Awamu ya Tano ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kutekeleza azma yake ya kukusanya kodi, mapato na gawio kutoka kwa wananchi, wafanyabiashara mbalimbali, wawekezaji na Taasisi na mashirika ya umma ili kuongeza makusanyo ya ndani ya nchi kwa lengo la kuiwezesha Serikali kujiendesha yenyewe na kupunguza misaada na mikopo kutoka nchi wahisani, wabia wa maendeleo na mashirika mbalimbali ya umoja wa mataifa. Taasisi za Serikali na mashirika ya umma yanaendelea kutekeleza agizo la Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutoa gawio kwa Serikali ili kuchangia pato la Taifa.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango amepokea hundi ya shilingi bilioni 1.032 kutoka kwa Benki ya Posta Tanzania ikiwa ni gawio la hisa ya asilimia 86.17 kwa Serikali kama mmoja wa wanahisa kwenye Benki hiyo. Hundi hiyo imekabidhiwa na Prof. Lettice Rutashobya, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Posta Tanzania. Vile vile Prof. Rutashobya amemkabidhi Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Posta Tanzania Dkt. Haruni Ramadhan Kondo hundi ya shilingi milioni 97.8 ikiwa ni gawio la hisa ya asilimia 7.98 kama mmoja wa wanahisa wa Benki hiyo.

Aidha, Mhe. Dkt. Philip Mpango amezitaka Taasisi za Serikali na mashirika ya umma kuilipa Serikali gawio la hisa zake na zijiendeshe kwa ufanisi na kwa faida ili makusanyo hayo yaweze kuwahudumia wananchi.

Katika tukio hilo, Dkt. Kondo ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango iweze kuilipa Shirika la Posta Tanzania shilingi bilioni 3.6 ambazo ni malipo ya pensheni ya wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Shirika limelipa pensheni hizo kwa niaba ya Serikali.

Utaratibu wa Taasisi za Serikali na mashirika ya umma kulipa gawio la hisa kwa Serikali na wanahisa wengine ni maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kuhakikisha kuwa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma yanafanya kazi kwa ufanisi, kuzalisha faida na kutoa gawio kwa Serikali ili mapato hayo yaweze kuhudumia wananchi katika Nyanja mbali mbali kama vile huduma za afya, elimu, maji na barabara.

Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dodoma na kushuhudiwa na Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Dkt. Maria Sasabo, Kaimu Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bwana Deogratius Kwiyukwa.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango akipokea gawio la hisa la shilingi bilioni 1.032 kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Posta Tanzania, Prof. Lettice Rutashobya. Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Eng. Dkt. Maria Sasabo ( wa tatu kushoto) akiwa maeshika hundi hiyo.
Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Dkt. Maria Sasabo (wa pili kushoto) akipokea gawio la hisa shilingi milioni 97.8 ya Shirika la Posta Tanzania kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Posta Tanzania, Prof. Lettice Rutashobya. Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (wanne kulia) akishuhudia tukio hilo pamoja na Kaimu Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Deo Kwiyukwa (wa tano kushoto).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...