Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Ian Ferrao akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari alipokuwa akitangaza mikakati ya kampuni hiyo kuipeleka Tanzania katika ulimwengu wa teknolojia na itakavyotumia kubadilisha maisha ya watanzania na kuwa bora zaidi.Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam.
 Baadhi ya waandishi wa habari na wafanyakazi wa Vodacom Tanzania, wakiwa katika mkutano wa waandishi wa habari na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Ian Ferrao (hayupo pichani)alipokuwa akitangaza mikakati ya kampuni hiyo kuipeleka Tanzania katika ulimwengu wa teknolojia na itakavyotumia kubadilisha maisha ya watanzania na kuwa bora zaidi.Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam.
(Picha na Mpigapicha Wetu).


  • Yawekeza zaidi ya Dola bilioni 1 nchini
  •  Mtandao wake wa 2G na 3G umewafikia wananchi kwa 87%
  • Inao mtandao wa mawakala zaidi ya 85,000 wa M-Pesa nchini kote.
  • Biashara zaidi ya 10,000 nchini kote wanatumia huduma ya Lipa kwa M-Pesa
  • Ni kinara wa kulipa  na kukusanya kodi za serikali katika sekta ya mawasiliano


KAMPUNI ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania ambayo inaongoza kwa kuwa na mtandao mkubwa nchini na mtandao wenye kasi zaidi wa 3G leo imetangaza mikakati yake ya kuipeleka Tanzania katika ulimwengu wa teknolojia na itakavyotumia teknolojia kubadilisha maisha ya watanzania kuzidi  kuwa bora.

Akitangaza mkakati huo kwa waandishi wa habari leo katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Ian Ferrao, alieleza mikakati hiyo mbalimbali “Tunafurahi kuona mchango wa Vodacom katika kuleta maendeleo nchini na kubalisha maisha ya watanzania kuwa bora, Hivi sasa tumejizatiti kuboresha huduma za mawasiliano nchini na pia tutaendelea kubuni huduma mbalimbali za kutumia teknolojia ya simu kurahisisha maisha ya wananchi.

Tutaendelea kuboresha na kusambaza huduma zetu za internet nchi nzima na kutoa huduma za kifedha na malipo kwa kutumia teknolojia,kuuganisha biashara mbalimbali kwa kutumia teknolojia tukiwa tunaenda sambamba na mkakati wa  serikali wa kuleta mapinduzi ya matumizi ya teknolojia katika kupata huduma mbalimbai nchini”

Mpaka sasa Vodacom imewekeza kiasi cha  zaidi ya Dola bilioni 1 za kimarekani nchini Tanzania,imejenga mtandao wa kutoa huduma za internet ya 2G na 3G na mtandao wake unawafikia asilimia 87 ya watanzania nchini kote.Ikiwa inajivunia kufanya kazi na mtandao mkubwa wa mawakala wake zaidi ya 85,000 wa kutoa huduma ya kifedha ya M-Pesa. Vodacom inayo wateja zaidi ya milioni 12 na pia ni kinara wa kukusanya na kulipa kodi za serikali katika sekta ya mawasiliano nchini.

Ferrao alisema licha ya changamoto mbalimbali zilizopo katika uwekezaji  kwenye sekta ya mawasiliano nchini kama vile kodi kubwa na ushindani katika bei za kutoa huduma, Vodacom itaendelea kuwekeza na kubuni huduma za kuleta ushindani kwenye mapinduzi ya matumizi ya teknolojia nchini.

Kuhusiana na ushindani wa bei za kutoa huduma Ferrao alisema  “Ushindani huu wa makampuni katika bei za kutoa huduma unawanufaisha wateja kwa muda mfupi,kinachotakiwa ni kuendelea kufanya uwekezaji endelevu kama vile kusambaza zaidi huduma ili ziweze kuwafikia wananchi wengi hususani wa maeneo ya vijijini.

