Pichani ni Katibu Mkuu Kiongozi Mh. Philemon Luhanjo na pembeni yake ni Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Salva Rweyemamu
Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na maneno na vijembe ati kuwa kuna mkono wa Rais Jakaya Kikwete katika kutoa tenda ya kuzalisha umeme wa dharura iliyopata Kampuni ya Richmond.
Kiini cha maneno hayo ni kauli za baadhi ya wanasiasa zilizopazwa sauti na baadhi ya vyombo vya habari.

Tunapenda kusema, tena kwa msisitizo, kuwa maneno hayo si ya kweli na hayana msingi wowote.
Rais hajahusika na uamuzi wa tenda hiyo kupewa kampuni ya Richmond kama vile ambavyo hakuhusika na kupewa tenda kwa kampuni za Aggreko na Alstom.

Kama mtakavyokumbuka wakati ule kampuni hizo tatu ndizo zilizopewa tenda ya kuzalisha umeme wa dharura. Kampuni ya Aggreko ilipewa tenda ya kuzalisha umeme wa megawati 40 na Richmond kuzalisha megawati 105.6 pale Ubungo kwa kutumia gesi asilia. Kampuni ya Alstom ilipewa tenda ya kuzalisha megawati 40 za umeme pale Mwanza kwa kutumia mafuta ya dizeli.

Katika uamuzi wa kupewa tenda kampuni hizo, Rais hakujihusisha, hakuhusishwa na wala hapakuwepo na sababu ya kuhusishwa au kujihusisha . Hiyo siyo kazi ya Rais. Hiyo ilikuwa ni kazi ya TANESCO na Wizara ya Nishati na Madini na ndiyo walioifanya. Hayo ndiyo matakwa ya Sheria ya Manunuzi ya Umma na ndivyo ilivyofanyika.

Katika shughuli nzima ya uteuzi kulikuwa na Kamati mbili za kushughulikia upatikanaji wa makampuni ya kutoa huduma ya mitambo ya kukodi ya kuzalisha umeme wa dharura. Ya kwanza ilikuwa Kamati ya Watalaamu kutoka TANESCO, Wizara ya Fedha na Wizara ya Nishati na Madini iliyokuwa na jukumu la kutathmini wazabuni wote waliojitokeza kuomba na kupendekeza wanaofaa kufikiriwa kupewa kazi hiyo.
Kamati ya Pili ilikuwa ni ile ya Serikali ya Majadiliano (Government Negotiating Team) iliyokuwa na wajumbe kutoka Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, TANESCO, Benki Kuu na Shirikisho la wenye Viwanda kuwakilisha sekta binafsi. Kamati hii ilikuwa na jukumu la kufanya majadiliano na wale waliopendekezwa na Timu ya Wataalamu na hatimaye kupendekeza anayefaa kupewa.

Kamati ya Majadiliano ilipomaliza kazi yake ilikabidhi taarifa yake Wizarani kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Ndugu Arthur Mwakapugi ambaye naye akaikabidhi kwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Ibrahim Msabaha kwa uamuzi. Kama tulivyokwishasema mamlaka ya uamuzi yalikuwa chini yao. Hakuna wakati wowote katika mchakato wa kuamua kampuni ipi ipewe tenda alipofikishiwa Rais kwa uamuzi wake wala kutakiwa kutoa maoni.

Mambo aliyofanya Rais

Katika suala zima la kukodisha mitambo ya kuzalisha umeme, Rais alihusika katika mambo manne. Kwanza, katika kuamua TANESCO itumie mitambo ya kukodi kuzalisha umeme na Serikali igharamie ukodishaji huo.




Suala hilo lilikuwa lazima liamuliwe na yeye kwa sababu lilikuwa linahitaji Serikali kugharamia ukodishaji. Kama si hivyo lisingefikishwa kwake kwani ni jambo ambalo lingekuwa juu ya TANESCO kuamua kukodisha na kulipia. Gharama hizo hazikuwa zimepangwa katika bajeti ya serikali hivyo ilikuwa ni lazima kupata idhini ya Rais ya kutafuta hizo pesa na kuzitumia kwa ajili hiyo.

Pili, Rais alihusika katika kuzungumza na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuwaomba wakubali sehemu ya pesa waliyopanga kuipa Tanzania kama msaada kutokana na mpango wa msamaha wa madeni itumike kugharamia ukodishaji wa mitambo ya kuzalisha umeme. Walikubali, na USD 225 milioni zilitumika kukodisha mitambo ya Kampuni za Aggreko, Alstom na Richmond (ambayo baadae ikawa Dowans) na matumizi mengine ya dharura za umeme. Matumizi hayo mengine yalijumuisha pia ununuzi wa mitambo ya aina ya Watsilla ya kuzalisha megawati 100 za umeme pale Ubungo kwa kutumia gesi asilia. Mitambo hiyo imeshanunuliwa, kufungwa na tayari inazalisha umeme.

