Mkurugenzi wa Chama cha kuzuia matumizi ya tumbaku Tanzania (TTCF) Bi. Lutgard Kokulinda Kagaruki (kulia) akiongea na waandishi wa habari juu ya kongamano la nne la kimataifa la kuunga mkono uidhinishwaji wa miongozo ya kudhibiti matumizi ya tumbaku.kushoto ni Mwanaharakati msaidizi wa (TTCF), Bw. Akilimali Shukuru.Mkurugenzi wa Chama cha kuzuia matumizi ya tumbaku Tanzania (TTCF),Bi. Lutgard Kokulinda Kagaruki(Kushoto) akionesha picha yenye mchoro wa mtu alieathirika na matumizi ya tumbaku leo katika ukumbi wa mikutano wa Idara ya Habari - Maelezo.kulia ni Mwakilishi kutoka mamlaka ya mapato (TRA),Bw. Shemu Simon.

Na Ripota wa Globu ya Jamii.

Wakati nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani walioridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Matumizi ya Tumbaku Duniani wakijitayarisha kuhudhuria Kongamano la Nne la Mkataba huo huko Uruguay, wanaharakati wa kuzuia matumizi ya tumbaku Tanzania wameshtushwa na mipango ya makampuni ya kimataifa ya tumbaku kupinga utekelezaji wa miongozo sahihi ya Vifungu namba 9 na 10 vya Mkataba wa Kimataifa wa Shirika la Afya Duniani wa Kudhibiti Matumizi ya Tumbaku, vinavyohusu udhibiti na kuweka wazi viungo katika bidhaa za tumbaku.

Katika miezi ya karibuni, chama kinachodai kuwawakilisha wakulima wa tumbaku duniani kimekuwa kinashawishi waziwazi dhidi ya baadhi ya vipengele vya agenda ya Kongamano la Nne la Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Matumizi ya Tumbaku.

Chama cha Wakulima wa Tumbaku Duniani (ITGA) ambacho ni chombo cha mawasiliano na umma kilichotengenezwa na makampuni ya tumbaku kwenye miaka ya 1980 kufanikisha jitihada za ushawishi wake dhidi ya mkakati wa kimataifa wa kudhibiti tumbaku, kimekuwa kinafuatilia miongozo inayopendekeza nchi zizuie au zisitishe viungo vinavyoongezwa kwenye tumbaku kuifanya ivutie zaidi hasa kwa vijana wavutaji na wale ambao hawajaanza kuvuta.

Vivyo hivyo Umoja wa Soko la Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) unashawishi nchi 19 za umoja huo kupinga zinachokiita “marufuku ya matumizi ya viungo vya ziada katika utengenezaji wa sigara”, ambavyo ni kama peremende, vanilla, lambalamba (ice cream), chokoleti nk.,.
Kwa mtazamo wa ITGA, miongozo kuhusu viungo vya ziada ikikubalika, eti itasababisha kusitishwa kwa tumbaku aina ya “burley” ambayo hukaushwa kwa mwanga wa jua na ambayo ni maarufu katika utengenezaji wa sigara za aina ya Kimarekani.

“Burley” hulimwa sehemu nyingi katika nchi zinazoendelea na ITGA inawaambia wakulima kuwa, miongozo iliyopendekezwa itasababisha janga kwenye ajira na maisha yao kutokana na upungufu wa soko la tumbaku yao.

Kitu ambacho ITGA haiwaelezi wakulima ni kwamba sigara za “burley” zinaendelea kuuzwa katika nchi ambazo tayari zinakataza matumizi ya viungo vya ziada, alisema Laurent Huber, Mkurugenzi wa Umoja wa Kimataifa wa Vyama vinavyoshughulikia Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti matumizi ya Tumbaku (Framework Convention Alliance).

Kufuatana na maelezo ya Lutgard Kokulinda Kagaruki, Mkurugenzi wa Chama cha Kuzuia Matumizi ya Tumbaku Tanzania (TTCF), tumbaku aina ya “burley” huzalishwa kwa kiwango kidogo tu ikilinganishwa na aina nyingine za tumbaku zinazozalishwa hapa nchini; hivyo hata kama ingesitishwa, isingekuwa na athari kubwa kwa wakulima.

Zaidi ya hapo, makampuni ya Tanzania hayatengenezi bidhaa za tumbaku zenye viungo vya ziada, hivyo swala la ukosefu wa ajira halitakuwepo maana ajira ya aina hiyo bado haipo. Alisisitiza kuwa jitihada zifanyike kuhakikisha kuwa bidhaa za aina hii haziingizwi nchini.

Wanaharakati wa kudhibiti matumizi ya tumbaku Tanzania, wanaiasa serikali ya Tanzania kukataa kurubuniwa na vishawishi vya makampuni ya tumbaku. Hivyo wanawasihi wajumbe wa Tanzania watakaohudhuria Kongamano la Nne la Kimataifa la Kudhibiti Matumizi ya Tumbaku kuunga mkono uidhinishwaji wa miongozo iliyopendekezwa ya Vifungu 9 na 10 bila mabadiliko.

Kuanzia tarehe 15 – 20 Novemba 2010, Uruguay itakuwa mwenyeji wa Kongamano la Nne la nchi wanachama wa WHO walioridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Matumizi ya Tumbaku.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...