MKUU wa mkoa wa Iringa Bw. Ally Hapi ameahidi kushirikiana kikamilifu na wakuu wenzake wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kutangaza fursa na vivutio vya kiutalii vinavyopatikana katika ukanda huo, ikiwa ni mwendelezo wa harakati za kuunga mkono adhma ya Rais John Pombe Magufuli ya kufungua na kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.

Katika kuthibitisha hilo kwa vitendo, Bw Hapi ameahidi kuunga mkono jitihada zilizoanzishwa na mtangulizi wake aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Bi. Amina Masenza za kuyaboresha zaidi Maonesho ya Utalii Karibu Kusini 2018 yanayoenda sambamba na Maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani ambayo Kitaifa yatafanyika mkoani Iringa Septemba 26 hadi 30 mwaka huu.

Bw Hapi ametaja mkakati wake huo, mapema wiki hii jijini Dar es Salaam alipotembelea Ofisi za Kampuni ya Capital Plus International (CPI) inayoshirikiana na ofisi ya Mkuu wa Iringa pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii kuratibu maonesho hayo yanayofanyika mjini Iringa kwa mwaka wa tatu mfululizo.

“Tungependa watu kutoka maeneo mengine ya Tanzania na hata nje ya nchi waje katika maonesho hayo ili waone na kutembelea vivutio vya utalii, kihistoria na kufahamu fursa za uwekezaji tulizo nazo”, alisisitiza kiongozi huyo wa Iringa.

‘’Mikoa ya nyanda za juu Kusini inasifika kuwa na hifadhi zenye sifa za kipekee ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha yenye makundi makubwa ya tembo na wanyama wengine. Aidha, hifadhi ya Kitulo yenye aina mbali mbali za maua ambayo hayapatikani mahali pengine Duniani na Udzungwa yenye wanyama na viumbe adimu duniani kama vyura wa Kihansi,’’ alitaja

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bw. Ally Hapi (katikati) akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya Capital Plus Internantional kuhusiana na maandalizi ya Maonesho ya Utalii Karibu Kusini 2018 alipotembelea ofisi za kampuni hiyo jijini Dar es Salaam leo. Kampuni ya Capital Plus International inashirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kuandaa maonesho hayo yanayotarajiwa kufanyika Septemba 26 hadi 30 mwaka huu kwenye Viwanja vya Kihesa Kilolo mkoani Iringa yakihusisha mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini. 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bw. Ally Hapi (kulia)akipokea zawadi ya kikombe maalumu chenye nembo ya Capital Plus Internantional kutoka kwa mfanyakazi wa kampuni hiyo Bi Farida Adam ikiwa ni ishara ya kumkaribisha kwenye ofisi hizo. Capital Plus Internantional inashirikiana na Ofisi ya Mkoa wa Iringa kuandaa maonesho ya Utalii Karibu Kusini 2018. 

Mratibu wa Maonesho ya Utalii Karibu Kusini 2018 kutoka kampuni ya Capital Plus Internantional Bw Clement Mshana akifafanua jambo kwa Mkuu  wa Mkoa wa Iringa Bw. Ally Hapi kuhusu maandalizi ya Maonesho hayo wakati wa kikao hicho.
Mratibu Msaidizi wa Maonesho ya Utalii Karibu Kusini 2018 kutoka kampuni ya Capital Plus Internantional Bw Malela Kassim (katikati) akifafanua jambo kuhusu maandalizi ya Maonesho hayo kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bw. Ally Hapi (hayupo pichani)wakati wa kikao hicho.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...