Tatu, Rais alihusika katika vikao vya Baraza la Mawaziri vilivyojadili matatizo ya upungufu mkubwa wa umeme nchini na kuamua hatua mbalimbali za kukabiliana na tatizo hilo. Moja ya hatua zilizoamuliwa kuchukuliwa, ni hii ya kukodisha mitambo ya kuzalisha umeme. Katika vikao hivyo vya Baraza la Mawaziri alitoa maelekezo ya mambo ya kuzingatiwa katika zoezi zima la kupata makampuni au watu watakaotoa huduma hiyo. Hususan, Rais alisisitiza kuwa pamoja na udharura uliokuwepo Kanuni na Sheria ya Ununuzi wa Umma zizingatiwe.

Nne, Rais alikataa Kampuni ya Richmond isipewe malipo ya awali (down payment) ya USD 10 milioni na kutaka ukweli kuhusu uaminifu na ukamilifu (integrity) wa kampuni hiyo ujulikane. Rais alikataa maombi yaliyopelekwa kwake na Wizara ya Nishati na Madini ya kumuomba aagize Wizara ya Fedha, iilipe kampuni hiyo fedha hizo. Rais aliagiza Wizara ya Fedha ibaki na msimamo wake na kuitaka Wizara ya Nishati na Madini pamoja na TANESCO wafanye mambo mawili. Kwanza, wafanye utafiti zaidi kujua undani wa Kampuni ya Richmond. Isije kuwa ni kampuni bandia wakapewa fedha wakatokomea nazo na mitambo isipatikane na hukuna namna ya kuipata kampuni wala wahusika wake. Pili aliagiza wawatake viongozi wa Kampuni ya Richmond kwanza walete mitambo, ikishafika, ndipo walipwe. Maagizo hayo ya Rais yalizingatiwa na Kampuni ya Richmond ikapewa sharti hilo. Lakini, ikashindwa kulitekeleza na kuishia kuingia mkataba na Kampuni ya Dowans iliyokuja kuleta hiyo mitambo badala yake.

Hivyo ndivyo alivyohusika Rais katika suala zima la ukodishaji wa mitambo ya kuzalisha umeme kutoka kwa makampuni ya Aggreko, Alstom na Richmond. Kama kweli kungekuwa na mkono wake wa upendeleo kwa Kampuni ya Richmond kupata tenda, iweje tena yeye ndiye akatae kampuni hiyo isilipwe fedha za kianzio mpaka kuifanya ishindwe kazi? Ndiyo maana tunasema maneno hayo hayana msingi, yanasemwa na watu ambao ama hawaujui ukweli au wameamua kutokusema kweli kwa makusudi kwa sababu
wanazozijua wao. Tunatoa ufafanuzi huu kuwafanya Watanzania waelewe ukweli wa mambo.

Watumishi wa Umma

Kuhusu watumishi wa Umma waliohusika na uchambuzi wa zabuni, majadiliano na uamuzi, napenda kuwahakikishia kuwa, Serikali imelishughulikia jambo hili na sasa linafikia ukingoni.




Mamlaka za nidhamu zimeangalia mambo mawili: tuhuma za rushwa na uzembe. Tuhuma za rushwa hazijathibitika mpaka sasa na tuko tayari kuchunguza zaidi. Lakini tuhuma ya uzembe imethibitika kwa ukweli kwamba Kampuni ya Richmond haikufanyiwa uchunguzi wa kina kuijua kampuni hiyo kwa undani kabla ya kuipa tenda. Due diligence haikufanywa. Kwa sababu ya makosa hayo mamlaka za nidhamu husika kwa watumishi hao zitawachukulia hatua zipasazo kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Utumishi.

Wenzetu hawa waliridhika tu na maelezo ya mwakilishi wa Kampuni ya Richmond aliyetosheleza masuala ya kuwa na mitambo ya kuweza kuzalisha megawati 105.6, mitambo ambayo itafaa kwa mfumo wetu wa umeme, itapatikana kwa wakati na umeme kuuzwa kwa bei nafuu. Ni kweli kwamba kampuni hiyo iliwashinda wazabuni wote kuhusu masharti hayo lakini walisahau msemo wa wahenga kuwa “si kila king’aacho ni dhahabu.” Naamini wangefanya uchunguzi wa kina kuhusu kampuni ya Richmond wangegundua kuwa ni ya bandia na haikuwa na uwezo wa kifedha wa kutekeleza zabuni ile. Kwa sababu ya upungufu huo hatua zipasazo za kinidhamu zitachukuliwa kwa kila mmoja kwa kiwango chake cha kuhusika.Yaani kwa uzito wa kosa lake. Kazi hiyo imeanza na inaendelea kufanyika.

