Na Veronica Kazimoto,Iringa

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere amewapongeza Wafanyabiashara mkoani Iringa kwa kuwa na mwitikio mkubwa wa kutumia Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFD) ambazo husaidia kutunza kumbukumbu za mauzo ya wafanyabiashara hao na kurahisisha ukusanyaji mapato ya Serikali.

Akizungumza leo mara baada ya kutembelea baadhi ya maduka na vituo vya mafuta mkoani hapa, Kichere amesema kwamba, mwamko wa matumizi ya Mashine za EFD umeongezeka kwa kiasi kikubwa na wafanyabiashara wengi wanatumia mashine hizo kwa ufasaha.

"Nichukue nafasi hii kuwapongeza wafanyabiashra wa Iringa mjini kwa mwitikio wao mkubwa wa kutumia Mashine hizi za EFD. Nimeona maduka mengi na wafanyabiashara wengi sana wakitumia mashine za EFD katika maduka na vituo mbalimbali vya mafuta hapa mjini," alisema Kichere.

Aidha, Kamishna Mkuu Kichere amewahimiza wafanyabiashara hao na wananchi kwa ujumla kuendelea kutoa na kudai risiti kila wanapofanya mauzo na kununua bidhaa na huduma mbalimbali.Kwa upande wake mfanyabiashara maarufu wa Kampuni ya ASAS iliyopo mkoani hapa, Feisal Abri amesema kuwa, ujio wa Kamishna Mkuu wa TRA ni wa muhimu kwa wafanyabiashara hao kwani huwasaidia kutambua Sheria mbalimbali za Kodi zikiwemo zile zinazohusiana na matumizi ya Mashine za EFD.

"Ujio wa Kamishna Mkuu unatupa nguvu sisi wafanyabiashara na kuona kwamba hatuko peke yetu ila kuna watu wanatufuatilia kwa maana ya kutusaidia kujua Sheria mbalimbali za Kodi. Hivyo, ninaomba utamaduni huu uendelee na uwe wa mara kwa mara," alieleza Abri.Naye, Rehema Shabani mfanyabiasha wa duka la nguo lililopo katika soko la Miyomboni alisema kuwa amefurahishwa sana na ziara ya Kamshina Mkuu wa TRA katika soko hilo kwa sababu amepata fursa ya kumueleza kero na malalamiko yake.

"Nimefurahi sana kumuona Kamishna Mkuu wa TRA kwa sababu nimetoa kero zangu na nimemueleza malalamiko yangu na amewaagiza viongozi wa TRA hapa mkoani kuyafanyia kazi," alisema Rehema.Kamishna Mkuu Charles Kichere amehitimisha ziara yake mkoani Iringa ambapo amefanikiwa kutembelea jumla ya maduka ya bidhaa mbalimbali 36 pamoja na vituo vya mafuta vinne.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere akisikiliza maoni kutoka kwa mfanyabiasha wa duka la nguo lililopo katika soko la Miyomboni mkoani Iringa Bi. Rehema Shabani wakati alipofanya ukaguzi wa matumizi ya Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFDs) kwenye maduka na vituo mbalimbali vya mafuta leo mkoani hapo.
Mfanyabiashara wa Kampuni ya ASAS iliyopo mkoani Iringa Feisal Abri akitoa maelezo kuhusu namna Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFDs) inavyofanya kazi katika kituo chake cha mafuta wakati Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere alipofanya ukaguzi wa matumizi ya mashine za EFD kwenye maduka na vituo mbalimbali vya mafuta leo mkoani Iringa.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (aliyevaa kofia kushoto) akizungumza na wafanyakazi wa moja ya kituo cha mafuta mkoani Iringa wakati alipofanya ukaguzi wa matumizi ya Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFDs) kwenye maduka na vituo mbalimbali vya mafuta leo mkoani hapo. (PICHA NA TRA).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...