Na Mwandishi Maalum
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameuagiza uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo kuwahamisha, mara moja, kutoka Idara za Utawala na Fedha za wizara hiyo maofisa wa idara hizo ambao wamekuwa wanasababisha ukosefu wa utulivu miongoni mwa walimu nchini kwa kutokuwa waaminifu.

Aidha, Rais Kikwete ameagiza kuwa kuanzia sasa mwalimu yoyote nchini asihamishwe kwenye kituo chake kama hakuna fedha ya kumlipa pesa zake halali za uhamisho.

Vile vile, Rais Kikwete ameuagiza uongozi wa wizara hiyo kukomesha mara moja tabia ya kulimbikiza madai na malipo ya walimu nchini akisisitiza kuwa mwalimu mwenye haki ya kulipwa lazima alipwe mara moja.

Rais Kikwete ametoa maagizo hayo jana, Jumatano, Februari 18, 2009, wakati alipokutana na kuzungumza na uongozi wa Wizara hiyo, Ikulu, Dar Es Salaam, katika mwendelezo wa mikutano ya kutathmini utendaji wa Serikali yake kati yake na Wizara mbali mbali na mashirika yaliyoko chini ya Wizara hizo.

“Naelewa kuwa kwenye Serikali yatakuwapo madai wakati wowote ule. Lakini inakuwaje kuwa mwalimu anapandishwa cheo mara ya kwanza halipwi mshahara mpya? Anapandishwa mara ya pili halipwi mshahara mpya? Anapandishwa cheo mara ya tatu halipwi mishahara mpya?”
Rais amewauliza viongozi wa Wizara hiyo na kuongeza:
“Hili linatokea vipi wakati vyeo vyote vipya vimepangiwa fedha kwenye bajeti? Na kwenye mfumo wote wa Serikali kwa nini hili linatokea katika Wizara ya Elimu tu?”
Rais amesema kuwa anazo habari kuwa lipo genge la watu ambalo kazi yao ni kutunza risiti baada ya kuzilipa, na baadaye kuzilipa tena na tena.

Amesema Rais Kikwete: “Machi mwaka jana tulilipa madai ya walimu. Mwezi Julai tukapata madai makubwa zaidi kuliko yale ya Machi. Kama vile hiyo haikutosha, mwezi Septemba tukapata madai mengine makubwa zaidi kuliko hata yale ya Julai. Naambiwa wale watu wanatunza risiti zile zile na kuzitumia kutoa madai hewa.”

“Mnasimamia vipi risiti hizi? Hatuwezi kamwe kuendelea namna hii. Madai ni yale yale, risiti ni zile zile…hili lazima tulikomesha na watu hawa wahamishwe mara moja ili tuanze upya… miaka nenda, miaka rudi tumekuwa na tatizo hili… watu wamekuwa masultani pale na wanaendelea kuvuruga utulivu wa walimu,” amesema Rais Kikwete na kusisitiza:
“Hatuwezi kuendelea kuwaruhusu wavuruge. Nataka wahamishwe haraka iwezekanavyo. Hatuwezi kukataa kuwalipa watu mpaka tuingie katika kutokuelewana. Watu hawajali, wamejisahau, bora wao wanalipwa, basi hawajali kama watu wengine wanateseka. Mambo yao yananyooka, huku walimu wanaendelee kuteseka na kulalamika.”

Rais Kikwete amesisitiza kuwa hataki tena kusikia habari ya madai ya walimu. “Nataka kila mmojawetu atimize wajibu wetu. Nimechoshwa na mambo ya namna hii. Tunataka watu waaminifu.”
Kuhusu kuhamisha walimu bila kuwalipa fedha zao za uhamisho, Rais Kikwete ameelekeza kuwa kuanzia sasa mwalimu yoyote nchini asihamishwe bila kuwapo fedha za kulipia uhamisho huo.
“Kuanzia sasa hakuna kuhamisha mwalimu yoyote bila kuwapo pesa za kumlipa. Kama hakuna fedha za uhamisho, hakuna kuhamisha mwalimu. Ofisa yoyote atakayefanya hivyo basi mshahara wake ukatwe kulipia uhamisho huo. Na wakati mwingine watu wanahamishwa bila sababu zozote za msingi.”

