JK na mama salma wakiweka shada la maua kwenye kaburi la hayati nyaulawa
JK na mama salma wakimliwaza mjane wa marehemu

Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo, Alhamisi, Novemba 13, 2008, amewaongoza mamia ya wananchi kumzika aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Vijijini, Ndugu Richard Said Nyaulawa.

Mazishi hayo yamefanyika nyumbani kwa Mbunge huyo katika kijiji cha Inyala, kiasi cha kilomita 25 kutoka mjini Mbeya kwenye barabara kuu inayoekelea Iringa.
Rais Kikwete na mamia ya waombolezaji hao wameshuhudia mwili wa marehemu ukiteremshwa kaburini kiasi cha saa 9.20 mchana katika shamba lake kijijini hapo.
Mbali na Rais Kikwete, ambaye amefuatana na mke wake, Mama Salma Kikwete, mazishi hayo ya Ndugu Nyaulawa yamehudhuriwa na mawaziri, wabunge, wafanyabiashara, viongozi wa vyombo vya habari na mamia ya wananchi.
Rais Kikwete amewasili kwenye uwanja wa ndege wa mjini Mbeya kiasi cha saa nane mchana na kwenda moja kwa moja kijijini Inyala kwa ajili ya mazishi ya Mbunge huyo ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumatatu ya wiki hii nyumbani kwake mjini Dar Es Salaam kwa ugonjwa wa kansa ya ini.
Kabla ya mwili wa marehemu kuteremshwa kaburini waombolezaji wameshuhudia salamu za rambirambi kutoka kwa viongozi mbali mbali akiwamo Mkurugenzi mwenza wa Kampuni ya Business Times Limited, Rashid Mbughuni, ambaye ameelezea ukaribu wa miaka mingi wa familia za akina Mbughuni na Nyaulawa.
Mbali na ubunge, Ndugu Nyaulawa alikuwa pia Mkurugenzi katika kampuni hiyo ya Business Times Limited.
Wengine waliozungumza kwenye mazishi hayo ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mbeya, Ndugu Mullah; Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Ndugu John Mwakipesile; Naibu Spika wa Bunge, Ndugu Anna Makinda; Naibu Katibu Mkuu wa CCM, George Mkuchika; mwakilishi wa wabunge wa upinzani, Ndugu Mwadini Abbas Jecha, mwakilishi wa wabunge wa CCM, Dk. Mahenge.
Mara baada ya kukamilika kwa shughuli za mazishi hayo, Rais Kikwete ameondoka Mbeya kurejea Dar Es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Dah michuzi unaharibu kiswahili.Siku ya majonzi sio ya kuliwazana bwana.Tafuta kamusi.
    kuliwaza=kuburudisha.
    Wabongo tujifunze kutumia "proper" misamiati sio kuongea-ongea ovyo tunakiharibu kiswahili chetu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...