Na Karama Kenyunko Michuzi Tv

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imeonya vikali wafanyabiashara wanaosafirisha mazao ya kilimo bila kusajiliwa, ikibainisha kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Onyo hilo limetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa COPRA, Irene Mlola, leo Julai 6, 2025 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea banda la Mamlaka hiyo katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba, jijini Dar es Salaam.

Mlola amesema kuwa COPRA inafanya juhudi kuhakikisha usalama wa chakula nchini na kwamba usafirishaji wa mazao bila usajili ni kinyume na sheria za nchi, zikiwemo Sheria ya Nafaka na Sheria ya Usalama wa Chakula.

"Unaposafirisha mazao bila kufuata taratibu, unajiingiza kwenye matatizo ya kisheria ambayo yanaweza kusababisha kufungwa kwa biashara yako, kutozwa faini au hata kufungwa gerezani," amesema.

Aidha, ameeleza kuwa lengo la hatua hizo ni kuhakikisha kuwa biashara ya mazao nchini inafanyika kwa njia rasmi na yenye tija kwa uchumi wa taifa.

"Tunataka Tanzania ijulikane kimataifa kwa kuuza mazao yenye ubora yanayozingatia viwango vya kimataifa. Kwa sasa tumefungua milango ya masoko ya kimataifa kwa mazao kama vile ufuta, kokoa, choroko na mbaazi kupitia mfumo wetu wa kidijitali," amesema.

Mlola amesema COPRA imefanikiwa kuwaunganisha wafanyabiashara wa ndani na wale wa kimataifa ambao wamekuwa wakionesha nia ya kupata vibali vya usafirishaji wa mazao kutoka Tanzania.

"Tumeona watu wengi wakifika kutaka kujua namna wanavyoweza kushiriki biashara hii. Jibu letu ni moja: Jisajili kwanza," amesisitiza.

Aidha ametoa wito kwa Watanzania wanaopenda kuingia katika biashara ya kusafirisha mazao kwenda nje ya nchi, kutembelea ofisi za COPRA zilizopo Makao Makuu, Dodoma na katika mikoa 14 nchini, au kupitia tovuti rasmi ya Mamlaka hiyo.

Ameeleza pia kuwa usajili huo unafanyika kupitia mfumo wa kidijitali wa E-Kilimo, ambapo wakulima na wafanyabiashara hujaza taarifa zao kwa ajili ya kupata kibali huduma ambayo ni bure.

"Milango iko wazi, tembeleeni banda letu hapa Sabasaba au ofisi zetu popote nchini ili mpate elimu ya kutosha kuhusu fursa zilizopo kwenye sekta ya mazao," amesema Bi. Mlola.

Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanaendelea hadi Julai 13, 2025, yakihusisha wadau mbalimbali wa biashara kutoka ndani na nje ya nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) , Irene Mlola akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 6, 2025 wakati alipotembelea banda la COPRA, wakati wa Maonesho ya 49 ya Biashara ya yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba Mbagala Jijini Dar es Salaam.


 


Wanafunzi na wakufunzi wa Jundokan Karate Do Tanzania leo Jumapili, Julai 6, 2025, wameungana katika Gasshuku – yaani semina maalum ya karate – iliyofanyika kwa mafanikio makubwa katika viwanja vya Shule ya Sekondari Azania, jijini Dar es Salaam.

Neno “Gasshuku,” lenye asili ya Kijapani, linamaanisha “kambi ya pamoja ya mafunzo,” ambapo wakarateka wa viwango mbalimbali hukusanyika kwa siku nzima au zaidi ili kuimarisha ujuzi wao, kushiriki uzoefu, na kujifunza kwa pamoja katika roho ya karate-do.

Kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa kumi jioni, washiriki walifundishwa na timu ya wakufunzi mahiri wakiongozwa na Sensei Yusuf Kimvuli, Naibu Mkurugenzi wa Ufundi wa Jundokan Karate Do Tanzania, akiwa na Sensei Maulid Pambwe, Sensei Dkt. Philip Swai, Sensei Bilal Mlenga na Sensei Wahid Aghful.

