Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania
Tahadhari Kuhusu Ongezeko la
Vyuo Vikuu Batili (Degree Mills)

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imepewa mamlaka ya kisheria kuthibiti na kusimamia ubora wa viwango vya elimu na mifumo inayotumiwa na vyuo vikuu katika kukidhi viwango vya ubora wa elimu ya juu, kusimamia uthibiti na kuhakiki uhalali na viwango vya kitaaluma vya tuzo za digrii na stashahada zinazotolewa na taasisi za elimu ya juu ndani na nje ya nchi.

Ifahamike kwamba, tuzo hizo zinahusisha pia digrii za heshima ambazo vyuo vikuu vimepewa mamlaka ya kuwatunuku watu ambao chuo husika kimeona ama mtarajiwa kupewa digrii hiyo ametoa mchango mkubwa wa kitaalam katika eneo lake la kitaaluma, au ametoa mchango mkubwa katika masuala ya kuhudumia ustawi wa jamii. Utoaji wa tuzo za aina hii kwa kawaida ni uamuzi wa vyuo husika kwa kutumia mifumo yao iliyowekwa kisheria inayotoa mamlaka kwa chuo kufanya hivyo.

Kwa mantiki hiyo, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania inatambua na kukubali uhalali wa digrii za heshima zilizotolewa na vyuo vikuu vilivyothibitishwa na vinavyotambuliwa na serikali au taasisi zilizokasimishwa mamlaka ya kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, digrii za heshima haziwezi kutumika kama sifa ya kitaaluma, kwenye jina la mhusika au vinginevyo, katika kutafuta ajira, kupandishwa cheo, au kama msingi wa kujiendeleza kielimu.

Katika miaka ya hivi karibuni Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania imebaini ongezeko la tuzo za digrii za uzamivu za heshima, yaani “honorary doctorates (honaris causa)” zikitolewa kwa watu wenye haiba na wadhifa mkubwa katika maeneo mengi ya Afrika. Hali hii pia inaongezeka kujitokeza kwa kasi nchini Tanzania. Haishangazi kuona kwamba katika kipindi cha muongo mmoja uliopita na hadi sasa hivi, watu maarufu wamekuwa wakitunukiwa digrii za aina hii kutoka katika taasisi ambazo kutambuliwa kwake kunatia shaka siyo nchini Tanzania tu, bali hata katika nchi zilimo taasisi hizo.

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania inastushwa sana na suala hili la ongezeko na nyendo za taasisi na vyuo vikuu visivyotambuliwa nchini Tanzania na kwingineko duniani, ambavyo vimepewa jina la utani “viwanda vya kutengeneza digrii au stashahada”, yaani “degree mills”, ambavyo vinawadanganya Watanzania kwa kuwatunuku digrii za uzamivu za heshima.
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania inatambua madhumuni potofu ya ongezeko la vyuo hivyo bandia hapa nchini kwetu. Mantiki na matokeo ya digrii zitolewazo na vyuo hivyo batili kwa wanaotunukiwa na kwa jamii wanayoitumikia ni hatari na inawapunguzia heshima watunukiwa hao wao wenyewe na taifa zima kwa ujumla.

Kwa hiyo basi, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania inatahadhalisha umma kuwa makini ili kuepuka wasitapeliwe na taasisi ambazo ni “viwanda vya kutengeneza digrii”, ambazo kwa hakika nia yao ni kujipatia pesa au kutafuta umaarufu kwa njia zisizo halali. Licha ya kutunuku digrii bandia za heshima, taasisi hizi pia zimewatapeli watu wengi pamoja na watanzania kwa kuwatunuku digrii, digrii za uzamili na hata za uzamivu (yaani doctorate degrees) bila ya wahusika kufanya kazi yoyote ya kitaaluma inayolingana na matakwa ya kutunukiwa digrii walizopewa, kwa kuwa tu waliweza kulipia gharama za digrii hizo.

Baadhi ya taasisi zinazotoa tuzo za digrii, na digrii za uzamivu za heshima zimefika mbali zaidi kwa kudai kuwa eti wanafanya hivyo kwa ajili ya kutoa heshima kwa Bara la Afrika kwa kuwa Waafrika walioleta mafanikio hawaheshimiwi na kuenziwa ipasavyo humu humu Barani Afrika, na kwa sababu hiyo pengo hilo linazibwa kwa kupewa tuzo ya digrii za uzamivu za heshima. Walengwa hasa ni watu maarufu na viongozi ikiwa ni pamoja na Marais na Mawaziri wa nchi zetu za Kiafrika, Wabunge, n.k.

