Na Fatma Abdallah, Maelezo - Zanzibar 

Wakulima wa Mpunga wa kilimo cha majaribio cha Shadidi wameongeza uzalishaji kutoka tani 4.3 msimu wa vuli kufikia tani 13.5 msimu wa mwaka baada ya kupatiwa mafunzo ya kilimo hicho.

Akizungumza na Mwandishi wa Habari Ofisini kwake Darajani, Afisa elimu kwa wakulima wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Sada Seif Said alisema Wakulima wa kilimo hicho wa Kisiwa cha Unguja walivuna tani 7.3 za mpunga na Pemba tani 6.2. Aliyataja mabonde yanayolima kilimo cha Shadidi kwa Unguja kuwa ni Uzini, Cheju, Bumbwisudi na Kibokwa na Pemba ni Makombeni, Weni, Kibirinzi na Kinyapunzi.

Alisema baada ya wakulima wa kilimo cha Shadidi kuongeza uzalishaji wataendelea kuhamasisha wakulima wengine wanaolima mpunga wa umwagiliaji maji ili waweze kujiunga na kilimo hicho.

Afisa Elimu kwa Wakulima alielezea matarajio yake kuwa iwapo  wakulima watakubali kujinga kwa wingi na kilimo cha Shadidi, Zanzibar inaweza kupunguza kwa asilimia kubwa kuagiza mchele kutoka nje.

Aliongeza kuwa kilimo cha Shadidi, kinacholimwa kwa vipindi viwili kwa mwaka, kilianza mwaka 2016 na wakulima 85 waliopatiwa mafunzo Unguja na Pemba wanaendelea kulima kwa mafaniko makubwa.

“Tumeweza kutoa elimu kwa wakulima wa kilimo cha Shadidi Unguja na Pemba kwa lengo la kukiimarisha zaidi na tumeanza kupata mafanikio”, alisema Afisa huyo.

Sada Seif alieleza kuwa wakulima wa kilimo cha Shadidi wanatumia mbegu na maji kidogo na kinauwezo wa kutoa polo 60 za mpunga kwa eka moja wakati kilimo cha kawaida kinazalisha polo 32.

Aliongeza kuwa kilimo cha Shadidi kinachuka muda mfupi zaidi kuanzia wakati wa kupanda mbegu, ukuaji hadi kufikia wakati wa kuvuna tafauti na kilimo cha mpunga wa kawaida.

Aidha  alieleza kuwa tayari Wizara ya Kilimo, Mali Asili, Mifugo na Uvuvi imeshatoa mafunzo ya kilimo cha hicho kwa Jeshi la Kujenga Uchumi  Upenja ili kukiendeleza na kufikia lengo la kujitosheleza kwa mchele Zanzibar.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...