WIZARI ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo imeandikia barua klabu ya Yanga kuiagiza iwe imekwishafanya uchaguzi wake hadi kufika Aprili 15, mwaka huu. Yanga imekwishapokea barua hiyo kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) wakisistizwa hilo ni agizo la Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye.

Pamoja na kwamba wapo kwenye maandalizi ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kesho dhidi ya Al Ahly, lakini tayari Yanga wameanza kulifanyia kazi agizo la Serikali na wakati wowote wanaweza kutangaza uchaguzi.

Lakini kuna wasiwasi kama uchaguzi unaweza kuwa umefanyika hadi Aprili 15, kwa sababu muda waliopewa ni mfupi mno kukamilisha taratibu.

Yanga inapaswa kuutangaza japo kwa wiki moja uchaguzi, kugawa fomu kwa wagombea japo kwa wiki moja pia, na baada ya hapo ipatikane angalau wiki moja nyingine kwa ajili ya usaili, mapingamizi kabla ya kupiga kura kuchagua viongozi.

Yanga kwa sasa ipo chini ya uongozi ambao umekwishamaliza muda wake, chini ya Mwenyekiti Yussuf Manji na Makamu, Clement Sanga. Manji na Sanga waliingia madarakani Julai 15, mwaka 2012 katika uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi za viongozi waliojiuzulu akiwemo Mwenyekiti Wakili Lloyd Nchunga na Makamu wake, Davis Mosha.

Walichaguliwa pamoja na Wajumbe Abdallah Bin Kleb, Moses Katabaro, Aaron Nyanda na Geroge Manyama ambao waliungana na Wajumbe waliobaki, akiwemo Salum Rupia na Mohammed Binda. Hata hivyo, baada ya uongozi huo kumaliza muda wake mwaka 2014, Manji akaunda Kamati ya Muda, yeye na Sanga wakiendelea na nyadhifa zao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...