Dah! Nilisahau leo kuwa ni Jumapili, siku ambayo natakiwa kuandika mada ya wiki  juu ya upigaji picha, kama nilivyoahidi wiki chache zilizopita. Hivyo najikuta sijajiandaa na hata topiki sijapanga iwe nini safari hii.
Hata hivyo, baada ya kupiga bongo kwa muda, nikakumbuka jambo moja muhimu sana ambalo nilinuia kulisema nitapopata nafasi. Na jambo hilo si lingine ila ule msemo kuwa picha inafanana na maneno elfu moja.
Naam! Picha haina tofauti na maneno 1000. Yaani unaweza kusema idadi hiyo ya maneno kwa picha moja tu ama mbili, na mtazamaji wa picha hiyo akapata somo ambalo vinginevyo ingekupasa uandike kurasa kama nne hivi za A4.
Nimeibuka ghafla na mada hii huku mawazoni nikiwa na timu yetu ya Taifa katika michezo ya Olimpiki inayoendelea jijini London, uingereza. Hapana, leo sizungumzii michezo na wala sina nia ya kugusia jinsi gani wawakilishi wetu wanavyotolewa kamasi huko ughaibuni.
Lengo langu la mada hii ni kukukumbusha umuhimu wa kuwa na tabia ya kuweka kumbukumbu kwa njia ya picha matukio muhimu katika maisha yetu, jambo ambalo nasikitika kusema kwamba hapa Tanzania tunalichukulia juu juu tu – yaani bora liende.
Hivi kuna ugumu gani ama tatizo liko wapi katika kuhakikisha kumbukumbu ya picha inawekwa pindi litokeapo jambo kubwa na muhimu kama michezo ya olimpiki ambayo hufanyika mara moja kila baada ya miaka mine?
Nasema hivyo kwa sababu sikumbuki kuona picha ya wanamichezo hao wakiwa ulingoni ama uwanjani, zaidi ya zile tunazopata kwa kubahatisha mitandaoni, tena zilizopigwa na watu wengine?
Ni kweli kwamba wawakilishi wetu (kwa kisingizio kile kile cha uhaba wa maandalizi) hawajafanya vyema, lakini si uwongo kwamba kulikuwa na haja, tena kubwa tu, ya kuwa na kumbukumbu ya ni nini wanakifanya ama walichokifanya huko London.
Kumbuka…picha moja sawa na maneno 1000. Hata kama hatujafanya vyema katika michezo ya olimpiki, lakini picha moja ama mbili za wanamichezo wetu wakiwa ulingoni huenda zingetuhadithia kwa nini hatufanyi vyema.
Yaani, zaidi ya vipicha viwili vitatu vya wanariadha wetu wakiagwa kwa kukabidhiwa bendera, ama safari hii walipokuwa London na kubahatika kukutana na Mhe Rais Jakaya kikwete aliyekuwa Uingereza wakati wanamichezo wetu wakiwasili huko, hatujaona taswira yoyote ya wawakilishi wetu wakiwa ulingoni.
Tutawaambia nini wajukuu wetu na vilembwe siku za mbeleni? Tabia hii, ambayo naikemea sana, naomba ikome.
Kwa nini tusiige miaka ya zamani ya akina Filbert Bayi na kina Suleiman Nyambui ambapo aghalabu  wanahabari  walipewa fursa ya kuongozana na timu, na kudaka na kuhifadhi kumbukumbu zao ambazo  tunazo hadi leo?
Najua fika kwamba kuna mitandao ya kimataifa inayokava matukio hayo, na kwamba kama angetokea mtu kushinda medali tusingekosa picha zake. Lakini kuchukulia ‘BORA LIENDE’ kwa jambo kama hili si kitu aali sana. Iko haja ya kujipanga na kuepukana na hili.
 Mikakati iwekwe kuanzia sasa kwamba mwanahabari mpiga picha asikosekane kwenye matukio kama hayo. Kuhusu gharama, sidhani kama atakosekana mfadhili mwenye uchungu na nchi yake kupiga jeki japo mpiga picha mmoja aongozane na wawakilishi wetu.
Na hapa  natoa changamoto kwa Chama cha Wapiga Picha nchini....
Wakubwa, tuweke mikakati ya kuwa na mwakilishi wetu katika matukio makubwa kama Olimpiki! 
 Tujipange, tupige harambee ama tuombe  ufadhili na kumtuma mwenzetu akatudakie kumbukumbu hizi muhimu kwa Taifa letu la leo na kesho.

