Na Mwandishi Wetu

WAHITIMU wa Shule kongwe ya Sekondari Ndanda iliyopo Masasi mkoani Mtwara, kupitia umoja wao (UWAHISSENDA) wanakusudia kuanzisha kampuni itakayotoa mikopo midogomidogo kwa lengo la kujiimarisha kiuchumi. Hatua hiyo imekuja miaka miwili baada ya wahitimu hao kuanzisha kundi la mtandao wa kijamii la Whatsaap lenye zaidi ya wanaumoja 250, na hivyo hivi karibuni kuazimia pamoja na kuimarisha umoja wao, wafikirie pia kuinuana kiuchumi.

Akizungumza baada ya kikao cha wanaumoja hao hivi karibuni, Kaimu Mwenyekiti wa UWAHISSENDA, Yohana Kasawala alisema dhamira yao itaanza kutekelezwa mapema mwakani baada ya kuwa tayari wameshapata mtaji kutokana na michango ya wanachama. Alisema, pamoja na kukopeshana huku riba ikitumika kutunisha mfuko wa umoja, wanakusudia kutanua wigo wa mikopo hata kwa wasio wanaumoja wa UWAHISSENDA.

Aidha, mipango hiyo ya kuinuana kiuchumi inakwenda sambamba na mpango wa uzinduzi wa umoja huo uliopangwa kufanyika shuleni Ndanda mapema mwakani ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 90 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo. “Daima umoja ni nguvu, utengano ni dhaifu, nasi tumeona ni vyema tukatumia mshikamano huu kama fursa ya kujiimarisha kiuchumi. Tuna ndoto nyingi, lakini kwa kuanzia tunakuja na hili la kampuni ya mikopo midogomidogo yaani Microfince company…

“Wataalamu wetu wa uchumi ndani ya umoja ambao wametapakaa katika taasisi za fedha nchini wametupatia mchanganuo wenye kutia matumaini kwamba tutaweza, na kama mambo yatakwenda hivyo, siku za usoni tunaweza kufikiria hata kuanzisha benki…Ni suala la muda tu,” alisema Kasawala na kuongeza kuwa, umoja una Katiba, umesajiliwa kisheria na kufuata taratibu nyingine za nchi.

Ndanda, shule iliyoanzishwa mwaka 1928, ni miongoni mwa shule kongwe zilizotoa wasomi wengi waliobahatika kushika nyadhifa mbalimbali katika nchi, miongoni mwao akiwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.

Pia wamo Hawa Ghasia, mmoja wa mawaziri waandamizi katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Utawala wa Rais Jakaya Kikwete. Subira Mgalu, Naibu Waziri wa Nishati katika Serikali ya Rais, Dk John Magufuli pia ni matunda ya sekondari ya Ndanda.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...