Imetolewa 01 Agosti, 2009


PHILLEMON LUHANJO
IKULU,


KATIBU MKUU KIONGOZI


DAR ES SALAAM.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 23 mpaka sasa

  1. luhanjo baba ni taarifa ya kiswahili hakukuwa na haja ya kutupia-tupia kiingereza. haya ukamilifu ndio integrity? integrity ni uadilifu.

    ReplyDelete
  2. upuuzi mtupu!! taarifa hii ina ualakini.

    ReplyDelete
  3. kwa kuwa taarifa hii imekuja kupitia kwa blog ya mithupu (maana si ya jamii kwa 100%) binafsi siwezi kuchangia chochote. maana tukisema ukweli tu atakachofanya ni kutotoa na hivyo kupoteza maana halisi ya kuileta hii habari kwa jamii.

    ReplyDelete
  4. Wakati wa uchaguzi ukiwa unakaribia utajua tu, maana wanasiasa wataanza kujiosha kwa kila jambo.

    Kama mambo mengi yalifanyika kwenye vikao vya Baraza la mawaziri, mwenyekiti wa vikao lazima apewe taarifa.

    ReplyDelete
  5. NDIO MZEE TUNASUBIRIA TAARIFA YA JULIUS NYERERE INTERNATIONAL AIRPORT - JNIA KWA HAMU KUBWA.

    ReplyDelete
  6. Huu ni mwanzo , mtafanya damage control nyingi sana kwani Serikali hii ya Kikwete hiko kwenye cruise control mode; kuna upungufu mkubwa wa uongozi.

    ReplyDelete
  7. Based on what Luhanjo said, There was no reason for Lowassa to resign. How does he explain Lowassa's resignation?

    Same old B.S

    ReplyDelete
  8. MAWAZIRI NI WATENDAJI WA RAISI NA KAMA MAKOSA LAZIMA RAISI AKUBALI MAJUKUMU NA KUFANYA MAAMUZI YA UWAJIBIKAJI. NCHI IMEINGIA HASARA KUBWA MAAMUZI YALIYO FANYIKA KUTOKA IKULU NI YA UBABAISHAJI. KWAHIYO LAZIMA RAISI ACHUKUWE MAJUKUMU YA KUONGOZA SEREKALI DHAIFU.

    ReplyDelete
  9. Mzee Luhanjo kama Mh. Rais, Wewe na Salva mnakubaliana na uchunguzi wa kamati teuli ya Bunge kuwa wakubwa Mwanyika na Hosea walizembea basi kuwaonya tu hakutoshi mzee kwa uzembee waliofanya uliolisababishia taifa hasara kubwa kiasi hicho. Mnajua hiyo pesa tuliyoilipa Richmond Feki kwasababu ya uzembe wao ingeokoa vifo vingapi vya watanzania kama inegwekezwa kwenye huduma ya afya au usafiri? Mwambie Mjombe muda wa kuwachukulisha kilicho chao umefika.

    ReplyDelete
  10. Nchi ya wajinga haikosi vituko kama hivi.

    ReplyDelete
  11. What a show this Gov. is puting up. Yeye si ndiye mwenyekiti wa baraza la mawaziri ? Inawajibika moja kwa moja lolote litakalotokea kwnyw maamuzi yake,hata kama kafanya tarishi,wacha tu waziri. Na kwanini maagizo anayotoa kwa wasaidizi wake hayafuatwi ? Kama wanafanya hivyo kwake, je unafikiri watatufanyia nini sisi walala hoi ? Kama hakuhusika,sasa kigugumizi cha nini kwenye kuwawajibisha hao waungwana wake ? Mbona mnatufanya hamnazo jamani nchi hii ni yetu sote ? Na tena hata baada ya bunge kuamua,bado tu kuna utata ? Sasa ni nani atasikilizwa? Maana,maana maamuzi ya mahakama nayo hayafui dafu kwa serikali, rejea kesi ya mgombea binafsi ? Nchi hii inahitaji kuombewa tu,labda itatusaidia. Ndugu zanguni masheikh na wachungaji, ingieni kazini sasa !!