Katika mkutano huo, Rais Kikwete pia ametaka kuimarishwa kitengo cha ukaguzi katika wizara hiyo akisisitiza kuwa kitengo chenye nguvu cha ukaguzi ndicho mkombozi wa elimu nchini.
“Idara imara zaidi ya ukaguzi itatusaidia zaidi katika kuimarisha elimu yetu. Ujumbe wangu kwetu ni ongezeni bidii,” amesema Rais Kikwete.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 13 mpaka sasa

  1. HONGERA SANA MH. RAISI KWA KUONYESHA MOYO WA DHATI KATIKA KUENDELEZA SEKTA YA ELIMU NCHINI,

    WASIWASI WANGU NI KUWA HIZO KAULI ZAKO NZURI NA NIA THABITI HUWA HAVISHUGHULIKIWI KAMA UNAVYO AGIZA NA UNAANGUSHWA NA BAADHI YA WATENDAJI WAKO WABOVU,

    SASA MBONA UNAENDELEA KUWAFUMBIA MACHO? AU UNATUPAKA MAFUTA KWA MGONGO WA CHUPA( a.k.a CHANGA LA MACHO)

    Mfano mzuri ni ahadi zako kwenye mikutano ya hadhara ni NGAPI ZIMESHUGHULIKIWA?

    KUNAUKIRITIMBA SANA HAPO WIZARANI(ELIMU) NA NYINGINEZO.

    NADHANI MH. HAUPO BUSY TENA KAMA MWAKA ULIOPITA SO UTAFUATILIA MAMBO YA KITAIFA KWA KARIBU ZAIDI,
    HASA ILE KAULI MBIU YAKO;

    'ARI, KASI NA NGUVU MPYA'

    NIKUTAKIE KILA LA KHERI NA M'MUNGU AKUBARIKI.

    MUNGU IBARIKI AFRIKA
    MUNGU IBARIKI TANZANIA. AMIN!

    ReplyDelete
  2. sio wao peke yao na waziri wao pia angatuliwe maana ameshindwa kufuatilia majukumu yake mpaka raisi anaingilia kati, waziri amepewa majukumu ya kumsaidia rais katika kuiendesha wizara nzima ya elimu sasa kama rais anarudi kufuatilia masuli ya walimu ina maana waziri kazi imemshinda na atoweke mara moja.

    ReplyDelete
  3. Hii mbona haiko sawa kabisa??? Sasa Rais anaagiza maofisa wahamishwe kwa kuzembea kazini. Je, wahamishiwe wapi ambako uzembe wao utavumiliwa? - Hii naona imekaa kisiasa zaidi!

    ReplyDelete
  4. Anony 12:26 PM, roho inaniuma tunakuwa na kiongozi anayeleta mzaa namna hii! hivi mtu akiiba anahamishwa au anashitakiwa tunapoeleke si kuzuri jamani tujaribu hata upinzani kidogo labda tutapata jipya

    ReplyDelete
  5. Kikwete kuwa jasiri na mwenye kauli thabiti, sasa kusema wale wanaovuruga wahamishwe siyo suluhisho lamatatizo yetu. Hao wanaovuruga wakifahamika wafukuzwe kazi na ikiwezekana wafunguliwe mashtaka mara moja. Tunaendela kulea uzembe mpaka lini? Hii inakuwa haina tofauti na enzi za mwalimu ambapo kiongozi akivuruga idara moja anahamishiwa idara nyingine ambapo pia anavuruga. Kwani hawa watu wanaovuruga wana kitu gani special ambacho watu wengine hawana? Kama ni wajuzi sana sasa ni kwanini wanavuruga tu kila siku. Aahhhggrr...hi inaboa kichizi!!!!!

    ReplyDelete
  6. Hivi solution hapo ni kuhamishwa au kufukuzwa kazi???

