Waziri wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage akifafanua jambo alipokuwa akizindua Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.  Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dkt. Egid Mubofu.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage (wa pili kulia) akisisitiza jambo kwa Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mhandisi Tumaini Mtutu (wa pili kushoto) wakati wa uzinduzi wa baraza la wafanyakazi la shirika hilo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.  Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo,Profesa Mekanya Maboko na wa tatu kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dkt. Egid Mubofu.

Serikali imewataka baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) walioshirikiana na wenzao wa Mamlaka ya Mapato (TRA) kupitisha makontena zaidi ya 100 bila kukaguliwa na shirika hilo katika Bandari ya Dar es Salaam kujisalimisha haraka.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw.Charles Mwijage alitoa agizo hilo mwishoni mwa juma wakati akizindua baraza la wafanyakazi wa Shirika hilo.“Nimeanza kukusanya orodha ya majina ya watu waliosaidia kupitisha makontena haya na nikija nayo hawatapona,” alisema.

Aliwataka wote wanaojijua kuhusika kujisalimisha mapema na kutubu ili wasamehewe kabla haya hatua hiyo.Makontena hayo yalipitishwa katika bandari ya Dar es Salaam hivi karibuni bila ya kuthibitishwa na shirika hilo.

Pia aliitaka TRA kuacha kutoa makontena bila ya shirika hilo kuthibitisha au kukagua ubora wa bidhaa zinazoingizwa hapa nchini sababu mwenye mamlaka hiyo ni TBS.

Alisema watakaotubu kuwa walishiriki waseme walishiriki vipi na lini, walishirikiana na nani na wataje sehemu yalikopelekwa makontena hayo ili serikali iweze kusaidia kukomesha hali hiyo.Alisema anaamini kuwa waliofanya hivyo katika mamlaka hiyo walifanya kwa utashi wao bila ya ushiriki wa viongozi wao na kwamba sasa wakati umefika wa kukomesha tabia hiyo.

Alilitaka baraza hilo kushirikiana na menejimenti na kuhakikisha matatizo yanayojitokeza yanapatiwa ufumbuzi kwa maslahi ya nchi na kwamba serikali itahakikisha inaongeza vitendea kazi na watumishi ili kufikia malengo ya shirika.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Egid Mubofu, baraza hilo lina wajumbe 48 wanaotoka katika vitengo mbalimbali na litakaa kwa muda wa miaka mitano.“Baraza hili linaundwa kutokana na mkataba wa menejimenti na Chama cha Wafanyakazi (RAAWU),” alisema Dkt. Mubofu na kuongeza kuwa menejimenti itashirikiana na baraza kufanyakazi za shirika kwa tija.

Alisema wafanyakazi wanatakiwa kufanya kazi kwa weledi na uadilifu katika majukumu yao ya kila siku.Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi (TBS), Prof. Mekanya Maboko alilitaka baraza hilo kufanya kazi kwa kushirikiana na menejimenti na bodi kuhakikisha shughuli za udhibiti wa ubora zinafanyika kwa ufanisi.

“Bodi itaendelea kuisimamia menejimenti na kuishauri ifanye kazi kwa kuzingatia sera na sheria,” alisema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...