    ReplyDelete
  12. Tunazo data kabisa kuwa Presidaa alijua na hata Mheshimiwa Luhanjo alijua kabisa kuwa huo mradi ulikuwa na mkono wa nani? Wakati kila mmoja anajua kuwa kulikuwa na wizi wa million 150 wiki hii pale benki ya NBC Temeke, kwa nini rais wetu asijue wizi wa mabilion ya shilingi zilizochotwa na Richmond? Basi kama ni hivyo Bongo hatuna rais. Kazi ya Rais ni nini kama siyo kusimamia shughuli za kila siku za nchi yetu? Mara ngapi watu wanaitwa Ikulu kwenda kuhojiwa kuhusu mambo mbalimbali lakini hili la Richmond likaachwa liendeleze kuiumiza nchi kwa faida za wakubwa. Hii riport naikataa>>>>

    ReplyDelete
  13. Sasa kama si kazi ya Rais kutaka kujua tenda zimetolewaje imekuwaje ameingilia au aliingilia malipo? Bwana au mheshimiwa Luhanjo hapo kuna kiini macho au hukutaka kutuelewesha hayo?
    Naomba kutoa hoja!

    ReplyDelete
  14. serikali isipende mchezo huu mchafu wa kusafishana. kama kiongozi alifanya uzembe hup ni udhaifu wake na kuwajibika ni muhimu. tunaona viongozi wengi tu ambao wamefanya uzembe,lakini inapofikia kuwajibishwa serikali inajifanya kama mbwa anayejificha uso ktk nguzo ya simu au umeme akidhani haonekani kiwiliwili chake baada ya kufanza zali.
    corruption is like garbage,it must be removed every day!kama ilifanyika kitu chafu mwanzoni msidhani haiendelezwi ktk mlolongo huu wa kujisafisha. mheshimiwa benja enzi za utawala wake tuliona alivyomkemea judge,sasa kama alifikia kumkemea msimamizi wa sheria imani ikowapi kuwa haki itatendeka?kuweni wakweli na wawazi kwa vitendo. kama ulishika kinyesi kubali ukaoge hakuna kufanya watu wajinga hapa.utaonekana muungwana.
    juzi tu dereva wa basi alisababisha ajali ikaua watu korogwe,huyo sheria kwake ni mara moja,lakini hawa mabosi ambao wao ikifika zamu yao kuingiza shingo kitanzini wanaona sio haki yao lakini wanasahau kuwa kuna vichanga vinakufa huko vijijini kwa ajili ya maamuzi yao!sitasahau neno hili"HATA KAMA NI KULA MAJANI ACHA WALE LAKINI LADA ITANUNULIWA" hao ndio wakubwa wetu,leo hii ukisema,hawatakosa neno la kuweka ili kufunika.

    ReplyDelete
  15. ubaya hauna kwao wala hauna kabila,
    unacheka nao na wabaya ni haohao,
    unakula nao na wabaya ni haohao.
    hii taarab inadhihirisha kile kinachofanywa na serikali yetu sasa,mtambue kwamba mzimu wa nyerere una wa haunt wale wote waliohusika kuiendesha ktk kleptocracy kwa kujineemesha na ku abuse power.
    sasa mtambue kwamba wabaya huwa hawazaliwi wakiwa na roho mbaya,bali hutengenezwa hapahapa duniani. nyie leo ni mashuhuda,kwamba wakati wa enzi za mwalimu ni jambazi gani angethubutu kuingia katikati ya mji na kupora mamilioni ya fedha mchana! lakini leo hii serikali ndiyo inacheka na ugonjwa huu mchafu. matokeo yake yakiwafika watu kooni badala ya kwenda kuiba NMB kwa mabomu,watawapigeni nyie hayo mabomu barabarani. maana wataona serikali yao inawasalati hadharani kwa kujineemesha wachache.
    dhambi ikemee kwa kuitaja jina tena hadharani nayo itakoma!lakini kwa style hii ya kukaa chini na kutunga mashairi matamu kuuhadaa umma kwamba hakuna dhambi iliyotendeka hakutatufikisha mbali. hii ni sawa na kufunga kidonda kitambaa ili kisionekane wakati usaha unatunga ndani. kubalini mkamuliwe jipu nchi ipone tupige hatua na kuacha upuuzi huu wa kuzungumzia swala hili miaka nenda miaka rudi.
    kama askofu kachafuka,haimaanishi kuwa biblia sio safi,na kama sheikh kachafuka haimanishi kurani imechachafuka. kuweni wanaume wa kazi,zamani ktk jamii zingine kijana/mwanaume alikuwa akileta aibu ktk jamii hajifichifichi,anajitokeza na kukubali na kuadhibiwa wakati mwingine hadi kuuwawa na kuiacha jamii safi. serikali acha kurudisha kiuno nyuma,kanyaga twende rigwaride rimekorea!

