Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya Rogers Sian'ga akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Kongamano linalotarajiwa kufanyika Februari 13 ambalo litawakutanisha wasanii wa fani mbalimbali nchini ili kujadili athari za dawa za kulevya ofisini kwake jijini Dar es salaam, Kulia ni Kamishna wa Kitengo cha Kinga na Tiba wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Dk.Peter Mfisi.
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini Tanzania Joyce Fissoo akizungumza katika mkutano huo leo.
Na Said Mwishehe,Globu ya Jamii
KAMISHNA Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na na Kupambana na Dawa za Kulevya
Rogers Sian'ga amesema kwa sasa wamefanikiwa kidhibiti njia ambazo zilizokuwa
zinatumiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya kupitia dawa hizo ili kuziingiza
nchini Tanzania.
Amesema kwa sasa njia ambayo inatumiwa na baadhi ya wanaojihusisha na
biashara haramu ya dawa hizo imebaki ya Kusini ambako dawa zinapitishwa kutokea
nchini Msumbiji na tayari wameweka mikakati ya kuidhibiti njia hiyo.
Sian'ga amesema hayo leo Februari 11, 2019 jijini Dar es Salaam wakati
anazungumzia Kongamano linalotarajiwa kufanyika Februari 13 mwaka huu ambalo
litawakutanisha wasanii wa fani mbalimbali nchini ili kujadili athari za dawa za
kulevya.Mgeni rasmi kwenye kongamano hilo anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais
Samia Suluhu Hassan.
Pamoja na kuzungumzia kongamano hilo, waandishi walitaka kufahamu ni kiwango
gani Mamlaka hiyo imefanikiwa kudhibiti biashara ya dawa za kulevya nchini
ambapo Sian'ga amejibu uingizwaji wa dawa upo lakini umepungua kwa kiwango
kikubwa sana ikilinganisha na miaka ya zamani kabla ya mamlaka hiyo kuwepo.
" Kwanza ifahamike kuwa usafirishaji wa dawa za kulevya sio Tanzania peke yake bali
lipo katika nchi mbalimbali duniani.Tunashirikiana na nchi nyingine katika
kupambana na dawa za kulevya na kuna njia ya Kusini ndio imeibuka.
"Katika mapambano hayo katika njia ya baharini mwaka jana zimekamatwa tani
9000 kutokana na ushirikiano wa nchi mbalimbali katika ukanda wa baharini.Pia
mwaka jana dawa za kulevya aina ya heroin zilikamatwa kilo 185 na sehemu chache
ya dawa hizo zilikwenda nchini Msumbiji,"amesema.
Amefafanua kwa ujumla kiwango cha uingizwaji dawa za kulevya nchini kimepungua
na kwa sasa hata wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo wameingia woga na kiasi
wanachoingia ni kidogo ambacho ni kati ya kilo nne hadi kilo tano na kwamba
mkakati uliopo ni kudhibiti njia ya Kusini ambapo dawa zinaingizwa nchini Tanzania
kutokea nchini Msumbiji.
Pia amesema dawa za kulevya aina ya Heroin na Cocaini matumizi yamepungua na
hivyo dawa ambazo zinatumika ni dawa za hospitali.
Kuhusu kongamano la Februari 13 mwaka huu ,Kamishna Jeneral Sian'ga amsema
lengo kuu ni kuhakikisha Watanzania wanaunganisha nguvu katika mapambano ya
dawa za kulevya.
Hivyo, kupitia kongamano hilo ambalo litawakutanisha wasanii mbalimbali nchini
ambapo kupitia kongamano hilo itatolewa elimu inayohusu athari za matumizi ya
dawa za kulevya, hivyo ametoa rai ya wasanii kujitokeza kwa wingi ili nao watoe
maoni yao ya nini kifanyike kukomesha uingizwaji wa dawa za kulevya.
Wakati huo huo Kamishna wa Kitengo cha Kinga na Tiba wa Mamlaka ya Kudhibiti na
Kupambana na Dawa za Kulevya Dk.Peter Mfisi amezungumzia umuhimu wa wasanii
wa mashirikisho mbalimbali kushiriki kongamano hilo hasa kwa kuzingatia kuna
baadhi ya wasanii wamekuwa wakitumia dawa za kulevya na wengine wanatumika
kukubebeshwa dawa.
"Tatizo la dawa za kulevya ni la dunia nzima na wanaoatharika zaidi ni vijana
wakiwamo wasanii maarufu ambao wengi wao wameathirika zaidi na wengine
wamepoteza maisha kutokana na utumiaji wa dawa za kulevya.
"Si kwamba wasanii hawajui kuwa dawa za kulevya zina athari,wanajua lakini
wanaangalia leo lakini ukweli athari zake ni nyingi sana.Kwa bahati mbaya
wanaotumia athari zake ni kubwa. Wapo wasanii ambao wametumika kubeba dawa
za kulevya kutokana na ahadi za fedha badala ya kuelezwa na matatizo
yanayopatikana kupitia dawa hizo. Hivyo kupitia kongamano hilo wataeleza athari
zake," amesema Dk.Mfisi.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini Tanzania Joyce Fissoo
ametumia nafasi hiyo kuwahamasisha wasanii wa mashirikisho mbalimbali kushiriki
kongamano hilo huku akifafanua kundi ambalo linaathirika na utumiaji wa dawa za
kulevya ni la wasanii.
"Tunaamini kuwa kupitia kongamano hilo ambalo mgeni rasmi atakuwa Makamu wa
Rais Samia Suluhu Hassan ,wasanii watapa fursa ya kupata elimu inayohusu athari
za dawa za kulevya.Tunaomba wasanii wote wajitokeze kwa wingi na wale wa mikoani
tanaomba wafuatilie kongamano hilo kupitia vyombo vya habari,"amesema Fissoo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...