Na Brighton James
Vilabu vya mpira hapa nchini vimeshauriwa kupima afya za  wachezaji wao kabla ya kuanza kwa mashindano ili kama watakutwa na matatizo waweze kupata matibabu mapema.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati akiongea na wachezaji wa Klabu ya Simba waliofika katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo.
Prof. Janabi alisema faida ya kufanya uchunguzi wa afya kutamsaidia  mchezaji kama atagundulika kuwa na matatizo ya moyo atapata matibabu mapema na kuepukana na kifo cha ghafla anachoweza kukipata awapo uwanjani.
“Vifo vya wachezaji vinavyotokea ghafla wanapokuwa uwanjani vinaweza kuzuilika iwapi wangefanya uchunguzi wa afya zao mapema. Nazishauri timu zinazocheza ligi kuu pamoja na mashindano ya kitaifa na kimataifa wajitahidi kupima afya za wachezaji wao ikiwemo uchunguzi wa magonjwa ya moyo”, alisisitiza Prof. Janabi.
Kwa upande wake Abasi Ally ambaye ni Mkuu wa msafara kutoka klabu ya Simba alisema wameamua kuwafanyia wachezaji wao uchunguzi wa magonjwa ya moyo  kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi kuu ya Tanzania inayotarajia kuanza mwishoni mwa mwezi ujao.
Ally alisema kwamba kuwapima afya wachezaji hao kutawasaidia kujuwa afya zao ili kama mchezaji atakutwa na matatizo aweze kupata matibabu mapema na kushiriki mashindano akiwa na afya njema.
Jumla ya wachezaji 27 wa klabu hiyo wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa kuangaliwa jinsi mioyo yao inavyofanya kazi (ECHO), umeme wa  moyo (ECG) na  umeme wa moyo wakati mtu anafanya mazoezi (Stress ECG)
 Mfanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Abuu Dalidali akimpima urefu Mchezaji  wa Klabu ya Simba Yussuf Mlipili wakati wachezaji wa timu hiyo walipofika katika Taasisi hiyo leo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo. 

 Muhudumu wa Afya wa  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Seleman Charles akimpima urefu Shiza Ramadhani Kichuya ambaye ni Mchezaji  wa Klabu ya Simba wakati wachezaji wa timu hiyo walipofika katika Taasisi hiyo leo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akisimamia  upimaji wa magonjwa ya moyo ulivyokuwa unafanyanyika kwa wachezaji wa klabu ya Simba wakati wachezaji wa timu hiyo walipofika katika Taasisi hiyo leo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.
Picha na JKCI

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...