Bodi ya Wadhamini wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, imekutana na viongozi wakuu wa Shirikisho katika Ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Sea Scape, Kunduchi, Dar es Salaam.

Bodi hiyo imekutana na uongozi wakuu wa TFF jana Septemba 2, mwaka huu kwa mara ya kwanza tangu ithibitishwe na Mkutano Mkuu wa TFF.Madhumuni ya Bodi hiyo kukutana na viongozi wa TFF – Rais Wallace Karia; Makamu wa Rais, Michael Wambura na Kaimu Katibu Mkuu, Kidao Wilfred ni kufahamiana.

Kwa upande wa Bodi walikuwa Mhe. Mohammed Abdulaziz, Mhe. Balozi Dk. Ramadhani Dau, Mhe. Abdallah Bulembo na Mhe. Stephen Mashishanga. Mjumbe Dk. Joel Bendera hakuhudhuria kwa udhuru.Kadhalika Bodi hiyo kwa mujibu wa katiba ya TFF, walipata nafasi ya kuchagua Mwenyekiti wa Bodi ambako Mhe. Mohammed Abdulaziz alichaguliwa kushika wadhifa huo. Mhe. Abdulaziz alikuwa Mlezi wa timu ya Daraja la Kwanza ya Kariakoo ya Lindi

Kwa niaba ya Wajumbe wa Bodi, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhe. Mohammed Abdulaziz ambaye ni Mbunge wa zamani wa Jimbo la Lindi Mjini, aliupongeza uongozi mpya wa TFF ulioingia madarakani Agosti 12, mwaka huu akisema: “Mmeanza vizuri.”Kadhalika Mwenyekiti ambaye alipata kuwa Mkuu wa Mikoa ya Tabora, Tanga na Iringa kwa nyakati tofauti , aliahidi ushirikiano kwa uongozi wa TFF ambako kwa upande wa TFF, Rais Karia alipokea pongezi hizo na baraka tele za kuanza vema na ushirikiano.

Mhe. Balozi Dk. Dau – alikuwa Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ni mwanafamilia ya mpira wa miguu aliyejitolea hata kwa nguvu zake binafsi kusaka vipaji vya mpira wa miguu kwa vijana.

Mhe. Joel Bendera ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara. Ni Kocha wa zamani wa timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ aliyekuwa na mchango mkubwa kuifikisha kucheza fainali za Kombe la Mataifa Huru ya Afrika (CAN 1980) sasa michuano hiyo inafamika kwa jina la AFCON. Fainali za mwaka 1980 zilifanyika Lagos, Nigeria.

Mhe. Stephen Mashishanga ni Mkuu wa zamani wa Morogoro mwenye historia nzuri ya unafamilia wa mpira wa miguu akitoa mchango mkubwa katika maendeleo tangu alipokuwa kiongozi hadi sasa. Pia alipata kuwa Mlezi wa timu ya Milambo ya Tabora iliyoshiriki Ligi Kuu Bara.

Mhe. Abdallah Bulembo ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyepata kuwa Makamu Mwenyekiti wa kilichokuwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) – kwa sasa ni Shirikisho (TFF).
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Mhe. Mohammed Abdulaziz (wa tatu kulia walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wenzake na viongozi wa TFF mara baada ya chakula cha mchana na wachezaji wa Taifa Starts kwenye Hoteli ya Sea Scape, Kunduchi, Dar es Salaam Septemba 2, 2017. Wengine mstari wa mbele kutoka kushoto ni Ofisi Meneja wa TFF, Bi. Miriam Zayumba, Kaimu Katibu Mkuu, Bw. Kidao Wilfred, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini, Mhe. Abdallah Bulembo; Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini, Mhe. Stephen Mashishanga; Rais wa TFF, Bw. Wallace Karia; Makamu Rais wa TFF, Bw. Michael Wambura na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini, Mhe. Balozi Dk. Ramadhani Dau. Taifa Stars baadaye Jumamosi ilicheza na Botswana katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa na kushinda mabao 2-0. (Picha na TFF).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...