mauritius Machi 20 hadi 21, 2017. Waziri
Mkuu alimuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli.
Waziri Mkuu
alisema viongozi hao wamekubaliana kwamba mataifa ya Afrika yawe na hati moja
ya kusafiria, ambayo itawawezesha wananchi kuingia nchi yoyote ndani ya bara
hilo bila ya vikwazo kwa lengo la kurahisisha muingiliano wa watu na bidhaa.
Alisema jambo
jingine walilokubaliana ni kuimarisha Jumuiya zao ikiwemo ya Afrika Mashariki
(EAC), Jumuiya ya Soko la
Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na kuzishawishi
nchi nyingine ambazo hazijajiunga kujiunga jumuia hizo.
Alisema viongozi
hao walijadili namna watakavyoweza kuinua uchumi na kuweka mikakati ya
kuimarisha viwanda, ambapo Tanzania ipo katika nafasi nzuri kwa kuwa tayari
inatekeleza mpango wa kukuza uchumi wake kwa kupitia sekta ya viwanda.
“Viwanda ndiyo mkombozi wa changamoto
mbalimbali barani Afrika ikiwemo ya ajira, hivyo Serikali ya awamu ya Tano
imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ili kuongeza ajira na kuondoa umaskini miongoni
mwa wananchi wake,” alisema.
Jukwaa hilo lilizinduliwa Machi 20,
2017 na Waziri Mkuu wa Swazland Bw. Barnabas Sibusiso Dlamini kwa niaba ya Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) na Rais wa Chad, Idriss Deby. Pia Bw. Dlamini alimuwakilisha Mfalme Muwsati wa III.
Bw. Dlamini alisema nchi za Afrika
zinatakiwa kuboresha mitaa yake na kujikita katika kutoa elimu ya masuala ya
sayansi na viwanda ili kuwajengea wanafunzi uelewa wa masuala hayo angu wakiwa
na umri mdogo.
Alisema iwapo wanafunzi wataanza
kujifunza masuala ya viwanda kuanzia shule watakuwa na uelewa wa kutosha wa
masuala hayo jambo ambalo litawarahisishia kupata ajira katika viwanda
mbalimbali, hivyo kuondokana na tatizo la ajira linalozibakili nchi nyingi za
Afrika.
Uzinduzi wa jukwaa hilo ulikuwa na ajenda nne ambazo zilihusu sekta ya
viwanda, kukuza biashara miongoni mwa nchi za Afrika, kukuza ujuzi katika taaluma
mbalimbali na kurahisisha muingiliano wa watu na bidhaa baina ya mataifa hayo.
Jukwaa hilo lilifanyika kwa siku mbili lilihudhuriwa
na viongozi wakuu wa nchi za Afrika, wanazuoni, wafanyabiashara pamoja na watu
kutoka kwenye asasi mbalimbali za kiraia barani Afrika.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, MACHI 23, 22017.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...