Fatma Salum- MAELEZO

TRENI ya kifahari inayojulikana kwa jina la ROVOS ambayo ni miongoni mwa treni tatu bora duniani imewasili jijini Dar es Salaam kwa kutumia reli ya Tazara ikiwa na watalii 64.
Watalii hao wamekuja Tanzania kwa ajili ya kutembelea maeneo mbalimbali yenye vivutio vya utalii hapa nchini ikiwemo mbuga za wanyama na visiwa vya Zanzibar.
Akizungumza katika hafla fupi ya kuwapokea watalii hao iliyofanyika stesheni ya TAZARA Dar es Salaam, Meneja Mkuu wa TAZARA Tanzania, Fuad Abdallah alieleza kuwa treni hiyo iliondoka mji wa Cape Town nchini Afrika ya Kusini Agosti 18, mwaka huu. “Watalii mbalimbali huja nchini mara tano kwa mwaka kwa kutumia ROVOS kupitia reli ya TAZARA na nchi yetu hunufaika na ujio huu hasa faida za kiuchumi,” alisema Fuad. Aidha alibainisha kuwa treni ya ROVOS ni miongoni mwa treni tatu bora duniani, hivyo ujio wa treni hiyo na watalii unatokana na vivutio bora vya utalii na miundombinu mizuri ya reli ya TAZARA. “Treni hii inatumia reli ya TAZARA kuleta watalii kwa sababu nchi yetu imekidhi vigezo vya utalii na reli yetu imekidhi vigezo vya usalama na mawasiliano ya uhakika,” aliongeza Fuad.  Alisema kuwa katika safari hiyo ya treni watalii hao pia walipata fursa ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Selous iliyopo kusini mwa Tanzania na kuona wanyama mbalimbali wanaopatikana kwenye hifadhi hiyo. Wakizungumza kwa furaha ya kuwasili Tanzania, watalii hao wa kijerumani walisema kuwa wamefurahia sana safari hiyo na mapokezi mazuri ya watanzania na kuahidi kurudi kwa mara nyingine. Kwa upande wake mfanyakazi wa treni ya ROVOS, Monica Rieder mwenye asili ya Ujerumani alisema kuwa amewahi kufika Tanzania mara 14 na anavutiwa na mabadiliko makubwa ya kimaendeleo yanayofanyika hapa nchini siku hadi siku. TAZARA ni shirika la reli ya pamoja ya Tanzania na Zambia iliyoanza mwaka 1976 na inamilikiwa kwa asilimia 50 kila upande.


 Meneja Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania na Zambia (TAZARA) Fuad Abdallah (kulia), akizungumza na Waandishi wa Habari katika makao makuu ya shirika hilo Jijini Dar es Salaam kabla ya kuwasili kwa treni ya kitalii ya ROVOS kutoka Afrika ya Kusini.
 Baadhi ya watalii kutoka Ujerumani wakifurahia buradani ya bendi ya Polisi baada ya kushuka kutoka kwenye treni ya ROVOS moja kati ya treni ya kifahari duniani, watalii hao wamekuja nchini kutembelea vivutio mbalimbali.
 Mama wa Kijerumani Linde Erdmann (katikati) akifurahia kuwasili Tanzania kwa mara ya kwanza akitokea Afrika ya Kusini kwa kutumia treni ya ROVOS kupitia reli ya TAZARA.
Moja ya mgahawa unaopatikana katika treni ya kifahari ya ROVOS iliyowasili leo hapa nchini ikitokea Afrika ya Kusini kupitia reli ya TAZARA.
(Picha na Paschal Dotto- MAELEZO).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...