JK akifunua kitambaa kuashiria kuweka jiwe lamsingi katika kiwanda cha Tanzania Breweries Limited (TBL) Tawi la Mbeya leo mchana.Kushoto anayepiga makofi ni Mwenyekiti wa Bodi ya TBL Waziri Mkuu mstaafu David Cleopa Msuya na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TBL Bwana Robin Goetzsche.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bia Tanzania TBL Bwana Robin Goetzsche akimwonesha JK mitambo ya kisasa ya kuzalisha bia muda mfupi baada ya Rais Kikwete kuweka jiwe la msingi katika kiwanda hicho mjini Mbeya leo mchana.Kushoto ni meneja wa kiwanda hicho Bwana Calvin Martin.
HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO TANZANIA, KATIKA SHEREHE YA KUWEKA JIWE LA MSINGI LA KIWANDA CHA BIA CHA TBL MBEYA TAREHE 1 NOVEMBA, 2009

Mheshimiwa Cleopa David Msuya, Waziri Mkuu (Mstaafu)
Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Bia (TBL);

Mheshimiwa Mary Nagu, Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko;

Mheshimiwa Mwakipesile, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya;

Waheshimiwa Wajumbe wa Bodi ya Kampuni ya Bia;

Menejimenti, Uongozi na Wafanyakazi wa Kampuni ya Bia;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Nianze kwa kuushukuru uongozi wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa kunishirikisha katika shughuli hii adhimu ya kuweka jiwe la msingi la kiwanda cha bia cha Mjini Mbeya.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha chini ya miaka mitatu nashiriki katika shughuli inayohusu upanuzi wa shughuli za Kampuni ya Bia Tanzania. Mara ya mwisho, tarehe 20 Januari 2007, nilishiriki kwenye sherehe za upanuzi wa Kiwanda cha Bia cha TBL mjini Mwanza. Nawashukuru sana kwa kuendelea kunishirikisha katika shughuli zenu.

