Na Rhoda James, DSM
Waziri wa Madini Angellah Kairuki mwishoni mwa wiki alikutana na Ujumbe
wa Benki ya Dunia jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufahamiana na
kuangalia hatua mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wa Miradi ya
Madini inayotekelezwa kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali
Madini (SMMRP) unaofadhiliwa na Benki hiyo kwa kushirikiana na Serikali.
Pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa katika kikao hicho, Waziri
Kairuki aliitaka Benki ya Dunia kuona namna ya kuwaendeleza Wataalam
wa Sekta ya Madini ili kuwezesha uwepo wa Watalaam wa kutosha
hususan katika masuala ya Uthaminishaji wa Madini ya Almasi, tanzanite
na madini mengine ya vito na pia masuala ya uongezaji thamani madini
kwa ujumla.
Pia, alishauri umuhimu wa kuboreshwa kwa Mtandao wa Huduma za
Leseni kwa Njia ya Mtandao (Online Mining Cadastre) ikiwa ni pamoja na
kuunganisha mtandao huo na Mamlaka nyingine ikiwemo Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) ili taarifa
zote zinazohusu madini na mapato yatokanayo na madini ziweze
kupatikana kupitia mtandao huo.
Vilevile, aliishauri Benki hiyo kuhusu uuzwaji wa Madini ya Almas kwa njia
ya Mnada kama vile inavyofanyika kwa Madini ya Tanzanite, lengo likiwa ni
kuwezesha Serikali kunufaika na madini hayo.
Aliongeza kuwa, baada ya Serikali ya Tanzania kupitisha Marekebisho ya
Sheria ya Madini kupitia Sheria ijulikanayo kama (The written laws
(Miscellaneous Amendements) Act, 2017), alisema kuwa, baadhi ya
wawekezaji wameonesha wasiwasi kuhusu marekebisho hayo.
Hivyo, Waziri Kairuki amewataka wawekezaji kutokuwa na hofu kwani
mabadiliko hayo yanalenga kuhakikisha kuwa Serikali inanufaika ipasavyo
kutokana na rasilimali zake za madini. Aidha, alisema kwamba, nia ya
Serikali kuhusu kuvutia wawekezaji iko palepale ilimradi wazingatie Sheria
na taratibu.
Vilevile, Waziri Kairuki alieleza kwamba, ni vema Benki ya Dunia ikaangalia
namna bora ya kuhakikisha madini yote ya Tanzanite yanayouzwa nje ya
nchi yanakuwa na Hati ya Uhalisia inayoonyesha chanzo cha madini hayo
suala ambalo litawezesha Taifa kupata mapato stahiki kutokana na
rasilimali hiyo.
Vievile, Waziri Kairuki alizungumzia suala la udhibiti wa utoroshaji madini
na kusisitiza kuhusu kuwepo na namna bora ya kuzuia utoroshwaji wa
madini ya Tanzanite ikiwemo kujulikana kwa idadi ya wachimbaji wadogo,
wa kati, kiasi kinachopatikana na mahali madini hayo yanapouzwa.
Pia, Waziri Kairuki aliishukuru Benki ya Dunia kutokana na ushirikiano
ambao umekuwepo baina ya Serikali kwa kipindi chote na kueleza kuwa,
Serikali iko tayari kutekeleza miradi husika kikamilifu kwa lengo la kukuza
uchumi wa nchi.
BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI
BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...