*Shule ambazo hazifuati waraka wa elimu nazo kuchukuliwa hatua
*Azungumzia ada kubwa kwa shule binafsi, aapa kutafuta suluhu
*Wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza wapewa siku 90...
Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
SERIKALI imetangaza kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria kwa shule
zote binafsi ambazo hazifuati waraka wa elimu nchini huku ikitangaza
kufanya msako kubaini wote wanaokiuka waraka huo.
Pia Serikali imetoa onyo kwa shule zote binafsi ambazo zina tabia ya
kupandisha ada kiholela, kukaririsha madarasa wanafunzi kinyume na
waraka uliopo pamoja na michango mikubwa inayotoza bila kufuata
utaratibu.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mwita Waitara amesema, hiki ni kipindi
cha elimu na kuna mambo lazima yawekwe sawa kwa wazazi, walezi, wadau
wa elimu na shule kufahamu nini ambacho kinatakiwa kufuatwa.
hayo ameyafafanua juzi alipokuwa kwenye kipindi katika kituo cha televisheni
cha Taifa (TBC) ambapo alitoa namba yake ya simu ambayo ni 0767221344
na kusema kuwa kupitia namba hiyo amepokea meseji nyingi za wazazi
ambazo nyingi ni za malalamiko na hasa kwa shule binafsi ambazo zimekuwa
zikifanya unyanyasaji wa hali ya juu kwa wanafunzi, wazazi au walezi.
Waitara ameeleza kuwa TAMISEMI ndio inayosimamia elimu ya msingi na
sekondari na ametumia nafasi hiyo kuzungumzia umuhimu wa ushirikiano
kwa pande zote akiwa na maana upande wa wazazi na shule husika katika
kupanga na kukubaliana mambo mbalimbali yakiwamo ya ada.
Pia amesema wakati wanashughulikia changamoto zilizopo, Serikali imetoa
siku 90 kwa kila mtoto anayetakiwa kuanza kidato cha kwanza kuripoti
ndani ya muda huo na iwapo hatafanya hivyo hatua zitachukuliwa kwa
mujibu wa sheria, na amewatoa hofu wazazi kuwa watoto wote ambao
wanatakiwa kuanza kidato cha kwanza ndani ya muda huo wa siku tisini
watakuwa shuleni na kuchelewa kuanza masomo hakutakuwa sababu ya
kumfanya mwanafunzi kufanya vibaya kwenye masomo yake.
VIPI KUHUSU ADA?
Waitara amesema moja ya malalamiko ambayo ameyapokea ni ada
kupandishwa kiholela kwa baadhi ya shule binafsi jambo ambalo amesema ni
marufuku shule kupandisha ada kiholela bila kumshirikisha mzazi.
"Tunafahamu hakuna muongozo rasmi wa ada kwa shule binafsi , hivyo ipo
haja ya kuuibua upya mjadala huu ili tuwe na ada ambayo itakuwa
inaeleweka. Kuna shule binafsi ambazo zipo zinazotoza ada kuanzia
Sh.milioni 1.5 hadi Sh.milioni sita na hapa ndipo yanapoanza maswali
unapoona mwanafunzi anayelipiwa ada hizo anaomba mkopo akiwa Chuo
Kikuu.Tunajua huenda kukawa na sababu nyingi lakini nachotaka kusema
lazima hili la ada tulizungumze upya na kupata muafaka. Ada ni kubwa
sana."amesema Waitara.
Hata hivyo amesema ada ambayo inalipwa ni makubaliano kati ya mzazi na
shule lakini ni jambo la ajabu mzazi anapoambiwa ada imepanda bila
kushirikishwa, hivyo ameagiza shule zote ambazo zimepandisha ada kiholela
ni marufuku kumlipisha mzazi na hivyo ada ambayo anatakiwa kulipa ni ile
ambayo walikubaliana na si hiyo iliyopandishwa bila utaratibu wa
kushirikisha wazazi au walezi husika.
