Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inapenda kuwataarifu waombaji wa mikopo kwa
mwaka wa masomo 2018/2019 na umma
kwa ujumla kwamba imetangaza orodha ya baadhi ya waombaji mikopo ambao fomu zao
za maombi ya mikopo zina upungufu ili waweze kufanya marekebisho kwa njia ya
mtandao https://olas.heslb.go.tz
kwa siku saba (7) kuanzia Jumatatu Septemba
24 hadi Jumapili Septemba 30, 2018.
Katika kipindi hicho waombaji wote wa mikopo ambao fomu zao zina upungufu
wa baadhi ya taarifa na nyaraka zao ama za wadhamimi wao, watapaswa kusoma
majina yao kwenye orodha iliyowekwa kwenye tovuti ya HESLB www.heslb.go.tz na kisha kuingia kwenye
mtandao wa maombi ya mikopo ili kufanya masahihisho kwa kufuata hatua
zilizowekwa na baada kukamilisha, waziwasilishe ndani ya muda uliopangwa
bila kutuma kwa njia ya EMS.
Nyaraka zote zinazokosekana ikiwa ni pamoja na vyeti vya kuzaliwa au vya
vifo vya wazazi, kurasa za taarifa na saini za mwombaji na/au mdhamini wake
zinapaswa kujazwa kwa ukamilifu, kuwa ‘scanned’ na kisha kupakiwa kwenye
mtandao baada ya kuthibitishwa na mamlaka husika.
Zoezi la Uhakiki wa Taarifa za
Waombaji wa mikopo
Baada kukamilika kwa muda wa kupokea maombi ya mikopo Julai 31, 2018,
HESLB ilikuwa imepokea jumla ya maombi 78,833 ambapo baada ya
uhakiki, HESLB ilibaini jumla ya waombaji zaidi ya 25,000 fomu zao za maombi zikiwa na upungufu wa nyaraka na
uthibitisho wa kuwezesha kuendelea na hatua inayofuata ya kupangiwa mikopo
katikati ya mwezi Oktoba, 2018.
Hitimisho
Kwa taarifa hii pia tunapenda kuwakumbusha waombaji wa mikopo ambao wamo
katika orodha hiyo yenye upungufu wa taarifa kusoma kwa umakini na kurekebisha
kasoro hizo ili waweze kupangiwa mikopo. Aidha tunawatahadharisha dhidi ya
matapeli wanaoweza kutumia taarifa hiyo kuwalaghai waombaji mikopo kuwa
wanaweza kuwasaidia kupata mikopo. Tangazo maalum na mwongozo wa marekebisho vinapatikana
katika tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz).
Iwapo wana maswali, wawasiliane nasi kupitia:
Simu: 0736665533
au 022 5507910
Barua pepe: adcp@heslb.go.tz au info@heslb.go.tz
Taarifa hii pia inapatikana kwenye tovuti ya HESLB www.heslb.go.tz
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mtendaji
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
DAR ES SALAAM
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...