Katika kuimarisha na kuboresha matibabu ya
magonjwa ya moyo kwa watoto, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeendelea
kuboresha wodi ya watoto iliyopo katika jengo la watoto ili ifikapo Desemba
mwaka huu wodi hiyo ianze kutoa huduma zote kwa watoto.
Wodi hiyo inatarajiwa kuwa na vitanda 32 ambapo
vitanda nane vitakuwa katika chumba cha kulaza watoto wanaohitaji uangalizi
maalum (ICU) na vitanda 24 katika wodi za kawaida za watoto, vyumba vitatu kwa
ajili ya kliniki za watoto pamoja na vyumba kwa ajili ya ofisi .
Kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2015 hadi
2018 Taasisi imeona jumla ya watoto 8,000 wenye matatizo mbalimbali ya kuzaliwa
nayo na yasiyo ya kuzaliwa nayo. Kwa upande wa upasuaji wa moyo jumla ya watoto
889 wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua na upasuaji wa bila kufungua
kifua
Watoto 519 walifanyiwa upasuaji wa moyo
wa kufungua kifua na kati ya hao watoto 238 walifanyiwa upasuaji na madaktari
wetu bingwa wa magonjwa ya moyo huku watoto 281 walifanyiwa upasuaji wakati wa
kambi maalum zilizowaunganisha madaktari wetu na madaktari kutoka shirika la
Mending Kids International, SACH, na mashirika mengine. Upasuaji wa moyo wa
bila kufungua kifua (Catheterization) kwa kutumia mtambo wa Cathlab ulifanyika
kwa watoto 370
Kwa upande wa kliniki ya watoto kila
siku inatoa huduma ya kati ya watoto 30 hadi 40 na kulaza mtoto mmoja hadi wawili. Tangu kuanza
kwa mwaka huu wa 2018 jumla ya watoto 95 wamefanyiwa upasuaji wa kufungua kifua
na bila kufungua kifua watoto 60
Zaidi ya asilimia 75 ya watoto
wanaofanyiwa upasuaji ni wale wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni
matundu na magonjwa yanayoshambulia milango ya mishipa mikubwa na midogo ya
moyo. Asilimia 25 ni wale ambao walizaliwa salama na kupata matatizo hayo baada
ya kuzaliwa.
Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
18/10/2018.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...