Na Mwandishi Maalum, New York
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, jana alhamisi amezindua rasmi mwongo wa Nishati Endelevu kwa wote (SE4ALL) wakati wa mkutano unaohudhuriwa na wajumbe zaidi wa 1,000 wakiwamo zaidi ya mawaziri 20 wa Nishati 20 wafanyabishara, mashirika ya kimataifa yakiwamo ya fedha na Asasi zisizokuwa za kiserikali.
Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano huu ulioanza Juni 4 na utamalizika Juni 6, unaongozwa na Waziri wa Nishati na Madini Professor Sospeter Muhongo ( Mb) ambaye pamoja na kuhudhuria na kuchangia mijadala mbalimbali leo Ijumaa June 6, atazungumza katika mkutano wa mawaziri kuhusu nafasi ya Nishati katika Ajenda za Maendeleo Endelevu baada ya 2015.
Akizindua mwongo huo Ban ki Moon, pamoja na mambo mengine alieleza kuwa licha ya kuwa pamoja suala la Nishati ni suala la kidunia, lakini katika maeneo mengi ni suala linalomhusu mwanamke zaidi.
“ Ni suala linalomhusu mwanamke zaidi, linaweza kumaanisha tofauti kati ya usalama na hofu, uhuru na utumwa , hata uhai na kifo. Dunia lazima ije pamoja kumaliza umaskini wa nishati na kuhakikisha watu maskini wanaweza kuhimili maisha yao na kustawi kiuchumi” akasema Katibu Mkuu.
Akaongeza kuwa mpango wa nishati endelevu kwa wote zimeanza kuzaa matunda na kwamba ahadi za mabilioni ya dola zilizoahidiwa zimetolewa, huku nchi zinazoendelea zaidi ya 80 zimejiunga na mpango huo.
Pamoja na Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa kuzungumza wakati wa uzinduzi wa mwongo huo, wengine waliopata nafasi ya kuzungumza ni pamoja na Rais wa Iceland, Olafur Ragnar Grimsson, Bw. John Ashe,Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Rais wa Banki ya Dunia Jim Yong Kim ( kupitia video) .
Mkutano huu utafanya tathmini ya matokeo ahadi za mabilioni ya dola kuhusu upatiakani wa nishati, ufanisi wake na nishati mbadala zilizoahidiwa wafanyabiashara, wawekezaji na watu wengine walizotoa wakati wa Mkutano wa Maendeleo Endelevu ( Rio+20) uliofanyika mwaka 2012.
Aidha unatarajiwa kuhamasisha upatikanaji wa raslimali fedha, uwezeshaji na mipango ya kufikia malengo ya nishati endelevu kwa wote.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mwongo wa Nishati Endelevu kwa Wote (2014-2024), uzinduzi huo umefanyika wakati wa Mkutano wa Kwanza wa Mwaka kuhusu Nishati Endelevu kwa Wote ( SE4ALL)unaoendelea hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa na kuhudhuriwa na wajumbe zaidi ya 1000. Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Profesa Sospeter Muhongo ( Mb) anaongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano huu.
Wajumbe wanaohudhuria Mkutano wa Nishati Endelevu kwa Wote wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Bw. John Ashe mara baada ya uzinduzi wa Mwongo wa Nishati kwa wote. Mhe. Waziri Muhongo anaonekana nyuma ya Katibu Mkuu
Mhe. Waziri wa Nishati na Madini Profesa Muhongo akiwa na Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi muda mfupi kabla ya uzinduzi wa Mwongo wa Nishati Endelevu kwa Wote. Walioketi nyuma ni wasaizidi wa Waziri.
Sehemu wa washiriki wa mkutano wa Nishati Endelevu kwa wote wakifuatilia uzinduzi wa Mwongo wa Nishati kwa wote .
Nishati kwa wote ni ujumbe muafaka kwetu sisi watanzania.
ReplyDeleteTuwe na mkakati wa kusitisha kuchora kuchoma makaa na kukata miti. Ama sivyo ni shati ya wa kubwa tu. Hii gesi twaisikia tu iko wapi?
ReplyDelete