Na Greyson Mwase, Arusha

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani tarehe 22 Novemba, 2017 alifanya ziara katika kampuni ya kuzalisha transfoma za umeme ya TANELEC iliyopo jijini Arusha lengo likiwa ni kukagua shughuli za kampuni hiyo pamoja na kuangalia namna ya kutatua changamoto katika uzalishaji wa vifaa vya umeme nchini.

Akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt. Kalemani alisema mara baada ya kukagua shughuli za kampuni hiyo na kujiridhisha uwezo wa kampuni hiyo katika uzalishaji wa transfoma, ni wakati wa TANESCO na REA kujipanga upya katika mahitaji ya transfoma za kutosha na kuwasilisha mahitaji hayo kwa kampuni husika na kuongeza kasi ya miradi ya umeme nchini.

Alifafanua kuwa mapema Juni mwaka huu Serikali kupitia Wizara ya Nishati ilipiga marufuku uingizwaji wa nguzo za zege na transfoma ili kuepuka gharama kubwa na tatizo la kuchelewa kwa miradi.

Aliendelea kusema kuwa baada ya kutoa agizo hilo, ameamua kufanya ziara ili kubaini uwezo na mahitaji halisi ya transfoma za umeme ambapo amebaini kuwa kampuni hiyo ina uwezo wa kuzalisha transfoma za umeme 10,000 wakati mahitaji halisi ya transfoma za umeme nchini yakiwa ni 6,500

Alisema kutokana na uwezo mkubwa wa uzalishaji wa transfoma katika kampuni hiyo, ni wakati wa TANESCO na REA kukaa pamoja na kuainisha upya mahitaji ya transfoma za umeme nyingi zaidi ili kuendana na kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme nchini.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati mbele) na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo (kushoto mbele) wakiendelea na ziara katika kampuni ya kutengeneza transfoma za umeme ya TANELEC, iliyopo jijini Arusha. Kulia mbele ni Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Zahir Saleh
Meneja Mkuu wa kampuni ya kutengeneza transfoma za umeme ya TANELEC, Zahir Saleh (kulia) akimwonesha Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani moja ya mifuniko ya transfoma za umeme inayotengenezwa na kampuni hiyo.
Msimamizi wa Idara ya Vyuma, Zakayo Mmbaga (kulia) akionesha jinsi mashine ya kukunja vyuma inavyofanya kazi kwa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa pili kushoto)
Meneja Mkuu wa kampuni ya kutengeneza transfoma za umeme ya TANELEC, Zahir Saleh (kulia) akielezea mafanikio ya kampuni hiyo kwa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa pili kulia mbele). Kushoto mbele ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo
Mafundi wa kampuni ya kutengeneza transfoma za umeme ya TANELEC, wakiendelea na kazi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...