IMEELEZWA kuwa, kati ya wateja 48,661 waliolipia huduma ya kuunganishiwa Umeme na  TANESCO kupitia Ofisi yake ya Kanda ya Kaskazini, tayari wateja 43,733 ambao ni sawa na asilimia 89.9 wameshaunganishiwa huduma hiyo kufikia Agosti 31 mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Meneja wa TANESCO, Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Stella Hiza wakati akiwasilisha ripoti kwa Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Profesa James Mdoe kuhusu utekelezaji wa Maagizo ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini aliyoyatoa kwa watendaji wa TANESCO tarehe 2 Septemba, 2017 mjini Dodoma.

Miongoni mwa  maagizo yaliyotolewa na Dkt. Kalemani ni kuhakikisha wateja wote waliolipia huduma ya kuunganishwa Umeme wameunganishwa  ifikapo mwezi Desemba mwaka huu na kubadilisha mita za zamani  na kuweka mita mpya za LUKU kwa wateja wote wa umeme pamoja na kufikisha huduma karibu na wananchi.

Mhandisi Hiza aliongeza kuwa katika wateja  waliounganishiwa Umeme, 35577 walikuwa hawahitaji nguzo na 8156 walihitaji nguzo za Umeme. 

Akizungumzia suala la uanzishwaji wa ofisi ndogo katika kila wilaya ili kusogeza huduma karibu na wateja, Hiza alisema kuwa katika baadhi ya wilaya Ofisi zimekwishaanzishwa na mpaka kufikia Tarehe 31, Agosti mwaka huu, kulikuwa na jumla ya ofisi ndogo 14 katika kanda hiyo. 
Aidha alibainisha kuwa, ifikapo tarehe 1 mwezi Oktoba mwaka huu, wanatarajia kufungua ofisi ndogo nyingine 11 katika Kanda husika.

Kuhusu zoezi la ubadilishaji wa mita kwenda kwenye mfumo wa LUKU, alisema kuwa mkoa wa Manyara umeshabadilisha mita kwa wateja wote na kueleza kuwa jumla ya mita 39,860 zinahitajika ili kukamilisha zoezi hilo ambapo mkoa wa Arusha zinahitajika mita 10,730,   Kilimanjaro mita 23,130 na Tanga mita 6,000.

Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe, aliagiza Watendaji wa TANESCO kufanya kazi kwa bidii na kuwa wazalendo ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma stahiki.

Pamoja na kuipongeza TANESCO kwa kutekeleza majukumu yao,  Prof. Mdoe aliwataka watendaji hao kuwa wabunifu na kutafuta njia  zitakazowasaidia kubaini watu wanaojihusisha na wizi wa Umeme ili kuliwezesha Shirika kupata mapato yake.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini akiwa  katika ofisi ya TANESCO, mkoa wa Tanga. Anayesalimiana naye ni Meneja Wa TANESCO mkoa wa Tanga, Mhandisi Abdulrahman Nyenye na kulia kwake ni Meneja wa TANESCO kanda ya Kaskazini, Mhandisi Stella Hiza.
 Mhandisi Stella Hiza akisoma ripoti ya utekelezaji wa majukumu katika Kikao na Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Prof. James Mdoe.
 Kaimu Katibu Mkuu akisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja wa TANESCO, Mkoa wa Tanga, Mhandisi Abdulrahman Nyenye.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe akizungumza wakati wa kikao chake na Watendaji wa TANESCO,  Kanda ya Kaskazini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...