    ReplyDelete
  7. Hivi solution hapo ni kuhamishwa au kufukuzwa kazi???

    ReplyDelete
  8. Watanzania chukueni muda wa kufikiri angalau kwa sekunde viongozi wetu wameisha tujua kuwa tunatawaliwa ha hisia hatufikiri.Kikwete hana jipya katika hilo, huu ni ujanja wa kuwapumbaza walimu waonekane wanatetewa kwani tunaanza kuhesabu miezi kufikia uchaguzi na wanajua mchango wa waalimu katika uchaguzi,kwa vile wamewaudhi na kuwadhalilisha wengine kwa viboko sasa Kikwete anataka kuficha ubovu uliopo kama kiini macho hakuna jipya hapo.Kusema ukweli haijawahi kutokea nchi hii ikatawaliwa kienyeji kama ilivyo sasa(hata kitine kasema).

    ReplyDelete
  9. Habari ya kuhamisha watu wanaostahili kusimamishwa au kufukuzwa kazi Mh Kikwete anaichukua moja kwa moja toka kwa Mwl. Nyerere na watakaomfuata Kikwete watafanya hivyo hivyo kwa watendaji wezi, wasiojua kazi, wasio wawajibikaji n.k. - kwamba hawa watu wasiofaa siku zote hushughulikiwa namna hii -- NI KUWAHAMISHA TU ILI WAKOME - ALA!! Sababu yeye ni raisi wa nchi yetu, mwananchi wa kawaida anaweza kudhani mheshimiwa huyu anatambua kwamba "ADHABU" YA KUHAMISHWA si kitu cha kumzuia mtendaji yeyote kufanya anavyotaka. Watakaofuata watamuiga baada ya yeye kutoka madarakani. Hata hivyo, kwani adhabu za kuhamisha anazitoa Raisi tu kwa watendaji anaoweza kuwahamisha yeye au anaoweza kuangiza wahamishwe? Sidhani

    ReplyDelete
  10. Anony 12:39 PM. kwa kweli roho inauma sana ila wazo la kuwajaribu wapinzani ni sawa na kumpa chizi rungu, maana wao wana wagombea uraisi wa kudumu toka tumeingia vyama vingi mpaka leo wanaogombea ni wale wale tena walikuwa huko huko ccm kwahiyo itakuwa hatuna tofauti na JK maana itakuwa ni kuwarudisha waliko kuwa. Juhudi za Jk ni nzuri sana ila swala la kuwahamisha wataenda kuharibu watakapo hamishiwa dawa yao nikufukuzwa kazi na kushitakiwa.

    Mungu ibariki Afrika
    Mungu ibariki Tanzania
    Wapatie hekima viongozi wetu ya uongozi. Amen

    Mbariki na misupu kwa kutuunganisha wanajamii.

    ReplyDelete
  11. Enzi za Mwalimu walikuwa wanahamishiwa Mtwara. Sijui wataendelea kuhamishiwa kwa Nkapa bado au vipi...
    Hii imekaaje mpaka Rais atoe agizo watu walipwe stahili zao mara moja? Hizi sio kazi za kawaida za kila siku za waliopewa dhamana hii? Mpaka Rais aagize?

    ReplyDelete
  12. Hongera NMB kwa kuwavalisha suit Taifa stars haya ndio mambo ya kwenda na wakati na kusikiliza maoni ya watu.Mungu ibariki Tanzani

    Misupu usiitupe kapuni najua ni nje ya habari iliyopo ila nafurahi katika watu tuliochangia wachezaji wapewe suit ni mmoja wao, baada ya kuona mambo ya DINA la mchana walivyokuwa wamevaa

    ReplyDelete
  13. katiak jina la mwenyezi Muumba Jehova,,hii roho ya mzaha ishindwe nadni ya kiongozi wetu wa Taifa
    hufanyi kazi huna kazi,,full stop uku ndo kuleana mtu afundishi afanya business tu,kwanini wasichapwe mboko?
    aaagh@*,_=;// mnaboa sana

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...