Amewataka wote wenye malalamiko kuhusu ada kupandishwa kiholela
waende kwa maofisa elimu wa wilaya au kwa mkurugenzi ili hatua
zichukuliwe kwa shule husika ili kukomesha tabia hiyo."Ni marufuku
kumrudisha mwanafunzi nyumbani kwa sababu ya ada, aachwe asome, kama
mzazi amelipa ada ya mtoto kwa miaka mitatu au minne kwanini ufukuze
mwanafunzi kwa mzazi wake kushindwa kuleta ada. Mwanafunzi aachwe
asome wakati mnajadiliana namna ya kulipana hiyo ada."amesisitiza
Waitara.
AWEKA WAZI KUHUSU WASTANI
Pamoja na mambo mengine Waitara amezungumzia wastani wa alama za
ufaulu kwa wanafunzi wa shule za msingi na shule za sekondari ambapo
amefafanua tayari Serikali ilishatoa muongozo na huo ndio unatakiwa
kufuatwa kwa shule zote nchini na si vinginevyo.
"Serikali ndio yenye kupima uwezo wa wanafunzi na hivyo kama kuna sababu
za mtoto kubakia kwenye darasa kwasababu yoyote ile lazima kuwe na
makubaliano ya kimaandishi ambayo ndiyo yatatumika kama kilelezo cha
kwanini mwanafunzi amekakariri dasara.
"Kuna shule binafsi ambazo zimeweka wastani wake na wamekuwa
wakiutumia huo kuwafanya wanafunzi wasiendelee na darasa linalofuata. Hilo
ni kosa kwasababu mwenye kutoa muongozo wa kupima ufaulu ni Serikali tu,
hakuna mtu au shule yoyote ambayo inaweza kwenda tofauti.Tutafuatilia
shule zote na iwapo tubabaini wamekiuka utaratibu tutachukua hatua za
kisheria na ikiwezekana tutafuta usajili wa shule husika." amesema Waitara.
Amesema kuna taarifa anazo kuna baadhi ya shule ambazo zimewarudisha
wanafunzi kwasababu ya wastani ambao wameweka kwenye shule zao, hivyo
ametoa maagizo wanafunzi hao waachwe waendelee na masomo na
warudishwe shuleni kwa kuwa upimaji wa ufaulu kwa elimu ya msingi
unafanyika darasa la nne na kwa sekondari inafanyika kidato cha pili,
wanafunzi ambao wamefaulu waachwe wasome na hili agizo ni kwa shule
zote zikiwemo hizo na binafsi.
Amesema anazo meseji kwenye simu yake ambazo zinazungumzia wanafunzi
kurudishwa kwasababu ya kushindwa kufikia alama zilizowekwa."Shule
ambazo zinashindwa kufuata muongozo baadhi tunazo na nimetoa maagizo
zifuatiliwe ili tuchukue hatua,"amesema Waitara huku akitaja baadhi ya
shule(majina tunayo) ambayo amedai yanakiuka utaratibu uliopo.
AONYA SHULE ZINAZOBADILISHA WANAFUNZI DINI
Wakati huohuo Waitara ametoa onyo kwa shule ambazo zimekuwa na tabia
ya kubadilisha imani za watoto kwa kigezo cha kuwa sifa ya kujiunga na
shule hizo ambapo amesema ni marufuku kama shule inamilikiwa na
Wakistro basi Waislamu waachwe wasome na hivyo hivyo kama inamilikiwa
na Waislamu, basi Wakristo wasome.
""Hatutaki kusikia mtoto amebadili imani yake ya dini au dhehebu lake
kwasababu ya masharti ya shule. Serikali ndio inayotoa muongozo kuhusu
elimu nchini, hivyo ni marufuku, wanafunzi waachwe wasome bila
kusumbuliwa,"amefafanua Waitara.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...