Wapalestina kila mwaka hunaadhimisha siku ya mateka inapofika tarehe 17 April kila mwaka, kufuatia kupitishwa kwa Azimio la Bunge la Palestina mwaka 1974 katika vikao vyake vya kawaida, kwamba siku ya tarehe 17 April ni siku ya kitaifa ya kuwaenzi mateka na hatua yao ya kujitoa muhanga. Hilo ni kuzingatia kuwa ni siku ya kupangilia mambo muhimu na kuunganisha juhudi mbalimbali, pia ni siku ya kuwakomboa, kuwasaidia na kuunga mkono haki yao ya kuwa huru.

Aidha ni siku ya kuwakirimu na kusimama nao na hata jamaa zao, kama ilivyokuwa ni siku ya kuwaenzi pia waliopoteza maisha katika juhudi za kitaifa.Tokea siku hiyo imekuwa na inaendelea kuwa siku ya mateka wa kipalestina ni siku rasmi, wanayoadhimisha wapalestina nchini humo na maeneo mengine duniani na kwa namna mbalimbali.
Suala la mateka linazingatiwa ni miongoni mwa masuala muhimu na yenye uzito mkubwa kwa taifa la Palestina, hilo ni kutokana na ukubwa wa kujitolea muhanga kulikofanywa na mateka wa kipalestina, katika kufanikisha uhuru na ukombozi wa taifa lao la Palestina kutokana uvamizi wa kimabavu wa Israel. Taasisi za mambo ya mateka na wakombozi wa kipalestina, klabu ya mateka na Taasisi kuu ya takwimu, katika ripoti yao ya pamoja ya mwaka huu zimetaja idadi ya wapalestina waliotekwa ambao wapo katika jela za Israel,wanafikia zaidi ya 6500, wakiwemo wanawake 57 na watoto 300.

Aidha ripoti hiyo ya pamoja, imetaja pia uwepo wa taasisi zinazojihusisha na haki za binaadamu zilizo rasmi, ambazo zimeorodhesha pia zaidi ya mateka laki moja (100,000) tokea mwaka 2000, huku zaidi ya watoto elfu kumi na tano (15,000) walio chini ya umri wa miaka kumi na nane (18), wanawake elfu moja na mia tano (1,500), mawaziri wa zamani na manaibu wao wapatao (70).Kipindi ambacho serikali ya Israel tayari imetoa maazimio zaidi ya elfu ishirini na saba (27,000) ya kukamatwa bila ya tuhuma na kuwekwa ndani bila ya kuhukumiwa.

Kwa mujibu wa ripoti ya pamoja, wameripotiwa zaidi ya watu milioni moja waliokamatwa, katika kipindi cha uvamizi wa kimabavu tangu kianze mnamo mwaka 1948, ripoti pia ikiongezea kusema kwamba serikali hiyo ya Israeli ilizidisha ukamataji tokea mwezi Oktoba mwaka 2015, ukafikisha zaidi ya watu waliokamatwa Ukingoni mwa Magharibi huku wengi wao wakiwa kutoka Jerusalemu.
Ripoti pia imetaja kwamba idadi ya mateka wanawake wa kipalestina wamefikia 57 katika jela za Israel,wakiwemo wasichana wanaoongozwa na mkongwe wao aitwae “Lin Jarbuniy” kutoka katika ardhi inayokaliwa kimabavu tangu mwaka 1948, ambae ameachiwa huru siku ya Jumapili ya jana tarehe 16 April 2017. Ripoti imetilia mkazo ya kwamba, serikali ya Israeli imewakamata watoto wa kipalestina zaidi ya mia tatu (300), huku taasisi mbalimbali zikifuatilia aina mbalimbali ya adhabu na mateso yawapatayo watoto hao wakiwa Jela.

Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya asilimia themanini (80%) ya mateka wa kipalestina wamekumbana na mateso hayo wakati wa uchunguzi, mateso hayo yamefanywa na wanajeshi waisraeli wanaosimamia uchunguzi huo. Aidha kuna aina mbalimbali ya mateso hayo wanayofanyiwa mateka wa kipalestina katika Jela hizo za Israeli, ikiwemo kuzuiliwa kulala, kuvuliwa nguo wakati wa usiku, kupigwa, kutikiswa na kadhalika ukiacha mateso ya kinafsi na kukamatwa bila ya tuhuma na kuwekwa ndani bila ya kuhukumiwa.

Hukumu inatolewa bila hata ya kutakiwa kukiri au kuthibitisha kosa, huku ikifikia idadi ya watu mia tano (500), waliokamatwa bila ya tuhuma na kuwekwa ndani bila ya kuhukumiwa. Ukiongezea kitendo cha serikali ya Israeli kubomoa nyumba zaidi ya mia mbili na thelathini (230) za mateka wa kipalestina, kama ni sehemu ya hukumu yao kwa kujiingiza kwao katika mapambano ya kisiasa yanayolenga kuleta ukombozi na uhuru wa nchi yao ya Palestina.

Aidha wengine wapatao thelathini na tano (35) wametengwa mjini Gaza, huku vikosi vya Israeli vikiwashambulia kinyume cha sheria mateka wengine wa kipalestina zaidi ya elfu moja na mia tano (1,500), baada ya kuwakamata.

Vile vile wapo mateka wa kipalestina zaidi ya elfu moja (1,000) wanasumbuliwa na magonjwa sugu mbalimbali hawapati matibabu, huku wengine zaidi ya mia moja na themanini (180) wakipoteza maisha tangu mwaka 1967 na familia za kipalestina zaidi ya elfu mbili haziwezi kuwatembelea watoto wao, kwa sababu ya zuio la kijeshi. Aidha mateka wengine wapatao mia tatu na sabini (370), bado wapo katika Jela za Israeli tokea kabla hata makubaliano ya Oslo mwaka 1993, wakiwemo ishirini na moja waliokaa zaidi ya miaka ishirini (20) hawajatoka hadi leo.
Kwa upande mwingine, kufuata mnasaba huu zaidi ya mateka wa palestina ndani ya Jela za Israeli wametangaza mgomo wa kula, wakitaka kuboreshewa hali ya Jela walipo na hali zao za kibinaadamu. Hatua hiyo ya kutangaza mgomo inakwenda sambambana maadhimisho ya Siku ya Mateka wa kipalestina ambayo ni 17 April kila mwaka.

Kwa mnasaba huu, Ubalozi wa Palestina nchini Tanzania unatilia mkazo ya kwamba, suala la mateka na wote waliotiwa nguvuni waliopo katika Jela na kambi za Israeli, ni katika masuala muhimu mno yanayoshughulikiwa na utawala wa Palestina, katika ngazi ya kikanda na kimataifa kwa mtazamo wake wa kisiasa, kitaifa na kibinaadamu.

Jambo ambalo ni wajibu lipewe umuhimu na wote, kufuatia na kugusa suala hilo haki za msingi za binaadamu, zilizodhaminiwa na sheria, kanuni, desturi na mikataba yote ya kimataifa, hasa ule mkataba wa nne wa Geneva unaohusu haki za binaadamu, tangazo la kimataifa la haki za binaadamu na maazimio mengine mengi pia mikataba ya kimataifa ihusuyo suala hili. 

Ubalozi pia unatilia mkazo ya kwamba, siku ya mateka wa kipalestina imekuja kuukumbusha Ulimwengu mateka hao na wanayokumbana nayo miongoni mwa aina mbalimbali za adhabu na mateso, yanayogusa utukufu wa binaadamu yaliyozidia na  kukiuka mikataba yote ya kimataifa na kibinaadamu,ukiwemo mkataba wa nne wa  Geneva na misingi yote ya haki za binaadamu ambayo nchi zote duniani zimekubaliana kuziheshimu.

Ubalozi  wa Palestina hapa nchini pia kupitia mnasaba huu, unaziomba jumuiya zote  za kimataifa na taasisi za haki za binaadamu, kuibana serikali ya Israeli iache kuwaadhibu mateka wa kipalestina na hatimae kuwaacha huru.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...