Na. Thobias Robert- MAELEZO.
Kamati ya utawala ya shindano la tuzo za utekelezaji maendeleo kwa kasi ya juu kwa Wabunge
na Mawaziri imezindua shindano la kutoa tuzo kwa Wabunge na Mawaziri (THSDA)
watakaofanya vizuri katika kutekeleza majukumu ya kuwaletea Wananchi maendeleo.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam leo na Katibu wa Kamati hiyo Bw. Wilson Maage
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, juu ya uzinduzi wa shindano hilo ambalo
litafanyika kwa muda wa miezi miwili.
“Tuzo hizo zimetokana na kuwepo wazo bunifu (intellectual property) ambalo azma yake ni
kuhamasisha utekelezaji wa shughuli za huduma na maendeleo kwa Wananchi wa Tanzania na
kupima kasi ya utekelezaji wa shughuli hizo kwa viongozi wa ngazi mbalimbali katika sekta na
taasisi za kiserikali hapa nchini,” alifafanua Bw. Maage.
Aliendelea kusema kuwa, vigezo vitakavyotumiwa katika kuteua viongozi hao ambao ni
wabunge pamoja na Mawaziri ni pamoja na kuwa mtetezi wa Wananchi wake bila uoga akiwa
ndani au nje ya Bunge, mtendaji bora wa maendeleo yenye kuonekana, sifa ya kutoa hoja zenye
tija kwa kutumia lugha ya staha bila matusi, sifa ya utekelezaji wa haraka apatapo matatizo ya
Wananchi wake pamoja na sifa ya kutetea demokrasia, uhuru na kutetea wanyonge.
“Faida za shindano la tuzo hizi ni kwamba zinaweka Wananchi karibu na viongozi, kuchochea
utekelezaji huduma na maendeleo kwa kasi ya juu, utawla bora na uwajibikaji wa viongozi kwa
Wananchi, uhusiano mzuri kati ya serikali na Wananchi na kuimarisha furaha, utulivu na amani,”
alieleza Bw. Maage.
Kwa uapnde wake Mkurugenzi mkuu wa Kamati hiyo, Bw. Herman Mnenuka alisema kuwa
Wananchi ndiyo nguzo kuu ya kupata kiongozi atakayepata tuzo hiyo kwani wao ndio
watakaopendekeza kwa majina ya wabunge pamoja na wamaziri wanaofaa kuwania tuzo hiyo.
Katika tuzo hiyo, hatua ya kwanza, wananchi wanapaswa kupendekeza wabumge 15 kwa kila
kigezo shindanishi, pia Wananchi watawateua Mawaziri 5 kwa kila kipengele shindanishi
kwaajili ya kuingia kwenye ushindani wa tuzo hiyo na wabunge watano watano na Mawaziri
watatu watakaopata kura nyingi kwa njia ya ujumbe mfupi (SMS) kutoka kwa wananchi
wataingia katika fainali ya king’anyiro kuwania tuzo hiyo.
Aidha aliongeza kuwa, katika hatua nyingine, Wananchi kupitia simu watawachuja washiriki
waliofika hatua ya fainali kwa kutuma SMS na mbunge pamoja na waziri atakayepata kura
nyingi ndiye atakaye kuwa mshindi katika kilele cha tuzo hiyo kitakachofanyika tarehe 23
Desemba Mwaka huu.
“Niwaombe wananchi washiriki kikamilifu ili kuweza kupata kiongozi anayejishughulisha na
anayechapa kazi kupitia tuzo hii na mwisho wa kilele tutapata mshindi wa kila kipengele
kilichowekwa ambacho kina tija muhimu katika taifa kupitia waheshimiwa wabunge na
mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alieleza Bw. Mnenuka.
Aidha aliongeza kuwa, Wananchi watapendekeza majina kwa kutuma ujumbe mfupi simu
kupitia namba 15555 kwa mitandao ya Tigo, Airtel, Vodacom, Halotel Smart na Zantel na kila
SMS itatozwa gharama ya shilingi 500 vilevile kutakuwa na vipindi vya radio runinga na
magazeti ili kuwakumbusha mwenendo na hatua za shindano la tuzo za THSDA hadi siku ya
kilele.
Hizi ni tuzo za kwanza kuandaliwa hapa nchini na kamati hiyo ambazo zitafanyika kwa awamu
kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...