Nawapongeza sana kwa mafanikio haya makubwa. Lakini vilevile, napenda kuwapongeza kwa sababu kadhaa:
Kwanza, hatua hii, ya uwekezaji mkubwa kama huu wa dola 56 milioni, ina maana kubwa sana kwa nchi yetu hasa katika kipindi hiki ambacho uchumi wa dunia unayumba na uwekezaji kwenye maeneo mengi umeshuka au kusimama kabisa. Mnatusaidia kujenga imani kwa wawekezaji wengine kwamba, licha ya hali mbaya ya uchumi duniani, Tanzania bado ni nchi nzuri yenye matumaini na yenye mazingira mazuri ya uwekezaji na ambayo mwelekeo wa uchumi wake unaruhusu uwekezaji mkubwa kama huu. Kwa hili, nawapongeza na kuwashukuru sana.
Pili, nawapongeza sana kwa kuendelea kuwa mfano mzuri wa mafanikio ya sera yetu ya ubinafsishaji. Kuanzia mwaka 1993, kampuni hii imebadilika kutoka kuwa kampuni iliyokuwa inaendeshwa kwa tija ya chini na uzalishaji mdogo, hadi kuwa kampuni yenye ufanisi mkubwa, tija ya hali ya juu na uzalishaji mkubwa. TBL leo ni kampuni inayopata faida kubwa na kutoa gawio kwa wanahisa wake. TBL sasa ndiyo mlipaji kodi mkubwa kuliko makampuni yote nchini. Watu wengi zaidi wamepata ajira moja kwa moja katika kampuni hii na wengine wengi zaidi wameajiriwa na kujiajiri kwa sababu ya shughuli za kampuni hii. Wapo wakulima wengi ambao wanauza shairi na mahindi kama malighafi. Wapo watu wengi wamepata ajira katika vilabu vya pombe kwa kuuza bia za TBL.
Mheshimiwa Mwenyekiti wa Bodi, Mheshimiwa Waziri na Wageni Waalikwa;
Nawapongeza sana pia kwa uamuzi wenu wa kujiandikisha na kuuza hisa za TBL kwenye Soko la Mitaji la Dar es Salaam (Dar es Salaam Stock Exchange). Kutokana na uamuzi huu, zaidi ya asilimia 11 ya hisa za kampuni hii zinamilikiwa na wananchi wa Tanzania. Hili ni jambo zuri ambalo linapaswa kuigwa na makampuni mengine makubwa nchini.
Ndugu Mwenyekiti, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Nimefurahishwa sana na uamuzi wa TBL wa kununua sehemu kubwa ya malighafi ya uzalishaji bia kwa kiwanda hiki hususan shairi kutoka Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Nimefarijika pia na taarifa kwamba TBL kupitia mpango wenu wa SAIDIANA PROJECT mmejipanga kuwashirikisha wakulima wadogo wadogo kulima shairi kwa matumizi ya kiwanda hiki na vinginevyo.
Kutokana na mradi huu, wakulima takribani 10,000 watanufaika. Hili ni jambo jema sana. Nawasihi wakulima wa kanda hii kujipanga vizuri kuitumia fursa hii ili kuweza kukidhi mahitaji ya kiwanda hiki.
Ni matumaini yengu kuwa TBL itashirikiana na viongozi na wakulima wa maeneo haya katika kuandaa mpango madhubuti wa kuingia mkataba (contract farming) na wakulima watakaokuwa tayari kuwekeza katika kilimo cha Shayiri. Ni jambo la faraja kwamba kampuni ya Bia Tanzania iko tayari kujihusisha na uendelezaji wa kilimo cha zao za shayiri ambalo ni muhimu kwa uzalishaji wa bia kiwandani.
Mhe. Mwenyekiti,
Nimefurahi pia kusikia na kuona kuwa, katika kiwanda hiki, TBL itatumia teknolojia mpya za kisasa kuongeza tija na uzalishaji pamoja na kupunguza uchafuzi wa mazingira. Naambiwa kwamba teknolojia hii itasaidia ufanisi katika matumizi ya maji pamoja na nishati. Nawapongeza sana katika harakati hizi za kuhakikisha kwamba maendeleo ya viwanda yanazingatia utunzaji wa mazingira.
Upatikanaji wa Umeme
Mhe. Mwenyekiti, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Natambua kwamba Serikali inalo jukumu la kuhakikisha kwamba mazingira ya biashara na uwekezaji yanakuwa mazuri. Napenda kutumia nafasi hii kuwahakikishia kuwa Serikali itafanya kila iwezalo kutimiza kwa ukamilifu wajibu wake huo. Naamini kufanikiwa kwetu kufanya hivyo ndilo jambo lililoshawishi TBL kupanua uwekezaji wake nchini na kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa bia.
Natambua kwamba hali ya umeme, katika miezi ya hivi karibuni, imekuwa sio ya kuridhisha na kuwa mtihani mkubwa katika uendeshaji wa viwanda nchini vikiwemo vya TBL Dar es Salaam, Arusha na Mwanza, uzalishaji umekuwa unaathirika na gharama zimepanda. Tumedhamiria kulimaliza tatizo la sasa na tumeweka mipango mizuri ya baadae ya kumaliza kabisa tatizo la upungufu na kukatikakatika kwa umeme nchini. Hatua ya juzi ya kuanza mchakato wa kuwasha mitambo ya IPTL ni sehemu ya mikakati na mipango ya kumaliza tatizo la sasa. Aidha, ipo miradi inayotekelezwa na itakayotekelezwa katika muda mfupi na wa kati ambayo italipatia taifa umeme wa kutosha.
Miundombinu ya Usafirishaji
Mhe. Mwenyekiti,
Nafahamu pia kwamba biashara ya bia inastawishwa na miundombinu ya uhakika ya usafirishaji kuwezesha usambazaji kuwa mzuri kote nchini. Mkakati wa Kampuni ya Bia kuanzisha viwanda na depots katika sehemu mbalimbali nchini unasaidia katika hili. Sisi katika Serikali tunatambua vyema jukumu letu la kuimarisha miundombinu ya barabara na reli. Napenda kuwahakikishia kuwa hatutarudi nyuma katika juhudi zetu za kutimiza kwa ukamilifu wajibu wetu huo.
Hitimisho
Ndugu Mwenyekiti,
Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama nitamaliza hotuba yangu bila ya kutambua kazi nzuri inayofanywa na Kampuni ya Bia (TBL) ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii. Mmefanya mengi na mnaendelea kufanya mengi mazuri. Nawaomba muendelee na moyo huo huo kwa maslahi ya taifa letu na watu wake.
Ni matumaini yangu kuwa kiwanda hiki cha bia kitakapokamilika kitaongeza mchango wa TBL kusaidia jamii.
Nawatakia kila la heri katika ujenzi wa kiwanda cha bia cha Mbeya.
Mhe. Mwenyekiti, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Asanteni sana kwa kunisikiliza.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. JAMANI MIE NINGEKUWA RAISI NISINGEKUBALI KUWEKA JIWE LA MSINGI KWENYE KIWANDA CHA BIA...SASA KAMA RAISI ANAFUNGUA KIWANDA CHA NA WANAINCHI WATAFANYAJE SASA..

    ReplyDelete
  2. Masikini JK hajuwi ni dhambi kubwa kwa muislam kushiriki katika mambo
    ya ulevi.

    ReplyDelete
  3. Acheni itikadi zenu za extrimism hakupigiwa kura na Waislam pekee! na serikali haina dini!

    ReplyDelete
  4. Wewe ano umeambiwa utoe maoni kuhusu hiyo mada sio ujadili maoni ya mtu mwengine.Hata wewe ni extrimist.Serikali haina dini bali wa Tanzania wanayo dini.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...