Majadiliano
kati ya Tanzania na timu ya wawakilishi wa kampuni ya Barrick Gold inayomiliki
migodi ya madini hapa nchini yamekamilika na makubaliano kati ya pande hizo
yametiwa saini leo tarehe 19 Oktoba, 2017 mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu, Jijini Dar es Salaam.
Timu
ya Barrick Gold Corporation ilikuwa imeongozwa na Mwenyekiti Mtendaji wa
kampuni hiyo Prof. John Thornton wakati timu iliyowakilisha Serikali ya
Tanzania imeongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba John Aidan
Mwaluko Kabudi.
Miongozi
mwa mambo waliyokubaliana ni kutekeleza mwelekeo mpya wa biashara ya madini
ambapo kutakuwa na mgawanyo sawa wa faida (yaani
Tanzania kupata asilimia 50 na Barrick Gold Corporation kupata asilimia 50 ya
faida) na kuundwa kwa kampuni ya ubia wa usimamizi wa migodi ya madini
iliyopo Tanzania ambayo itakuwa na makao makuu yake Mwanza na ofisi ndogo Dar
es Salaam nchini Tanzania badala ya nchini Uingereza.
Mengine
ni kufunga ofisi za uhasibu na fedha zilizopo Johannesburg Afrika Kusini na
kuhamishia Tanzania na kutekeleza masharti yote ya mabadiliko ya sheria mpya ya
madini na rasilimali za nchi ya mwaka 2017.
Aidha,
Barrick Gold Corporation imekubali kuwepo kwa wawakilishi wa Serikali katika bodi
za migodi yake yote hapa nchini, kazi mbalimbali za kwenye migodi kufanywa na kampuni
za Kitanzania, Migodi kutoa ajira za kudumu kwa wachimbaji, wachimbaji hao kuishi
majumbani kwao badala ya kuishi kwenye makambi ya migodi na mashauri yote ya
kesi mbalimbali kufanywa hapa nchini.
Kampuni
ya Barrick Gold pia imekubali kutoa Dola za Kimarekani Milioni 300 sawa na
takribani Shilingi Bilioni 700 kama malipo ya kuonesha nia njema ya kufidia
fedha zilizotokana na upotevu wa mapato kupitia biashara ya kampuni hiyo.
Akizungumza
baada ya kutia saini makubaliano hayo Prof. Thornton amempongeza Mhe. Rais
Magufuli kwa msimamo wake unaojenga misingi ya biashara ya kuaminiana na uwazi,
ambayo ni muhimu na ya namna yake kwa biashara katika karne hii ya 21.
Prof.
Thornton amesema Barrick Gold Corporation watazingatia makubaliano haya na
wanaamini kuwa yamefungua ukurasa muhimu utakaowezesha kufanya biashara kisasa.
Kwa
upande wake Mhe. Rais Magufuli amezipongeza timu zote mbili yaani Tanzania na
Barrick Gold Corporation kwa kazi kubwa ziliyofanya kufikia makubaliano hayo na
kwa kipekee amempongeza Prof. Thornton kwa nia yake thabiti ya kukubali
kufanyika kwa mazungumzo na kukubali mambo yaliyofikiwa.
Mhe.
Rais Magufuli amesema makubaliano hayo yataisaidia nchi kuzalishaji ajira
zaidi, kupata manufaa mbalimbali yanayostahili ikiwemo fedha za kugharamia
huduma za kijamii kwa wananchi na yanajenga msingi imara ambao utaiwezesha
Tanzania kunufaika na rasilimali zake za madini.
Mhe.
Dkt. Magufuli amemuagiza Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Kabudi kuunda timu
zitakazoshughulikia biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi pamoja na migodi
mingine ya dhahabu haraka iwezekanavyo ili nchi iweze kunufaika ipasavyo.
“Nataka
machimbo yote ya dhahabu mchakato kama huu ufanyike, pia nakuagiza Prof. Kabudi
biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi nako ni lazima kufuate utaratibu huu,
asiyetaka aondoke” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Pia
Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi hizi badala ya
baadhi yao kuzibeza kwa kuwa zina manufaa kwa taifa na wananchi wake.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar
es Salaam
19
Oktoba, 2017
Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation Profesa John L. Thornton akiwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam Jumanne jioni tayari kushiriki katika mazungumzo ya mwisho na hatimaye makubaliano baina ya Kamati ya serikali na timu ya wataalamu wa kampuni hiyo kuhusiana na makinikia pamoja na biashara ya madini kwa ujumla.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimlaki Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Barrick Gold Corp.Profesa John L. Thornton alipokutana nae wakati wa kupokea ripoti ya makubaliano baina ya Kamati ya Serikali na timu ya wataalamu wa Barrick Gold kuhusu bishara ya madini Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 19, 2017
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Barrick Gold Corp.Profesa John L. Thornton alipokutana nae wakati wa kupokea ripoti ya makubaliano baina ya Kamati ya Serikali na timu ya wataalamu wa Barrick Gold kuhusu bishara ya madini Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 19, 2017
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akishuhudia Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Barrick Gold Corp. Profesa John L. Thornton akiwa na Afisa Uendeshaji wa Barrick Gold Richardc William huku Waziri wa Sheria na Katiba Profesa Palamagamba Kabudi na Florens Luoga nao pia wakiweka saini ripoti ya makubaliano baina ya Kamati ya Serikali na timu ya wataalamu wa Barrick Gold kuhusu bishara ya madini Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 19, 2017
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akishuhudia Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Barrick Gold Corp. Profesa John L. Thornton akiwa na Afisa Uendeshaji wa Barrick Gold Richardc William huku Waziri wa Sheria na Katiba Profesa Palamagamba Kabudi na Profesa Florens Luoga nao pia wakiweka saini ripoti ya makubaliano baina ya Kamati ya Serikali na timu ya wataalamu wa Barrick Gold kuhusu bishara ya madini Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 19, 2017
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...