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania inaamini kuwa huu ni upotoshaji na kukwepa ukweli kwamba kwa hakika digrii nyingi za aina hii zinatolewa kwa misingi ya kubadilishana fedha au kutangaza umaarufu wa taasisi husika. Mfano wa taasisi za aina hii uliandikwa katika makala iliyotolewa hivi karibuni katika gazeti la “The Guardian” la hapa nchini la Jumatatu tarehe 19 Julai, 2010 ikihusisha taasisi moja ya kidini nchini Marekani. Imethibitika kuwa anwani ya mahali ilipo taasisi hiyo haiko bayana na taasisi hiyo haitambuliwi na nchi yoyote ya Kiafrika na hata nchini Marekani kwenyewe.

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania inapenda kutahadhalisha umma kuhusu kuwepo kwa matukio haya na kutoa ushauri kwa yeyote anayehusika kuwasiliana na Tume kwa ajili ya ushauri na uthibitisho wa masuala yote yanayohusu elimu ya juu ili kuepuka kutumia gharama kubwa zisizo za lazima kupitia njia za mkato na hatimaye kutunukiwa “digrii ya kutengenezwa”, digrii isiyokuwa na thamani, iwe ya heshima au vinginevyo.

Prof. Mayunga H.H. Nkunya
KATIBU MTENDAJI
TUME YA VYUO VIKUU TANZANIA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 15 mpaka sasa

  1. Huraay!! It is about time wenye initials za Dr tuanze kuwauliza wamepatia wapi huo u-Dr ndio tutawaumbua watu wanaoingilia fani za watu!

    ReplyDelete
  2. Yap!!! all people who hold fake Degree stand & get away now before anything goes worse, ni kweli kabisa watu tunasumbua vichwa na kusoma Finace watu wengine tunabaniwa kukaa kwenye position tezu toa hao wenye kutaka urahisi wa maisha tuingie wapiga kitabu

    ReplyDelete
  3. Hii tume nayo ni michosho pia au pia feki..Inashindwaje kuandkika lists hata ya Vyuo vya nyumbani na nje ambavyo sio kanyaboga?

    Kuna kazi gani ngumu kusema chuo hiki ni sawa na hiki sio...na kama mnaenda Uk...someni kwenye vyuo hivi, Norway hivi, India hivi?
    Au nini kazi yao, kukalia habari? waweke kwa website kama wako serious?

    ReplyDelete
  4. Annoy wa tatu kutoa maoni umesema kitu ambacho ni point hata mimi nashindwa kuelewa hiyo tume tena inafanya kazi gani, wangeorodhesha vyuo ambavyo ni halali, na si ajabu hata ukienda kuuliza pale ofisin kwao mikocheni wakupe ushauri utaishia kuambulia majibu machafu yasiyo na tija, kejeli, dharau, kuna wengine hawapendi kwenda kusoma vyuo feki isipokua tu ni kutokua na taarifa sahihi, tuamke watanzania tuache kufanya kazi kwa mazoea panapohitajika kuwapa watu taarifa wape usizikalie ofisin asilimia 80 hiyo tumehamna mnachokifanya.

    ReplyDelete
  5. Professor Mkunya umebaki tu kusema taasisi yake ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia utoaji wa vyeti vya elimu vinavyotumika nchini viwe vya ndani au nje ya nchi. Watu wengi tu wamesharipotiwa kuwa wana degree za viwandani, sasa wewe na taasisi yako umechukua hatua gani ambayo inaonekana?

    Inatia sana uchungu kuona mtu anakula starehe mitaani kila siku baadaye unasikia eti ni Dr wakati watu wengine wanafanya kazi ya ziada kupata hiyo degree. Miaka minne watu wanazota kutafuta PhD huku wengine wananunua halafu hakuna hatua yeyote ya maana imechukuliwa na hiyo Taasisi ya Prof Nkunya.

    Hivi hiyo taasisi haina mamlaka ya kisheria kumchunguza mtu mwenye degree na kama ikigundulika kweli si halali anapeleke mahakamani kama kosa la jinia?

    Fanya mambo ya onekane kama kweli mna mamlaka ya kusimamia hutoaji wa vyeti vya elimu ya juu Tanzania. Sio kusema tu kila siku ohoo unajua sisi ndio tuna mamlaka ya kusimamia utoaji wa vyeti, wakati watu wakiendelea kutengeneza vyeti feki na kujipatia umaarufu wasiositahili kuwa nao.

    ReplyDelete
  6. Hivi wewe anony wa tatu hapo juu naona ni kama huelewi unachoongelea. Ulimwengu mzima una mamilioni ya Universities. Hao TCU wataweza kweli kuorodhesha vyote wakitengasnisha feki na halali. Hili ni kwamba haliwezekani hata siku moja.
    Mdau

    ReplyDelete
  7. SISHANGAI KIASI NCHI ZINGINE WAOGOPE VYETI VINAVOTOKA AFRICA NA ASIA

    ReplyDelete
  8. TUNAOMBA ORODHA YA VYUO KANYABOYA NA VILE VISIVYO KAYABOYA NYUMBANI NA UGENINI.TUNAAMINI KUWA WASOMI HUFANYA RESEARCH KABLA YA KUFIKIA CONCLUSION. TUNAAMINI KUWA TUME HII NI YA WASOMI WANAOFUATA MAADILI YA ELIMU WALIYOPATA NA WENYE MAPENZI MEMA NA NCHI YETU.

