Katika kutambua kujitolea kwa Tanzania kutoa askari wake kwenda kulinda amani katika nchi zingine, Umoja wa Mataifa (UN) umesema unatambua huduma inayotolewa na Tanzania ikiwa kama mwanachama wa UN na unafurahishwa na hatua iliyopo ya kuendelea kusaidia kulinda amani katika operesheni zinazofuatia.

Hayo yamesemwa na Mwakilishi Msaidizi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Amon Manyama katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa ambapo kwa nchini siku hiyo iliadhimishwa Dar es Salaam katika Uwanja wa Mashujaa wa Mnazi Mmoja

Manyama alisema Tanzania imekuwa ikijitolea kusaidia ulinzi wa amani katika mataifa mengine licha ya kupoteza baadhi ya wanajeshi wake lakini bado wamekuwa wakiendelea kujitolea kusaidia kuimarisha ulinzi wa mataifa mengine ambayo hali ya usalama inakuwa siyo ya uhakika.

“Tumefurahishwa na historia ya Tanzania ya kuzisaidia nchi jirani kulinda amani na kutatua migogoro ya hapo zamani na kuziwezesha kujipatia uhuru,” alisema Manyama.

Aidha Manyama alisema Umoja wa Mataifa umekuwa ukijitahidi kuendelea kushirikiana na wanachama wake ili kwezesha upatikanaji wa amani kwa mataifa yote na itaendelea kutoa heshima yake kwa wanawake na wanaume ambao walipoteza maisha wakiwa kazini kulinda amani ya mataifa mengine.

“Mwaka jana idadi ya waliokufa ilikuwa 129, walinda amani hawa walitoka katika nchi 50, wakiwa ni pamoja na wanajeshi, polisi, watumishi kutoka mataifa mbalimbali, wafanyakazi wa kujitolea wa Umoja wa Mataifa na watumishi wa ndani,

“Tunapenda kutoa heshima kwa mashujaa wetu zaidi wanaume na wanawake milioni moja waliotumikia chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa kwa majivuno, weledi tangu kuanza kwa kazi hiyo 1948,” alisema Manyama.

Nae mgeni rasmi katika siku hiyo, Meja Jenerali James Mwakibolwa aliupongeza Umoja wa Mataifa kwa jinsi wanavyofanya kazi na kusaidia kuokoa maisha ya watu wengi na kuahidi Tanzania itaendelea kutoa wanajeshi wake ili waendelee kulinda amani.

“Tumeshatoa walinda amani 2,328 katika operesheni mbalimbali zilizopita na tutandelea kufanya kazi pamoja ili kuimarisha amani na utulivu katika maeneo mengine,” alisema Meja Jenerali Mwakibolwa.

Mgeni rasmi Meja Jenerali James Mwakibolwa akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Mashujaa wa Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam 31 Mei, 2016.
Mwakilishi Msaidizi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Amon Manyama akisoma hotuba pamoja na ujumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon kwenye sherehe za maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Mashujaa wa Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam 31 Mei, 2016.
Mgeni rasmi Meja Jenerali James Mwakibolwa akiweka shada la maua kwenye mnara wa mashujaa kuwakumbuka Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa walipoteza maisha wakiwa kazini kulinda amani ya mataifa mengine yenye machafuko wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Mashujaa wa Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam 31 Mei, 2016.
Mkuu wa Jeshi la Akiba wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Meja Jenerali, Elias Athanas akiweka shada la maua kwenye mnara wa mashujaa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Mashujaa wa Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam 31 Mei, 2016.
Mwakilishi Msaidizi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Amon Manyama akiweka shada la maua kwenye mnara wa mashujaa kuwakumbuka Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa waliopoteza maisha katika oparesheni ya kulinda amani katika nchi zenye machafuko wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Mashujaa wa Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam 31 Mei, 2016.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...