Naomba kuwasilisha…
ANKAL






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 9 mpaka sasa

  1. Ankal hili sasa linaelekea kuwa janga maana linashuka kwa kasi hadi katiaka ngazi ya kaya / familia.
    Teknolojia ya Digital photos ndio kabisa inatumaliza. Tunapiga picha nyingi ambazo zinaishia kwenye electronic gadgets kama simu, computers, memory cards. Matokeo yake ni kuzifuta ili kuendelea kupiga nyingine au kupotea kwa kuharibika, kuibiwa kwa vifaa hivi.
    Tunahitaji kuelemishana juu ya njia za kufanya ili kuhifadhi kumbukumbu za picha.
    Kwangu bado zile conventional photo albums ndio suluhisho pekee la kudumu.

    ReplyDelete
  2. Nakubaliana nawe kabisa. Michezo mingi Huwa inafanyika nje ya Nchi na hakuna picha tunazoziona na Wala hakuna Hana ya kuumiza kichwa hapa uncle Chama cha wapigapicha kinaweza Kukosa pesa Za kupeleka Mpiga picha nje lakini wizara husika yenye dhamana na Michezo Ina kazi gani? Manake Wakati Waziri Wa Habari anawakilisha hotuba yake ya bajeti alisema Kuwa kazi kubwa ya idara ya Habari Ni
    Kutunza kumbukumbu Za serikali ikiwa Ni pamoja na picha Za matukio mbalimbalimbali. Je Inamaana idara Hiyo yenyedhamana ya kufanya kazi Kama Hizo haina bajeti ya kupeleka wapiti picha na waandishi wake katika matukio yankinataifa Kama haya? Siku njema uncle. Hayo ni maoni yangu machache Ingawa Nina mengi sana kichwani

    ReplyDelete
  3. Ankal, pamoja na kusema hujaandaa mada leo lakini hakika ulichotoa ni mada kubwa na umetumia 'contemporary on-going major event' kueleweka na kuingia kwenye mitima pia ya sote wapenda picha, wapiga picha, wakutubi, wanahistoria, viongozi, wasomaji, wamiliki wa vyombo vya habari, wasomaji, wafanya biashara ya vielelezo, nk, nk. Umesema jambo KUBWA kweli.
    Ankal, mada yako pita imeweka mwanzo mzuri wa sisi viongozi wa serikali kusutana. K.m. mimi nimekuwa natafuta CD ya wimbo wa Taifa, walau basi hata a digital copy, deposited at some site in the web, lakini mekuwa haiwezekani kabisa. Nimejaribu hata kuwasiliana na ninaoamini wanatakiwa kuwa na kitu kama hicho, nao hata hawajali mbali ya kuwa nilidhani wangeiona pia kama ni fursa ya biashara!
    Nisitoke kwenye mada, Ankal. Umeweka changamoto mbele yetu wengi, jambo ambalo naamini sasa Mwambene (MAELEZO) atalielewa kwa urahisi na kulifanyia kazi.
    By the way, Ankal na wanahabari wenzako naomba niwaseme kidogo. Ukosefu wa umakini wa kuweka kumbu kumbu ya matukio, na labda uzembe tu wa baadhi yenu wanahabari wa picha, umeleta mifadhaiko mara kadhaa, silo tu kwa kutokuwa na picha husika, Sara nyingine hata kwa kutojali kelewa usahihi wa baadhi'contents' za picha yenyewe. Utakuta picha ni ya Nisitoke 'Rashid' lakini jina ni la 'Ramadhan', n.k. Hii siyo tu huwa inakuwa nilidhani'misinformation au hata disinformation' bali pia fedheha kwa wanaoguswa moja kwa moja na makosa kama hayo.
    Well, nadhani nimechangia vya kutosha. Nasubiri kutokuwa kwa wadau wengine.

    Mdau. ....... Ughaibuni.

    ReplyDelete
  4. Haah!: Hivi kumbe hatuna wapiga picha huko.Kama alivyosema mdau hapo juu,hii teknolojia itatupeleka kubaya...kumbukumbu muhimu,ndiyo maana mm nikinunua gazeti la Daily news lazima niende kule kwenye picha za zamani wanaita sijui Back Memory Lane?Picha za miaka 1960s,1970s huwa zinanisisimua sana.Wakati mwingine naona jiji letu la Dar enzi hizo,burudani tosha.

    David V

    ReplyDelete
  5. Ankal Hiki ni Kiama cha Taifa letu zaidi ya kuwa janga kwa uzito wake kwa sasa!