    ReplyDelete
  16. wote ni mafisadi, kumbaf

    ReplyDelete
  17. Huku kutufanya Wadanganyika hatujaenda shule iko siku hata mawe tu yatasema mnatunea katika nchi yetu wenyewe!Jamani naomba kumuuliza Luhanjo mwenye Dhamana au aliyepewa ubia na wananchi wa kuongoza nchi hii alikuwa Lowassa au mwingine?????????????????????????? Hivi ni nani mwenyekiti wa baraza la mawaziri! Hili kwa kweli nimenikera sana hii ni kama kutufanya watanzania wote tumeishia darasa la nne!

    ReplyDelete
  18. Naona mheshimiwa yeye anataka kuiba kwa style ya pekee, hii ni kama kupiga kidonda alafu kupuliza taratibu... teh teh

    Wizi, Rushwa na Ushenzi wa aina hii umekuwepo kwa miaka mingi, lakini hawa mafisadi wa siku hizi, yaani hawaogopi kabisa, hata baada ya kutambua kwamba macho ya watanzania yashafunguka.

    Ufisadi Mkuu Part 1: Ulianza rasmi 1995, baada ya Mkapa alipotangaza mpango wake wa kubinafsha mashirika yote ya huma kabla ya 2005. Imekaaje hiyo? Kwa mtu mwenye akili timamu utagundua tu, hawa mafisadi walishajipangia miaka kumi ya kugawana mali za watanzania. Kwa nini aweke deadline inayoendana na mwisho ya awamu yake ya urasi?
    Ukichambua vizuri utagundua kwamba mashirika haya yote waligawana wenyewe kwa wenyewe.
    Kikomo cha CCM na wala rushwa wote kimefika.

    Ufisadi Mkuu Part2: Serikali ya Mh Kikwete, ikaingia madarakani ikakuta wataalamu washamaliza msosi wote mezani. Ikabidi watengeneze mchongo wao wa kula. Tender (Zabuni) zikaanza kutolewa, EPA & Richmond na nyingine nyingi.

    Tanzania haya mambo yataisha lini, tunaitaji mabadiliko makubwa ili kuweza kupata maendeleo ya ukweli kwa nchi nzima.
    Majengo marefu, Simu za mikononi, Laptop, Matv ni vijisehemu tu vya maendeleo. Wacheni kubweteka. Tudai kuwajibishwa kwa wale wote walilolitia taifa hasara kubwa.
    Ili hata kwa viongozi wa kesho watambue kwamba kuingia kwenye uongozi inabidi uwe na moyo wa kulifanyia kazi taifa na wanchi.
    Watu wengi wanaingia kwenye siasa kutafuta pesa. Tukate hiyo ili tuwaondoe mashetani(fisadi waliokubuu) ili tubakize viongozi safi.

    ReplyDelete
  19. mh hebu nyie wenzangu semeni, manake mimi nimechoka hapa hasira debe natamani nimrukie mtu usoni!! nyani si nyani sokwe si sokwe basi tu ali mradi. huku sasa ni kutaka kuchokozana watu waseme muanze kusema watanzania wanatukana viongozi mitandaoni!! sasa hizi ni pointi za katibu kukaa chini kuandika na kutulea sisi?? aagh bwana ee haya ngoja tuone tutaishia wapi.
    KINACHOTUTESA WATANZANIA SI UONGOZI MBOVU ULIOPO BALI NI SISI WENYEWE!!!! SIKU TUKIAMUA YAISHE YATAKWISHA trust me!!!!
    ahsanteni, ahsante pia michuzi kwa taarifa, lakini pia sikulazimishi kutoa maoni yangu ni utashi wako kama kawa.

    ReplyDelete
  20. “The ultimate tragedy is not the oppression and cruelty by the bad people but the silence over that by the good people.”
    Martin Luther King Jr.
    M.Bugoye

    ReplyDelete
  21. Jamani Watanzania tushirikiane kuikataa hii nondo. Naikataa.

    ReplyDelete
  22. Sasa, hapo mnachofanya si ndio kile kile alichofanya Hosea halafu mkampigia kelele?

    ReplyDelete
  23. Ndugu wajumbe mie kwa upande wangu nimeshachoka na hadithi hizi za sungura kwa upande wangu wabunge ningewashauri kupiga kura ya kutokuwa na imani na serekali maana tutadanganywa mpaka lini!! Kila mtu mwongo mwongo tu tutafika kweli.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...