Na Stella Kalinga, Simiyu
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
anayeshughulikia Mawasiliano, Dkt. Jim Yonaz amemkabidhi Mkuu wa Mkoa
wa Simiyu, Anthony Mtaka kompyuta 100 na vifaa vingine zikiwemo
printa 10, vilivyotolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF),
vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 220.
Makabidhiano hayo yamefanyika Aprili 09, 2019 katika Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu Mjini Bariadi na kushuhudiwa na baadhi ya Wakuu wa
Taasisi za Umma, Wakuu wa shule na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya
Sekondari Bariadi.
Akikabidhi kompyuta hizo Dkt. Yonaz amewapongeza viongozi mkoani
Simiyu kwa kuendelea kufanya ubunifu katika masuala mbalimbali
yanayouwezesha mkoa kukua katika nyanja mbalimbali hususani katika
uchumi na elimu.
Aidha, amesema Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano itaendelea
kushirikiana na Mkoa wa Simiyu kuharakisha maendeleo kupitia Sayansi
na Teknolojia.
" Ninaamini kompyuta hizi zitawasaidia sana wanafunzi hawa na walimu
pia yapo mambo yatakayotatuliwa kupitia kompyuta hizi, ili tuweze
kuleta elimu bora, tutengeneze wasomi wazuri ambao watachangia katika
uchumi wa Taifa letu" alisema Dkt. Yonaz.
Akipokea kompyuta hizo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka
ameshukuru kwa msaada huo huku akibainisha kuwa lengo la Mkoa ni kuwa
mkoa ambao uko kiganjani ambao taarifa yoyote inaweza kupatikana muda
wowote.
“Tungehitaji mfahamu kuwa sisi ni miongoni mwa mikoa michache sana
Tanzania yenye Mpango Mkakati wa TEHAMA wa mkoa na (focus) lengo letu
kama mkoa ni kuwa mkoa ambao uko kiganjani, mkoa ambao mtu ataweza
kupata taarifa yoyote wakati wowote” alisema Mtaka.
Mkurugenzi Mkuu wa UCSAF, Mhandisi. Peter Ulanga amesema UCSAF kwa
kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao inaandaa mpango wa kutoa
mafunzo kwa Maafisa TEHAMA ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao
kibunifu.
Nao walimu na wanafunzi wa shule za sekondari mkoani Simiyu
wameishukuru Serikali kutoa kompyuta hizo na kueleza namna
zitakavyowasaidia.
"Kompyuta hizi kwanza zitatusaidia kuwezesha mawasiliano hususani
katika masuala ya intaneti kwa ajili ya kutuma na kupokea taarifa
mbalimbali kwa wakati na kuchapa majaribio ya wanafunzi" Mkuu wa Shule
ya Sekondari Itilima, Mwl.Flora Shimbi.
"Vifaa hivi vitasaidia sana wanafunzi kujifunzia kwa vitendo wawapo
shuleni na kutafuta 'notes' za masomo mbalimbali ili waweze kujifunza"
Mkuu wa Shule ya Sekondari Bariadi, Mwl.Ally Simba
"Hizi kompyuta zitatusaidia kujifunza kwa vitendo na tutaelewa zaidi
kuliko kama tungesoma bila kompyuta, kila atakachokuwa anafundisha
mwalimu tutakuwa tunakiona moja kwa moja" alisema Naomi Mathias
Mwanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Bariadi.
Kompyuta hizo pamoja na vifaa vingine vimekabidhiwa kwa baadhi ya
Wakuu wa Taasisi, Ofisi za wakuu wa Wilaya, Ofisi ya mkuu wa mkoa na
baadhi ya wakuu wa shule za Sekondari mkoani hapa mkoani.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano, Dkt. Jim Yonaz(kulia) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka moja ya kompyuta 100 zilizotolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa Mkoa wa Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka akimkabidhi Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini moja ya kompyuta 100 zilizotolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa niaba ya Ofisi ya Mkoa wa Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka akimkabidhi Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa, Mwl. Kuyunga Jackson moja ya kompyuta 5 zilizotolewa na mkoa kwa shule hiyo kutoka katika kompyuta 100 Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Mkoa wa Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wakuu wa shule, wanafunzi wa shule ya sekondari Bariadi na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano, Dkt. Jim Yonaz na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF), Mhandisi. Peter Ulanga baada ya makabidhiano ya kompyuta 100, printa 10 na vifaa vingine vilivyotolewa na UCSAF kwa mkoa wa Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka(kulia) akimkabidhi Kaimu Mkuu wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Simiyu, Ins. moja ya kompyuta 5 zilizotolewa na mkoa kwa shule hiyo kutoka katika kompyuta 100 Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Mkoa wa Simiyu.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF), Mhandisi. Peter Ulanga(wa tatu kulia), Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano, Dkt. Jim Yonaz na Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini wakiwa katika picha moja baadhi ya wanafunzi wa Shule ya sekondari Bariadi, baada ya makabidhiano ya kompyuta 100, printa 10 na vifaa vingine vilivyotolewa na UCSAF kwa mkoa wa Simiyu.
Kutoka kulia Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF), Mhandisi. Peter Ulanga, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano, Dkt. Jim Yonaz na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka wakifurahia jambo na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya sekondari Bariadi kabla ya makabidhiano ya kompyuta 100, printa 10 na vifaa vingine vilivyotolewa na UCSAF kwa mkoa wa Simiyu.
Sehemu ya kompyuta 100 , printa 10 na vifaa vingine
vilivyotolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) kwa mkoa wa
Simiyu na kukabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka
Aprili 09,2019.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...