Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje, Zanzibar, Mhe. Balozi Mohamed Hamza akizungumza wakati wa majadiliano kuhusu fadia na athari za utandawazi katika Mkutano wa Wajumbe wa Kamati ya Pili Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa, Kamati ya pili inahusika zaidi na masuala ya uchumi. katika mkutano huo wajumbe wengi waliozungumza walielezea kutoridhishwa kwao na matokeo ya utandawazi na kwamba kumekuwa na changamoto zaidi kuliko faida hasa kwa nchi zinazoendelea.

Na Mwandish Maalum

New York

Imeelezwa kuwa, hapana shaka yoyote kwamba, karibu kila nchi hasa zile zinazoendelea kwa namna moja ama nyingine zimeathirika na utandawazi kulivyo ilivyokuwa imefikiriwa hapo awali.

Athari za utandawazi pamoja na mdororo wa uchumi unaoikumba dunia hivi sasa siyo tu kumekwamisha ukuaji wa uchumi kwa nchi nyingi duniani , bali pia kumeongeza idadi ya watu maskini.

Kauli hizo zimetolewa na karibu wajumbe wote wa Kamati ya Pili ya Uchumi na Fedha ya Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa, wakati walipokuta siku ya Jumatano katika mkutano wao wa siku mmoja. Ambapo walipokea na kujadili taarifa mbalimbali zihusuzo masuala ya uchumi, utamaduni, sayansi na teknolojia pamoja na faida na hasa za utandawazi.

Kwa ujumla wakati wa majadialiano hayo na hasa kuhusu taarifa ya utandawazi, wajumbe wa Kamati hiyo wakizungumza kwa nyakati tofauti, wameeleza kwamba pale ambapo ilidhaniwa kwamba utandawazi ungeleta manufaa na nchi kutegemeana na kushirikiana kama kijiji kimoja. Badala yake dunia imejikuta ikigawanyika zaidi kati ya wale walio nacho na wasio nacho.

Akichangia majadiliano hayo mwakilishi wa Tanzania katika Mkutano huo, Balozi Mohamed Hamza ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar. Yeye alisema kuwa ingawa utandawazi umeifanya dunia kuwa kijiji kidogo lakini utandawazi katika Afrika haujaleta faida zilizotarajiwa.

Akizungumzia zaidi kuhusu faida na hasara za utandawazi pamoja na suala ya kutegemeana, Balozi Mohamed Hamza amesema , utandawazi unatishia hata utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millennia(MDGs) kutokana na ukweli kwamba kumekuwa na ukuaji mdogo wa uchumi, ukwasi wa raslimali fedha, uhaba wa chakula na mabadiliko ya tabia nchi.

“ kwa kweli kutokana na hayo yote na mwelekeo ulivyo hivi sasa wa hali ya dunia, tunakabiliwa na hatari kubwa ya kushindwa kufikia malengo ya maendeleo ya Millenia ifikapo mwaka 2015” akasisitza Balozi Hamza.

Akaongeza “ Ni kweli dunia bado inakabiliwa na mtikisiko wa uchumi, mtikisiko ambao madhara yake yameendelea kuwa makubwa siku hadi siku. Mtikisiko huu umerudisha nyuma mafanikio ya ukuaji wa uchumi yaliyopatikana miaka kumi iliyopitia”.

Akaongeza kwa kusema kwamba kutokana na mdororo huo wa uchumi, nchi nyingi zimejikuta zikiwa na ongezeko la watu maskini.

Naye mwakilishi wa Argentina akizungumza kwa niaba ya nchi za Kundi la77 na China, aliunga mkono kwa kusema ingawa utandawazi unaweza kuwa na nguvu ya kuimarisha ushirikiano na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo. lakini utandawazi pia umeleta changamoto nyingi hasa kwa nchi zinazoendelea.

Akaongeza kuwa nafasi pekee kwa Umoja wa Mataifa ni katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya kukuza maendeleoa katika mazingira ya utandawazi, hasa katika kuunganisha nchi zinazoendelea katika uchumi wa utandawazi.

Mwakilishi wa Libya akizungumza kwa hisia kali juu ya mwenendo wa utandawazi, yeye amesema kuwa ingawa baadhi ya watu waliamini kuwa utandawazi ulikuwa kwa ajili ya kubadilishana mawazo na kukuza biashara na bidhaa. Ukweli ni kwamba utandawazi umekuwa ufunuo wa maovu na uchoyo.

Akasema kuwa kumekuwa na ongezeko za utofauti kati ya nchi na nchi pamoja na kukosekana kwa utulivu wa kiuchumi na akatoa wito wa kuwepo kwa sera zenye kuzingatia haki na umadhubuti katika biashara ya kimataifa na kuhakikisha usawa na utulivu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Wadau naomba msaada. Nimesoma habari hii lakini sijaielewa kwa kuwa neno moj tu ndilo linlonikwamisha. Naomba mnielezee maana ya 'Utandawazi' taf. Au hata kwa lugha ya kigeni 'English'.

    ReplyDelete
  2. nazani utandawazi inamaanisha globolaisation inavyospredi faster mkuu

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...