Washiriki kutoka mikoa mbalimbali nchini – wakiwemo kutoka Zanzibar, Morogoro, Dodoma, Mafinga na Moshi – walipitia vipindi mbalimbali vya mafunzo. Mafunzo yalianza kwa Jumbi Undo (mazoezi ya maandalizi ya mwili), yakafuatiwa na Kata (miondoko ya msingi ya karate) na kisha Bunkai, yaani maelezo ya nadharina ya vitendo ya hatua za Kata hizo.

Gasshuku hii ilionyesha sio tu umahiri wa wakufunzi na ukakamavu wa wanafunzi, bali pia mshikamano wa familia ya Jundokan nchini.










TOLEO la Sheria ambazo zimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili zinatarajiwa kuanza kutoka ifikapo Agosti mwaka huu ikiwa baada ya hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan kuagiza kutafsiriwa kwa sheria ili iweze kueleweka kwa urahisi na watu wa makundi yote.

Ameyasema hayo leo Julai 6, 2025 Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorius Njole, katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ‘sabasaba’ yanayoendelea Jijini Dar es Salaam. 

Aidha Njole amesema kuwa sambamba na kuendelea na mchakato wa kukamilisha zoezi hilo pia Ofisi hiyo imefanya mabadiliko makubwa ya kuhakikisha sheria zilizopo zinatekelezeka na kuwafikia wananchi.

“Mpaka sasa tumefanya mabadiliko makubwa ya kuhakikisha tunakuwa na sheria zinazowafikia wananchi kama Sheria na ukamilifu wake na lugha ambayo wananchi wanaifahamu” amesema Njole.

Amesema kuwa ofisi hiyo imefanywa urekebu wa sheria mbalimbali ili ziweze kuendana na mahitaji ya sasa ya nchi “ tumefanya urekebu wa Sheria hizi kwa kuzikisanya sheria zote za nchi pamoja na kuingiza marekebisho ambayo yamekuwa yakifanyika kila wakati” amesema

Pamoja na hayo, amesema kuwa Serikali ipo katika mchakato wa kutengeneza mfumo wa sheria wa kusimamia matumizi ya Akili Mnemba (IA) na kubainisha kuwa mchakato huo utakapokuwa tayari utaandaliwa sheria.

Kwa upande wake Mwandishi Mkuu Msaidizi wa Sheria, Rahema Katuga amesema kuwa baada ya kukamilika kwa urekebu wa sheria mbalimbali ambazo zimeanza kutumika Julai mosi mwaka huu za awali hazitatumika tena. 








Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Taifa (UWT)Ndg. Mary Chatanda leo tarehe 06 Julai,2025 ametembelea Banda Jumuishi ya Ofisi ya Waziri Mkuu lililopo katika Viwanja vya Maonesho ya 49 ya Biashara (SABASABA) yanayoendelea Jijini Dar wa Salaam.

Maonesho hayo yamebebwa na Kauli Mbiu isemayo; "Maonesho ya Biashara ya Kimataifa, Fahari ya Tanzania"



-Waomba ushirikiano katika suala la Nishati Safi ya Kupikia

Wanufaika wa Mradi wa ARDHI (Accelerating Reforestation for the Development of Households) wa Mkoa wa Tanga wametembelea Banda la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) Jijini Dar es Salaam Julai 6, 2025 kwa lengo la kujifunza mbinu bora za kuhifadhi mazingira na kujiongezea kipato kupitia miradi ya nishati safi ya kupikia.

Akizungumza kwa niaba ya wanufaika hao wa mradi unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Shirika lisilo la Kiserikali la World Vision Tanzania, Audiphonce Jonas alisema mradi huo umejikita katika suala la uhifadhi wa mazingira.

"Tumefika hapa katika banda la REA kwa ajili ya kujifunza namna ambavyo tunaweza kutumia nishati safi ya kupikia kutimiza azma yetu ya kuhifadhi mazingira sambamba na kuona ni vipi tunaweza kuitumia kujipatia kipato," alisema Jonas.

Alisema mradi umeanza mwaka huu na utafika kikomo mwaka 2027 na unanufaisha wilaya nne za Mkoa wa Tanga ambazo ni Pangani, Kilindi, Mkinga na Handeni.