    Inasikitisha sana hata kwa kiwango cha kuwa na Rekodi kwa picha inashindikana, zaidi ya hapo unakuta hata Rekodi ya kwenye Vitabu hakuna!

    Iliwahi kutokea Wanaridha wawili Mashuhuri waliowahi kupeperusha VEMA Bendera ya Tanzania miaka ya nyuma ktk Mchezo wa Riadha Kimataifa Mwinga Mwanjala ambaye anaishi Milwaukee, Winsconsin-Marekani na Mosi Ali ambaye anaishi Oslo-Norway walifika nyumbani Bongo wakaenda hadi Ofisi za RT (Chama cha Riadha Tanzania) kuchukua ushahidi (CV) kujitetea huko walipo ktk shughuli za maendeleo ya Riadha,,,cha kustaajabisha hata ile REKODI ANGALAU KWA PICHA HAIKUPATIKANA!

    ReplyDelete
  6. Ni kweli ankal,

    Pamoja na faida ulizozitaja, upigaji na utunzaji picha zetu sisi wenyewe itatusaidia kuamua hadithi gani tunataka kuisimulia kwa dunia nzima. Itatusaidia kuondokana na ulalamishi na lawama kwamba vyombo vya habari vya nje vinaandika na kuonyesha mabaya tu ya Tanzania.

    Ignorant,

    EU

    ReplyDelete
  7. Aggrey UrioAugust 05, 2012

    Nakupa mia kwa mia kukumbusha jambo hili la kumbukumbu; sio lazima sana kuambatana na mpiga picha toka nyumbani kama uwezo haotoshi ila kwa maoni yangu ni kwamba siku hizi kuna vijana wengi na jumuia za kitanzania walio nchi za nje. Kwa mfano hapa Uingereza kuna jumuia ya Watanzania waishio Uingereza inaitwa TA (TANZANIA ASSOCIATION UK)Jumuia hii iko karibu sana na Ubalozi wetu hapa Uk; waandaji wa michezo hii wangeweza kuwasiliana na Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza nina uhakika tungeweza kupata picha kwa gharama nafuu sana bila kutumia nguvu au kuomba msaada wa wadhamini. Ankali tafadhali nawakilisha.

    ReplyDelete
  8. Kwa sisi tulokuwa karibu na wanamichezo walipofika tumegundua ya kuwa:wakati wanamichezo hawa walipotakiwa wafike London kwa Balozi,
    1) Kwa ushahidi kabisa Walipodai hela za nauli kutoka Bradford Ubalozi ulisikitika kuwa ni nyingi walipoambiwa wakati nauli ya Coach ni at least 40.-50 hasa kwa wakati huu inafika hadi 70- Safari ni ya MASAA 5 na nusu.licha ya kuwepo ma coach kwa pound 3. lakini hayo utafika kesho kutwa.

    2.) kulikuwa na malalamiko mengi ya chakula kwa wana riadha hao ukizingatia wao ni wana michezo walitakiwa wawe na lishe bora.

    Swali linakuja JE Wataweza kumlipa mpiga picha hata huyo wa huku huku awe Mtanzania ina maana alipwe vile vile kila one hour 7-8 Pound kiwango cha chini cha mshahara lakini professional ni kuanzia 10.-14.5 an hour je wangeliweza hivo? kutokana mtu afuatane nao hatujali uzalendo tu inamaana anawacha muda wake wa kufanya kazi na maisha ya UK kama hufanyi kazi basi huwezi kuishi labda uwe umejiripua.
    Ahsante Mdau UK

    ReplyDelete
  9. Hapa kuna kiongozi wa Msafara wa Team TZ anaitwa Jarufu.Jamaa nuksi sana.Kaja na wana riadha kawaficha kijiji kiitwacho bradford bila kuwasilian na ubalozi.Jama kawaficha wanariadha kutoka tanzania kama wafungwa.Mtu ukitembelea olyimpic stadium una kutana na wana riadha tofauti kasoro Tanzania . Hivyo hawa jama bado wako hapa uk na wana fanya nini?Nilisikia eti moja wao sijui bondia kapoigwa ndio basi tena .Maskini Tanzania watu wana ilampa hivi hivi.Mjanja moja jarufu ana wakosesha furaha na ukumbusho watu million 40 huko nyumbani.Ili kuaje hata shirika la olympic TZ washindwe hata kuja na muandishi hata mmoja?This is a big scandal.These are the rules:All Olympic press accreditations (including those granted to websites) are distributed by National Olympic Committees (NOCs) and National Paralympic Committees (NPCs) in each country.Mr Jarufu and co had the capacity to organise that

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...