WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amepokea taarifa rasmi ya uchunguzi wa kifo cha
Faru John kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele
ambaye alikuwa akiongoza tume maalum iliyoundwa na Waziri Mkuu.
Waziri
Mkuu amepokea taarifa hiyo, leo (Jumatatu, Machi 27, 2017) kwenye
ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es
Salaam.
Akisoma taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Prof. Manyele amesema tume
yake ilifanya uchunguzi wa kifo cha Faru John kwa kupima vinasaba vya
sampuli mbalimbali vikiwemo mzoga, fuvu, mifupa, pembe, damu, ngozi na kinyesi kilichokaushwa ambapo ilibainika kuwa vyote ni vya mnyama mmoja, aina ya faru mweusi ambaye ni dume.
Prof.
Manyele amesema matokeo hayo yamethibitisha kuwa faru John alikufa
katika hifadhi ya Sasakwa Grumeti kwa kukosa matunzo na uangalizi wa
karibu.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali,
Profesa Samwel Manyele taarifa ya Tume aliyoiunda ya kuchunguza suala
la Faru John, ofisini kwake jijjini Dar es salaam Machi 27, 2017. (Picha
na Ofisi ya `Waziri Mkuu)
“Maabara
iliyotumika ni ya Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini chini ya
usimamizi wa timu ya wataalamu kutoka Tanzania, wachunguzi wa Serikali,
chini ya Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Sababu za kifo chake
zilichangiwa na kukosa matunzo na uangalizi wa karibu, kukosa matibabu
alipoumwa, mazoea yanayotokana na kutofuata taratibu zilizowekwa
kisheria na mapungufu ya kiuongozu kwa Wizara husika, hifadhi na taasisi
zake,” amesema.
Prof.
Manyele amesema mapungufu waliyoyabaini kutokana na uchunguzi huo ni
kutokuwepo kwa kibali rasmi cha kumhamisha Faru John; kukosekana kwa
mkataba wa kupokelewa kwa Faru John hifadhi ya Sasakwa Grumeti na
kutofuatiliwa kwa afya na maendeleo ya Faru John baada ya kuhamishwa.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya
kukabidhiwa taarifa ya tume ya kuchunguza suala la Faru John na Mkemia
Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele, Ofisini kwake jijini Dar es
salam Machi 27, 2017.
Mengine
ni uchukuaji holela wa sampuli za wanyama pori kwa lengo la utafiti na
kuzisafirisha nje ya nchi; migongano ya kimaslahi kati ya watumishi
waliolenga kusimamia taratibu na wale wenye kusimamia maslahi binafsi na
uwepo wa taasisi nyingi zenye mamlaka sawa juu ya masuala ya uhifadhi
wa wanyamapori.
“Pamoja
na kwamba mawasiliano yanaonyesha zoezi hilo liliridhiwa na Wizara,
hapakuwepo na kibali rasmi kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori cha
kuruhusu kumhamisha Faru John kutoka NCAA kwenda Grumeti,” amesema Prof.
Manyele katika ripoti yake.
Akizungumzia
kuhusu uchukuaji holela wa sampuli za wanyama pori kwa lengo la utafiti
na kuzisafirisha nje ya nchi, Prof. Manyele amesema kumbukumbu za
watafiti na aina ya sampuli wanazochukua haziwekwi vizuri na kwamba
tume inashauri TAWIRI na TANAPA wapewe msisitizo juu ya umuhimu wa
kuzingatia majukumu yao.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Mkemia Mkuu wa Serikali , Profesa
Samwel Manyele wakati alipowasilisha taarifa ya tume ya uchunguzi wa
suala Faru John baada ya kukabidhi taarifa hiyo , Ofisini kwa Waziri
Mkuu jijini Dar es salaam Machi27, 2017.
Amesema
kuna umuhimu wa kudhibiti watafiti na tafiti ili kulinda taarifa muhimu
za vinasaba vya wanyamapori (Genetic information) dhidi ya mataifa
mengine. “TUME inashauri maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ianzishe
kitengo cha Sayansi Jinai na Uchunguzi wa Vinasaba vya Wanyamapori (DNA
Forensic Wildlife Laboratory) ili Serikali na vyombo vyake iweze kufanya
maamuzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata ushahidi wa kimahakama
katika kesi za jinai zinazohusu wanyamapori (Expert Witness).
Akizungumza
na waandishi wa habari mara baada ya kusomewa ripoti huyo, Waziri Mkuu
aliishukuru timu ya uchunguzi iliyokuwa chini ya Mkemia Mkuu wa Serikali
kwa kazi iliyoifanya ikiwemo kuainisha udhaifu uliokuwemo ndani ya
Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake.
“Ofisi
yangu itaipitia taarifa hii ambayo ni kubwa kiasi na kuifanyia kazi.
Matokeo ya kazi hiyo, tutayatoa hivi karibuni ili kuonyesha Serikali
imeamua kufanya nini juu ya mapendekezo yaliyotolewa.”
Alimtaka
Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa
Wanyamapori, Bw. Robert Mande, afuatilie mapendekezo yaliyoainishwa na
tume hiyo na wayafanyie kazi mapema iwezekanavyo.
Waziri Mkuu aliiunda tume hiyo Desemba 10, mwaka jana baada ya kupokea pembe mbili za faru John na taarifa yenye nyaraka zilizotumika
kumhamisha faru huyo. Hatua hiyo ilifuatia agizo alolitoa Desemba 6,
2016, akiwa ziarani mkoani Arusha, ambapo alitoa siku mbili na kuutaka
uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote
zilizotumika kumhamisha faru John kutoka kwenye hifadhi hiyo.
Alitoa
agizo hilo alipotembelea ofisi za makao makuu ya NCAA zilizoko wilayani
Ngorongoro, mkoani Arusha na kuzungumza na watumishi wa mamlaka hiyo
pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya
kikazi mkoani humo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...