Alisema lengo la mradi ni kuwa na usimamizi endelevu wa misitu na hilo linafanyika kwa kubuni njia mbadala za matumizi ya kuni na mkaa ambazo ndio chanzo kikuu cha nishati ya kupikia kwa wakazi wa wilaya hizo.

"Lengo la mradi huu wa ARDHI ni sawa na kinachotekelezwa na REA; itakuwa vyema REA ikatazama namna ya bora ya kushirikiana nasi katika hili jukumu la uhifadhi wa misitu," alisema.

Alisema kwa sasa mradi unashirikiana kwa karibu na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na ni wakati sahihi pia kushirikiana na REA kupitia miradi yake ya Nishati Safi ya Kupikia.

"Tunaipongeza REA kwani tumeshuhudia hatua kubwa imepigwa; tumejionea bidhaa mbalimbali za nishati safi ya kupikia zilizotengenezwa kwa teknolojia iliyoboreshwa," alisema.

Alisema malighafi za utengenezaji wa bidhaa mbakimbali za nishati safi ya kupikia ikiwemo mkaa mbadala zinapatikana kwa wingi katika maeneo yao hivyo itakuwa jambo rahisi kuanzisha miradi ya nishati safi ya kupikia.





 WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa Wadau wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii Afrika (ASSA), unaotarajiwa kufanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Ridhiwani amesema kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, anatarajiwa kufungua rasmi mkutano huo Julai 10, 2025  

Amesema mifuko ya hifadhi ya jamii itakayoshiriki kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ni pamoja na NSSF, PSSF, NHIF, WCF, ZSSF, na ZHHF.

Aidha, mkutano huo utahusisha ushiriki wa wadau wa sekta hiyo, ambao pia watahudhuria kongamano litakalofanyika Julai 9 mwaka huu jijini humo,  ambapo pamoja na mambo mengine mada mbalimbali zinazohusiana na mifuko ya hifadhi ya jamii zitajadiliwa kwa kina.

Ridhiwani amesema kuwa lengo la kongamano hilo ni kuwakutanisha wadau, watunga sera, wasimamizi na watendaji wa sekta ya hifadhi ya jamii Afrika, ili kwa pamoja wajadili na kuazimia namna sekta hiyo ilivyokuwa na uwezo mkubwa katika ujenzi wa miundombinu na huduma nyingine za kijamii katika Bara la Afrika.

Jumuiya ya ASSA inaundwa na mifuko ya hifadhi ya jamii kutoka nchi 15 za Bara la Afrika ambazo ni pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Zimbabwe, Malawi, Sudan ya Kusini, Comoro, Sierra Leone, Côte d’Ivoire, Gambia, Mali, Namibia, na wenyeji wao wa mkutano huo kutoka Tanzania.


Na Nasra Ismail

Wizara ya Mifugo na Uvuvi leo imezindua chanjo ya homa ya mapafu kwa ngombe mkoani Geita pamoja na kuzindua zoezi la uvikwaji wa hereni kwa ngombe na kuachana na utaratibu wa kuwagonga mihuri ya moto kwenye ngozi.

Zoezi hilo la uzinduzi limefanyika katika halmashauri ya wilaya ya Chato pamoja na wilaya ya Bukombe huku lengo likiwa ni kupandisha thamani ya mifugo nchini pamoja na kupunguza upotevu wa mifugo.

Kupitia hereni hizi za ng'ombe wataweza kusajiriwa kupitia jina la mmiliki Pamoja na kuwa na uwezo wa kufatiliwa wakiibiwa kupitia hereni hizi.

Waziri wa ufugaji na uvuvi Dkt Ashatu Kijaji ametoa wito kwa wafugaji kujitokeza kupeleka mifugo yao kupata chanjo ili mifugo hiyo iwe na thamani na kuweza kuuzwa nje.

Aliongeza kuwa uchanjaji wa mifugo hii utakuwa ni bure ambapo chanjo zinazotolewa ni pamoja na homa ya mapafu, sotoka kwa mbuzi na kondoo pamoja na chanjo ya kideli kwa ajili ya kuku na bata.

