Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania imeihakikishia Serikali ya Norway kuwa inaendelea
kuelekeza nguvu zake kwenye kuweka mikakati sahihi ya kuvutia uwekezaji kutoka
nje ya nchi, ikiwemo nchi ya Norway, ili kuleta maendeleo kwa wananchi wa
Tanzania.
Hayo yamesemwa na
Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki wa Tanzania alipokutana na Bw. Jon Lamoy, Mkurugenzi wa Shirika la
Maendeleo la Norway lijulikanalo kwa kifupi kama NORAD mwanzoni mwa ziara yake
ya kikazi ya siku tatu Mjini Oslo, makao makuu ya Norway.
Katika mazungumzo
yao, Mkurugenzi Lamoy alimueleza Waziri Mahiga kuwa shirika hilo limekuwa na
uhusiano wa karibu na wa kindugu kwa zaidi ya miongo mitano na nchi ya
Tanzania. Yeye binafsi na washirika wengi wa Tanzania nchini humo wanasifu
utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli hususan kwenye mapambano dhidi ya rushwa.
Rushwa
inarudisha nyuma maendeleo kwa kuikosesha nchi mapato, hivyo jitihada za
Tanzania za kupambana na rushwa, hususan kwenye ukusanyaji kodi, zitawawezesha
wananchi wa Tanzania kunufaika na huduma za kijamii na hatimaye kupata
maendeleo kwa haraka.
Hata hivyo
mkurugenzi huyo alitoa angalizo kuwa nia nzuri ya Serikali ya Tanzania ya
kuweka mifumo thabiti ya uwekezaji wenye faida ukiwemo ule wa sekta
ya madini, ni muhimu ikakamilika mapema ili kutoa fursa kwa wawekezaji wapya
kuwekeza kwenye sekta hiyo kwa wakati.
Kwa upande wake,
Mheshimiwa Mahiga alielezea kuwa suala hilo tayari linafanyiwa kazi ambapo
pamoja na Serikali kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji, uwekezaji huo
ni lazima uwe na faida kwa Watanzania na kwa maendeleo ya nchi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...