Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetoa msaada wa vitanda vya wagonjwa 24 na vyandarua 24 vyenye thamani ya jumla ya shilingi milioni kumi tano (Tshs.15 milioni) kwa hospitali ya Wilaya ya Mafia ili kupunguza upungufu wa vitanda katika hospitali hiyo na kupambana na ugonjwa wa malaria.
Mbali na msaada huo, TPA imeahidi kusaidia vifaa tiba zaidi ikiwa ni pamoja na meza za wagonjwa, mito ya kulalia pamoja na mashuka ili kusaidia sekta ya Afya Wilayani Mafia. 

Akiongea katika hafla fupi ya kukabidhi msaada huo iliyofanyika hospitalini hapo, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko alisema msaada huo umetolewa kama sehemu ya sera ya misaada ya TPA ambayo imejielekeza katika masuala ya afya, elimu, maendeleo ya jamii na majanga. 

Katika kuunga mkono juhudi za Serikali za maendeleo ya jamii, Kakoko ameahidi kuchangia kiasi cha Tshs. 20milioni kwa ajili ya Kituo cha Afya kipya kitakachojengwa katika Wilaya hiyo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kupokea vifaa hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Mafia Bw. Shaibu Nnunduma aliishukuru TPA kwa msaada huo ambao alisema umekuja wakati muafaka hasa ikizingatiwa kwamba Mafia ni pembezoni na ni mara chache kukumbukwa na wadau kama TPA. 
Nnunduma alisema msaada huo utasaidia sana kupunguza changamoto ya uhaba wa vitanda hospitalini hapo na kuahidi kwamba vifaa hivyo vitatunzwa ili viweze kutumika kwa muda mrefu zaidi.

Naye Mkurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya hiyo, Bw. Erick Mapunda alisema kwamba Serikali imewapatia jumla ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya  cha Wilaya lakini kutokana na jiografia ya Wilaya Mafia ilivyo, upatikanaji wa vifaa hivyo huwa ni wa gharama kubwa sababu maunzi (materials) yote lazima itoke Dar es Salaam na hakuna usafiri wa uhakika wa kuvifikisha Mafia.

Alisema wanaishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho ambacho kitapunguza idadi ya wagonjwa wanaolazimika kwenda hospitali kwa kukosa Kituo cha Afya. Aliishukuru TPA kwa kuunga mkono juhudi za wananchi ambao wataweka nguvu zao katika ujenzi huo na kuwataka wadau wengine kujitokeza ili kusaidia juhudi hizo za Serikali.
Gati la Mafia ni moja kati ya magati yanayomilikiwa na kuendeshwa na TPA ambapo ina uwezo wa kuhudumia vyombo vya abiria na mizigo kisiwani hapo.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko akikabidhi vifaa tiba kwa Mkuu wa Wilaya ya Mafia Bw. Shaibu Nnunduma mjini Mafia.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...