Mkoa wa Geita una takribani ng'ombe milion 1 ambapo katika wilaya ya Chato jumla ya ng'ombe 600 watapata chanjo hizi.










Na.Ashura Mohamed -Arusha.

Mashabiki wa Timu za Simba na Yanga ambao ni watumishi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru(TICD), wamecheza mechi ya kirafiki katika juhudi za kuendelea kudumisha mahusiano na ushirikiano katika maeneo ya kazi.

Akizungumza katika bonanza hilo Mgeni rasmi Kaimu Naibu Mkuu wa chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD),anayeshughulikia Mipango na Utawala bi.Janeth Zemba alisema kuwa lengo hasa la bonanza hilo ni kuendelea kutangaza taasisi hiyo kupitia michezo.

"Bonanza hili ni la tatu kufanyika na leo hakuna aliyepatikana mshindi kwa kuwa sio mashabiki ya Simba wala Yanga aliyemfunga mwenzake hivyo tutaendelea kushirikiana katika michezo kwa kuwa inajenga mahusiano mema,ni furaha amani na pia inatuweka vizuri kiafya kupitia mazoezi tunayoyafanya mwaka mzima hivyo tutaendelea kuboresha na kushirikiana pia na wadau mbali mbali ".Alisema bi.Zemba

Aidha alitumia fursa hiyo kuwaasa wadau mbali mbali kuendelea kudumisha mshikamo na ushirikiano,na kuendelea kuitangaza taasisi hiyo kupitia sekta hiyo ya burudani ambayo inaleta makada mbali mbali.

Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho Daktari Bakari George alisema kuwa bonanza hilo linaleta watumishi na jamii ya maendeleo ya tengeru pamoja na ni mfulululizo wa bonanza ambalo linawakutuanisha pia na watu maarufu ambao wamewahi kutumikia vilabu vikubwa nchini vya Simba na Yanga.

"Mwaka Jana katika bonanza kama hili tuliwashirikisha wasemaji wa timu hizi mbili na Leo pia Mwaka huu tuna wachezaji ambao ni Mrisho Khalifan Ngassa ambaye amewahi kucheza katika klabu ya Yanga na Daniel Mrwanda ambaye aliwahi kucheza katika timu ya Wekendu wa Msimbazi Simba na timu ya Taifa pia "Alisema dkt.Bakari

Dkt.Bakari alisema kuwa nia kubwa ni hamasa ya michezo na vilevile kuitangaza taaisisi hiyo ya TICD,kupitia sekta ya michezo ambayo huleta watu wengi pamoja.
Hata hivyo alisema kuwa bonanza hilo ni kichocheo kikubwa kwa watumishi kuendelea kufanya mazoezi mwaka mzima na kulete tija katika maeneo ya kazi.

Bonanza hilo limekutanisha mashabiki wa timu ya Simba na Yanga kutoka katika viunga wa mkoa wa Arusha,ambapo limekuwa likijipatia umaarufu mwaka hadi mwaka ambapo lengo ni kulipeleka katika maeneo mengine nchini.

Mechi ya utangulizi ilikutanisha timu ya Wanafunzi wa chuo Cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD) ambao ni mashabiki wa Simba na Yanga,ambapo matokeo yalikuwa ni 1-1 mchezo uliofanyika katika uwanja wa chuo Cha Mifugo Tengeru.

Mchezaji wa Zamani Mrisho Khalifan Ngassa akimkabidhi zawadi ya Jezi mkuu wa chuo hicho dkt.Bakari George uwanjani hapo.




Pichani ni Mashabiki wa timu ya Simba ambao walifika uwanjani hapo kushuhudia mtanange huo.
Timu ya Mashabiki wa Yanga ambao ni watumishi katika taasisi hiyo ya Maendeleo ya Jamii Tengeru


Mgeni rasmi bi.Janeth Zemba ambaye ni kaimu Naibu Mkuu wa Chuo hicho anayeshughulikia Mipango na Utawala wakifuatilia kwa karibu mtanange huo.

Top News