Tukiwa ni moja ya nchi inayotoza viwango vya juu vya kodi katika seka ya mawasiliano duniani tunachopaswa kufanya ni kutumia huduma hizi kuleta mapinduzi yatakayoleta mabadiliko kwa wananchi kuwa bora na kujenga uchumi imara na wenye ushindani”Alisema

 Katika kufanikisha  mchango wa sekta ya mawasiliano kuleta mapinduzi nchini alisema kuna mambo yanapaswa kuangaliwa “Tumekuwa tukishuhudia  ongezeko la kodi hususani kodi ya zuio, katika sekta ya mawasiliano ambapo kodi zinazotozwa hapa nchini ni kubwa katika nchi zote za Afrika Mashariki na nchi za SADC.

Utafiti wa Taasisi ya Deloitte Consulting  katika mkutano wa makampuni ya mawasiliano uliofanyika jijini Dar salaam mapema mwaka huu inaonyesha kuwa sekta ya mawasiliano inachangia asilimia 3.8%  ya pato la Taifa na asilimia 11 ya mapato ya serikali kupitia kodi na  kodi hizo zinaongeza gharama za uendeshaji  kwa kampuni ambapo mzigo wote humwangukia mtumiaji kutokana na gharama za huduma kupanda.

Kwa mfano serikali ikipunguza kodi ya zuio katika huduma ya muda wa maongezi kutoka asilimia 17 mpaka asilimia 10 itawezesha wateja wapya 1.7 millioni kujiunga na huduma za simu na kwa kufanya hivyo zitawanufaisha katika shughuli zao mbalimbali za uzalishaji na kutakuwepo ongezeko la mapato linalofikia Dola 0.5 bilioni katika pato la taifa hadi kufikia mwaka 2020”.

Kuhusiana na suala la masafa yaliopo kwa makampuni ya simu  nchini alisema leseni zake zimetolewa kwa makampuni zaidi ya 14  ambayo mengi yao yanashikilia masafa  bila kuyatumia lakini leo hii wateja zaidi ya asilimia 99 wanahudumiwa na makampuni yenye masafa ya mawimbi ya mtandao  ya asilimia 53 ambapo makampuni yanayotoa huduma za mawasiliano hivi sasa hayapati masafa ya kutosheleza mahitaji ya kusambaza huduma zake kwa ufasaha.

 Ferrao alisema wakati umefika kwa masafa ya makampuni kuongezwa hadi kufikia 700Mhz kuwezesha makampuni kuwekeza kwa kutumia teknolojia za kisasa zaidi na zenye gharama nafuu ambazo zinaweza kuwezesha kuzinduliwa interneti mpaka ya 4G nchini.

Alisema pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo Vodacom imewekeza zaidi shilingi Bilioni 180 kwa muda wa miezi sita iliyopita  katika kuboresha mtandao wake wa internet na imejipanga kuboresha huduma zake mbalimbali.

Ferrao aliongeza “Wakati Vodacom inajizatiti kuboresha huduma zake taasisi yake ya kuboresha huduma za jamii ya Vodacom Foundation imejikita kuendelea kutoa misaada mbalimbali kwa jamii hususani kwa ajili ya kuendeleza akina mama na makundi mbalimbali yenye mahitaji.

Mwaka huu imewezesha operesheni kwa ajili ya wanawake 2,274 walioathirika na fistula , na kuwezesha wasichana 7,077 kubaki shuleni kupitia mradi wa Hakuna Wasichoweza na imewezesha zaidi ya wanafunzi 6,000 kusoma elimu ya kompyuta kwa vitendo mashuleni.Vodacom Foundation imekwishatumia shilingi bilioni 12 kusaidia jamii tangu ianzishwe mwaka 2006 na itaongeza zaidi kiasi hicho cha fedha kusaidia miradi mbalimbali katika mwaka wake wa fedha ujao”

Alimalizia kwa kusema “Hatutaacha kubuni na kutoa huduma bora lengo kubwa likiwa ni kuhakikisha watanzania wote wameunganishwa na huduma ya mtandao wa intaneti”

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...