Wadau wa madini wametakiwa kuhakikisha sekta hiyo inaakisi maendeleo ya jamii inayozunguka eneo hilo ili waone faida ya kuwepo kwa rasilimali hiyo muhimu. 

Mkuu wa Mkoa wa Geita Robert Luhumbi aliyasema hayo mjini Geita kwenye ufunguzi wa majadiliano ya wachimbaji wadogo Tanzania yaliyowashirikisha wadau wa madini wa nchi mbalimbali duniani. 

Akizungumza kabla ya washiriki hao hawajaanza safari ya kutembelea migodi ya madini ya dhahabu, Luhumbi alisema faida ya uwepo wa madini hayo inapaswa kuonekana dhahiri kwa jamii. Alisema uwepo wa rasilimali ya madini ya dhahabu mkoani Geita bado haujaonekana ipasavyo kwa jamii ya eneo hilo kwani zinapaswa kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara, maji, elimu, afya na mengineyo. 

"Hatutaki kuona rasilimali ya madini inaoneka kuwa ni laana kwa jamii badala ya baraka, kwani kupitia tunu hiyo wananchi wanapaswa kunufaika kwa kuona maendeleo yanafanywa kwenye maeneo hayo," alisema Luhumbi. Alisema sekta ya wachimbaji wadogo wa madini inafanywa na idadi ya watu milioni moja hadi milioni moja na nusu nchini hivyo wanapaswa kuwekewa mazingira rafiki yatakayoboeesha maisha yao. 

Mkurugenzi wa asasi ya Haki Madini, Amani Mhinda alisema wameandaa mdahalo huo kwa uwezeshwaji wa taasisi ya kimataifa ya mazingira na maendeleo  (IIED) kituo cha kimataifa cha utafiti wa misitu (CIFOR) na kampuni ya ushauri ya MTL. Mhinda alisema lengo ni kutoa suluhu juu ya changamoto zinazomkumba mchimbaji mdogo nchini na kupendekeza majawabu. Alisema sekta ya uchimbaji madini nchini ni kati ya sekta zinazokua kwa kasi kubwa na yenye mchango mkubwa wa uchumi wa Taifa. 

Alisema ingawa mipango mahususi ya kisera juu ya uchimbaji mdogo imeanzishwa, bado kuna changamoto nyingi hasa katika uelewa, ujasiri, mipango, fedha na taratibu zinazokwamisha utekelezaji wa sera na maboresho. Mchimbaji wa madini wa kampuni ya Nsangano Gold mine, Renatus Nsangano alisema bado wachimbaji wadogo wana changamoto ya kufanya kazi bila kufanya utafiti. Nsangano alisema endapo wangekuwa wanafanya utafiti na kubaini madini yalipo ingekuwa na tija kubwa kwa wachimbaji wengi. 

Hata hivyo, alisema wamesaidia jamii zinazowazunguka kwenye maendeleo mbalimbali ikiwemo ya sekta ya elimu, afya na maji. 
 Mkuu wa Mkoa wa Geita Robert Luhumbi akizungumza na wadau wa madini juu ya rasilimali hiyo kunufaisha jamii inayozunguka eneo hilo. 
 Mkurugenzi wa kampuni ya Nsangano Gold mine ya Nyarugusu Mkoani Geita Renatus Nsangano (kulia) na Mkurugenzi wa kampuni ya Kadeo, Christopher Kadeo (wa pili kulia) wakiwa na wadau wa madini waliotembelea migodi yao ya dhahabu. 
 Mdau wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Joseph Lyimo akivuta udongo kwa kutumia nyenzo katika mgodi wa dhahabu kwenye machimbo ya wachimbaji wadogo wa Nyarugusu Mkoani Geita. 
Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu wa mgodi wa Nsangano Gold mine ya Nyarugusu Mkoani Geita, wakiendelea na shughuli za uchenjuaji wa dhahabu kwenye moja kati ya migodi yao. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...