    ReplyDelete
  9. HAMNA LOLOTE WIVU TU KWA SABABU WATU WANAJIKATA KWENDA KUSOMA MBELE,NYINYI MMESHINDWA KUBORESHA ELIMU TOKA MWANZO LEO MMESHTUKA NDIO MNAANZA KUJENGA VYOU VIKUU NA MNAKOSA WANAFUNZAI MNADAI VYETI FEKI ILI WATU WABAKIE BONGO,KAMA KWELI NI KUHUSU VYETI FEKI POA ILA NIONAVYO MIMI HUU NI UPUUZI MTUPU NA FITNA,BADO VIJANA TUTAKIMBIA TENA MBIO SANA NA TUKIRUDI TUNACHUKUA VITI VYENU,EBOOOO

    ReplyDelete
  10. Huyu katibu wa hii tume nadhani alitakiwa kuweka hata mawasiliano ya baruapepe au fax na kadhalika ili tuwasiliane nae.

    kwa kifupi hii tume nadhani inatakiwa ifunguke macho kwa sasa dunia imekuwa kijiji,wanatakiwa kajua vyuo vyote katika kila nchi na waviweke katika ubora wake ili hata washikadau waweze kujua na kufanya maamuzi sahihi,hapa nikiongelea washika dau nawalenga wanafunzi na waajiri.

    mtu unatoka nje umepiga book kwa usongo na unaporejea bongo wanasema eti degree au masters yako haitambuliki sababu chuo hakitambuliwi na tume ya Tanzania,
    kwa kweli haya yanakuwa matusi kwa namna moja au nyingine kwa sisi tunaosoma nje ya nchi.
    nadhani kungekuewa na utaratibu wa kuhakiki vyuo na vyeti vya wahitimu katika kila idara.
    vyuo Tanzania havina hadhi sawa hivyo basi kila nchi vyuo vina hadhi tofauti,ili kujua thamani ya cheti cha mtu ni kufanya utaratibu wa kujua chuo kipo kwenye hadhi gani na kukithaminisha cheti cha muhitimu iwe wa nje au ndani.
    nawakilisha.

    ReplyDelete
  11. Nafikiri kuwa tume haiwezi kuorodhesha vyuo vyote duniani, ni vingi mno. Ushauri wangu kwa wanaotaka kusoma UKIPATA CHUO BORA UULIZE KWENYE HII TUME KAMA CHUO HICHO KINAFAA AU LA.

    Ushauri wangu kwa tume. WEKA MAWASILIANO YENU BAYANA ILI WATU WAWASILIANE NA NINYI. Hasa napendekeza mawasiliano ya internet, wekeni website yenu wazi, ili wale wanaojali wasipoteze muda bure.

    ReplyDelete
  12. Professor Nkunya,

    Kama ni katibu muhtasi amekuandikia jaribu kupitia neno la kiswahili fasaha ni TAHADHARI na sio TAHADHALI.

    ReplyDelete
  13. walist vyuo vyote vya nje na ndani na kutambulika kwake hiyo ndiyo kazi yao, wanaweza kufanya hivyo kwa kushirikiana na nchi husika dunia mtandao hakuna ugumu wowote, mbona hapa nilipo tume yao inalist ya kanyaboya za russia na hutangazwa public, ebo...

    ReplyDelete
  14. watu mnao lalamika hapa kwamba hakuna list ya vyuo mmeshafungua lakini website ya hiyo tume?mbona manachokiomba kiwekwe mimi nilishakiona ktk website ya hiyo tume,kuna lunk unaclick inafungua unachagua nchi unapata list ya vyuo kwa alphabet. sasa kama i-net yenyewe huna usilalamike kuwa hakuna link ya list ya vyuo wanavyovitambua. sema tu tofauti kidogo inaweza jitokeza pale chuo kinapobadili jina,haimaanishi kuwa na quality yake ya elimu inakuwa imeharibika.kwamfano MUHAS ilipotoka kuwa tawi la UDSM sidhani kama kimekuwa chuo kichanga na kubadili quality ya elimu yao.

    ReplyDelete
  15. AnonymousJune 14, 2013

    Toeni basi listi ya vyuo vikuu hasa vya nje ambavyo si kanyaboya tuelewe..Wengine tunatarajia kusoma elimu ya juu majuu.....

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...